Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nichukue nafasi hii kuweza kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi ninayo maswali kwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha. Tunataka tujue, Jeshi lina madeni makubwa sana linayodaiwa na watu waliohudumia Jeshi. Sasa sifahamu ni lini Serikali itaweka pesa tunazozipitisha hapa Bungeni na kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kwenye Wizara hii kuweza kutimiza majukumu yao? Leo hii mnajinasibu kwamba mnahitaji Jeshi lisiaibike, lakini wakati huo huo shilingi bilioni 200 lakini mnatoa chini ya asilimia 14. Sielewi mnaongea nini na mnafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tunafahamu Kiwanda cha Nyumbu ni sehemu ambayo Tanzania yetu ingweza kujivunia, wanatengeneza magari, lakini ukifika pale utashangaa sana mashine ni toka Nyerere yupo, alipokuwa akitegemea mkonge na sasa tuna dhahabu. Mnasema Tanzania ya viwanda, kwa nini tusiwekeze kwenye jeshi pale upande wa nyumbu tukaona hiyo dhamira ya viwanda ikitekelezwa kwa kutumia jeshi lile? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pale vifaa havifanyi kazi, mashine ni mbovu, lakini pesa bado ni ndogo. Ndugu zangu mimi ninaomba tuache siasa katika mambo ambayo ni ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huohuo wanajeshi hawa, amezungumza aliyepita, unawezaje kuhamisha wanajeshi ukawaleta, ni kweli wao wanatii, wakati wa kuhama unaambiwa uondoke asubuhi unaondoka, lakini ni lazima tufikirie hawa watu wana familia zao! Mheshimiwa Waziri utakapokuja kutujibu, utuambie ni lini wanalipwa, kwa sababu si kweli kwamba tunasubiri bajeti hii; kama pesa ni za bajeti iliyopita lazima utuambie wanalipwa lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapinga UKIMWI kama Taifa, leo mwanaume mwanajeshi yuko Dodoma, familia yake iko Dar es Salaam, hajui anarudije kwa sababu kazi zao zinaenda kwa order, usipompatia hela unataka nini? Mke wake kule atatafuta mtu, atatafuta mbadala na yeye huku atatafuta mbadala. Kwa hiyo, ninaomba walipwe sawa sawa na stahiki yao wanayotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jeshini kulikuwa kuna maduka ambayo yana punguzo la bei, lakini tunaambiwa kwamba yale maduka yamefungwa. Wanajeshi hawa hawana muda wa kufanya biashara, wanahitaji kupata incentives, kumuwekea duka lenye bei nafuu ni kumtia moyo wa utendaji kazi. Sasa sijajua hizo bajeti na jinsi ya kufunga mikanda kama kunafika hadi kwenye Jeshi, tukifika hapo nchi inaangamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kauli zinasemwa na Waheshimiwa Wabunge wengine, sitaki kuwataja umekataza, tunapozungumzia haki sisi sio Wazambia, sisi ni Watanzania, ni wazawa, tunazungumzia mustakabali wa Taifa hili bila kupendelea. Si sawa kutuona sisi ni magaidi tunapozungumzia na kusema tunawachonganisha wanajeshi na wananchi, kwani wanajeshi hawajui kama wao wanakosa haki zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna haki ya kuzungumza pasipo kupendelea; na msijifiche kwenye kichaka cha kwamba sisi ni wapinzani, tunayo haki, tunalipwa mshahara sawa na ninyi na lazima tulalamike na lazima msimamie haki na muifanye kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi linajitahidi sana kutetea Taifa letu, lakini ijapokuwa hii inahusika na miundombinu pia, kwenye mipaka yetu madaraja ni mabovu. Leo hii tukipata shida kama nchi mimi nakwambia hivyo vifaru ambavyo wanavyo kwa kupitisha hawana. Sasa hapa Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi uonane na Waziri wa Miundombinu uone ni jinsi gani utaweka mipakani madaraja. Kule kwetu Kyela madaraja ni mabovu, Malawi wameonesha chokochoko kuja kwetu, je, wakifanya kweli, tunapita wapi? Ninaomba unapokuja kuhitimisha ujaribu kuliweka hili wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vijana wanafanya kazi ya ulinzi kwenye SUMA JKT, mishahara wanayopata ni midogo. Sote tunajua kuna makampuni ya ulinzi yanalipa hadi shilingi 500,000 wafanyakazi wao, vijana hawa wanapata chini ya shilingi 200,000, mimi nafikiri si sawa. Ninaomba Mheshimiwa Waziri kwa bajeti inayokuja ufikirie jinsi gani vijana wale wataongezewa mshahara. Na ninaomba pia na ninashauri kama ikiwezekana makampuni binafsi mengine yapunguzwe, ili tuongeze idadi ya vijana kwenye JKT na kuchukua tender, ikiwezekana zote kwenye Serikali, lakini pia hata makampuni binafsi tulazimishe wachukue SUMA JKT. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi pamoja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.