Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Peramiho
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia Waheshimiwa Wabunge wote uzima na afya njema kiasi cha kutuwezesha kukutana tena leo katika ukumbi huu kwa majukumu yetu ya Kibunge lakini kwa manufaa ya Watanzania wote ambao tunawawakilisha ndani ya Bunge hili kwa ujumla wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Meza na Kiti chako ili kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge zinazohusiana na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu toka nilipoteuliwa na Mheshimiwa Rais wetu kwa wadhifa huu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia mambo ya Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa dhamana hii kubwa. Naamini kabisa kwamba sote tunafahamu uzito wa majukumu ya kuwatumikia wananchi na umma mzima wa Watanzania. Naahidi kwamba nitajitahidi kutenda kazi zangu zote kwa moyo wote ili kuleta maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kwa dhati kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na miongozo mbalimbali anayonipa katika kutekeleza majukumu yangu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika kipindi hiki kifupi cha Serikali ya Awamu ya Tano. Toka nimeingia madarakani nimeona kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu amesheheni umakini mkubwa wa uongozi na uongozi usioyumba katika kusimamia, kufuatilia masuala ya msingi yanayohusu maslahi ya umma. Ni mchapakazi na ni muadilifu katika uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwa dhati niwashukuru sana Manaibu Waziri wawili, Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Dkt. Possi kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu. Nimeamini hawa Naibu Mawaziri wawili kwa kweli ni vijana ambao ni ma-caterpillar wenye uwezo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru pia Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi na viongozi wa taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa na ushirikiano ambao wamekuwa wakinipa katika kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa dhati pia niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Peramiho kwa kunichagua lakini kwa kuendelea kuniunga mkono katika utekelezaji wangu wa majukumu haya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii ambayo inanifanya leo kuja kuhitimisha hoja hii mbele yako isingeweza kufikia mahali hapa kama si Wajumbe wa Kamati mbili za Kudumu za Bunge ambao walifanya kazi ya umakini katika kupitia mapendekezo ya bajeti yetu na kuifanya bajeti hii iweze kuja hapa mbele yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, Ndugu yangu Mheshimiwa Mchengerwa na Naibu wake dada yangu Mheshimiwa Giga na Wajumbe wote wa Kamati ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano mkubwa waliotupatia wakati wa kuchambua bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya UKIMWI wakiongozwa na Mheshimiwa Mwenyekiti Hasna Mwilima na Makamu wake Mheshimiwa Kanyasu na Wajumbe wote kwa kazi kubwa waliyoifanya na ushirikiano mkubwa waliotupatia katika kuhakikisha kwamba tunafanikiwa katika kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe mwenyewe umejidhihirisha kwamba umekuwa kiongozi mahiri wa kuliongoza Bunge letu pamoja na Wenyeviti wa Bunge na Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge. Kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, napenda niwapongeze, niwashukuru na niwatakie kila la kheri katika kutekeleza majukumu haya mazito wakiwemo Makatibu wanaotuhudumu katika Kamati mbalimbali za Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 99(2) ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inayohusu kujadili utekelezaji wa bajeti za Wizara, naomba sasa kwa heshima na taadhima uniruhusu nitoe ufafanuzi katika maeneo mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyachangia na kutaka kupata ufafanuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachukua maeneo machache na maeneo mengine Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja mbele hapa leo wakati wa kuhitimisha hoja hii basi atayatolea ufafanuzi wa kina.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokwenda kutoa ufafanuzi wa maeneo haya, nawashukuru sana Wabunge wote waliochangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hasa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ambao walishiriki kikamilifu na kwa ufanisi katika kuchangia mapendekezo ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa huu wa fedha wa 2016/2017. Niwahakikishie tulikuwa wasikivu na tumeyachukua maoni na ushauri wenu na kama yote hayatajibiwa ipasavyo hapa basi Ofisi yangu itafanya utaratibu wa kuyajibu kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge mtaweza kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kujibu hoja hizi pia kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, nitoe pole sana kwa maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania waliokumbwa na maafa ya mafuriko. Tumekuwa tukishuhudia katika Bunge letu na sehemu nyingine, maeneo mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania yamekumbwa na mafuriko makubwa na Watanzania wengi wamejikuta wakihangaika na hii yote ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mvua zilivyonyesha kwa wingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kushirikiana na Kamati zetu za Maafa, lakini tuendelee kuwaagiza viongozi wote katika maeneo mbalimbali wahakikishe wanaendelea kuchukua tahadhari na hasa kuwahamisha wananchi katika maeneo hatarishi ili kuweza kuepusha majanga ya maafa katika kipindi hiki ambacho utabiri unaonyesha tutakuwa na mvua nyingi sana zinazoweza kupelekea kupatikana kwa maafa mengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kujibu hoja hizi, nianze na hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wenyeviti wa Kamati zote mbili, nikianza na hoja zilizotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria alituagiza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kubaini tuhuma zilizotolewa katika miradi ya NSSF na kuchukua hatua za kisheria za kuwawajibisha watu wote waliohusika katika kadhia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakubaliana na ushauri huo wa Kamati, ripoti ya hesabu za Serikali imeshatolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndani ya Bunge. Kwa hiyo, kwa kufuata taratibu zile zile za kikanuni lakini taratibu za Serikali za kufuatilia ripoti hiyo, Serikali inaahidi kwamba italifanyia kazi suala hilo kwa namna yoyote ile itakayowezekana ili kuendana na agizo la Kamati kama lilivyowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia SSRA kwa kushirikiana na Benki Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 39 kikisomwa pamoja na kifungu cha 40 na 48 cha Sheria Na.8 ya mwaka 2008, Sheria ya SSRA itaendelea kufanya ukaguzi maalum kwa maana ya special inspection kwenye vitega uchumi vyote ndani ya Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Sheria Na. 8 ya mwaka 2010 ilianza kutumika mwezi Septemba 2010. Sheria hiyo iliyomuunda Mdhibiti Mkuu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ililetwa kwa maana halisi ya kuondoa migongano ya kisheria katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini vilevile ilitaka kuweka sera jumuishi za uwekezaji ndani ya mifuko hiyo na ilitaka pia kusimamia suala zima la kuongeza wigo na ufinyu wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi ya pekee, naomba nimpongeze sana Mkurugenzi Mkuu wa SSRA dada Irene kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika kusimamia sekta yetu ya hifadhi ya jamii nchini. Na sisi kama Serikali tutaendelea kumpa ushirikiano na niwaombe Waheshimiwa Wabunge mnaweza kumtembelea na kupata ushauri mara zote bado anaendelea kusimamia sekta hii vizuri na kwa uadilifu wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo lingine lilikuwa ni SSRA iendelee kusimamia na kuchukua hatua kali kwa waajiri ambao hushindwa kuwasilisha michango ya wanachama wakiwemo waajiri wa sekta binafsi na taasisi za Serikali. Kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria Na. 8 ya mwaka 2008, SSRA ina wajibu wa kutekeleza na kulinda maslahi ya wanachama wote katika mifuko yetu.
Hata hivyo, SSRA imekuwa ikijikuta wakati mwingine ikipata shida katika kusimamia suala zima la kuwalazimisha waajiri kuhakikisha kwamba wanapeleka michango yao kwa wakati katika mifuko hii ya hifadhi ya jamii. Hivyo basi, SSRA kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu tumeandaa rasimu ya mabadiliko ya Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 kwa lengo la kuipa nguvu SSRA ipate meno ya kuhakikisha kwamba waajiri wote wanakusanya michango na kuifikisha kwenye Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati na kuondoa usumbufu kwa wanachama wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati iliiagiza Serikali ichukue hatua za dhati na za makusudi kuboresha mitambo na mazingira ya Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali ili kuiwezesha idara hiyo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kibiashara. Tunayo mipango ya muda mrefu na muda mfupi katika kuhakikisha kwamba tunaboresha Idara hiyo ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali. Kwa sasa tumeamua kabisa kuyatambua mazingira hayo magumu ya Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali na tumeamua kwa haraka kuanza kuchukua hatua za dharura za kukarabati mitambo yote ambayo ilikuwa imenunuliwa na bado inaweza kufanya kazi nzuri ya kuweza kurahisisha kazi katika kiwanda hiki. Tumejipanga kwa mpango wa muda wa kati na muda mrefu ili kuhakikisha tunaendelea kuboresha mazingira na majengo ya kiwanda hicho. Vilevile kwa kushirikiana na taasisi za Serikali ikiwemo Benki ya TIB na taasisi nyingine tumeamua kufanya kazi kwa pamoja ili kuboresha kiwanda hicho. Pia tuna mpango wa kujenga kiwanda kingine katika Makao Makuu ya nchi hapa Dodoma ambacho kitakuwa cha kisasa na kinaweza kukidhi mahitaji ya Taifa na tayari Serikali imepata ekari tano za kuweza kujenga kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliagizwa pia kwamba Serikali ijitahidi kadiri inavyowezekana kuboresha huduma za maafa ili kuiwezesha Serikali kutoa misaada ya haraka pindi maafa yanapotokea katika nchi yetu ya Tanzania mahali popote. Serikali imeanza kuchukua hatua za dhati kabisa kuhakikisha tunaboresha huduma za Idara ya Maafa katika nchi yetu ya Tanzania. Hii ni pamoja na kupitishwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 7 ya mwaka 2015.
Pamoja na kazi hizi tunazozifanya, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi anayesimamia Idara ya Maafa nchini kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha kwamba kwa resources hizo ndogo tulizonazo lakini shughuli hii imeendelea kufanyika kwa ufanisi na Waheshimiwa Wabunge wengi walisema na kumpongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo sheria hiyo inaweka maagizo mbalimbali ya kisheria yanayotakiwa kufuatwa ikiwemo kuanzishwa kwa Kamati za Maafa katika ngazi ya Kata, Wilaya, Mikoa. Kamati hizo zinaweza kutoa mchango mkubwa wa awali katika kusimamia suala zima la maafa pale yanapotokea na kutambua pia viashiria hatashiri ili kuchukua hatua kama vile kuwahamisha watu katika maeneo yanayoonekana ni hatarishi na hasa wakati wa masika kama inavyotokea sasa.
Waheshimiwa Wabunge, niwaombe sana tuendelee kushirikiana na viongozi wenzetu na hasa wale viongozi wa Kamati za Maafa katika maeneo yetu ili kusaidiana kuhakikisha kwamba ama tunatoa taarifa mapema majanga haya yanapotokea ama tunachukua nafasi ya kushauri kuchukua tahadhari katika maeneo mbalimbali ili kupunguza maafa katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengine waliomba Serikali iongeze fungu kwa ajili ya Idara hii ya Maafa. Serikali imeendelea kuweka fedha kwa Idara hii ya Maafa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti. Vilevile tumeendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Wizara na taasisi nyingine ili kuhakikisha vifaa vya misaada ya maafa katika nchi nzima vinapatikana. Serikali imeweka maghala mbalimbali kwa ajili ya huduma hii katika mikoa mbalimbali nchini kwa kuzingatia kanda. Serikali pia imejiandaa na inaendelea kufanya tathmini ya majanga yaliyokwisha kutokea, imeendelea kuwafundisha wataalam mbalimbali mbinu na namna bora za kukabiliana na maafa na majanga mengine nchini ili majukumu haya yaweze kusimamiwa vema na Serikali yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuliagizwa pia na baadhi ya Wabunge waliochangia na vilevile Kamati ya Katiba na Sheria ya kwamba Serikali ichukue hatua za makusudi kukamilisha haraka ujenzi wa jengo la makazi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa Dodoma. Naomba kulihakikisha Bunge lako Tukufu kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa makazi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, yanayojumuisha nyumba na makazi ya Waziri Mkuu, ofisi binafsi na nyumba ya wageni imekwishakamilika na kukabidhiwa Serikalini tarehe 19 Februari 2016. Awamu ya pili ambayo itajumuisha ujenzi wa uzio, barabara, mandhari, nyumba za walinzi, wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu na uwekaji wa samani ikiwemo ujenzi wa barabara. Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ulitolewa wito na Wabunge kadhaa ndani ya Bunge lako ya kwamba Serikali iboreshe huduma za malipo kwa wastaafu wakati wa kustaafu na kusiwe na mapungufu na kadhia nyingine kwa wastaafu wanapomaliza muda wao wa kazi. Hadi kufikia Juni 2015, idadi ya wastaafu wote kwa kila mfuko wa pensheni katika nchi yetu ya Tanzania wale ambao walikuwa wamekwishalipwa kupitia Hazina ilikuwa ni wastaafu 89,532. Aidha, utaratibu wa kuhakiki wastaafu kwa mifuko yote hufanyika kila mwaka kwa lengo la kubaini mahali walipo na kama tayari mafao yao ya kustaafu wamekwishayapata. Serikali inaahidi kuendelea kusimamia zoezi la malipo ya pensheni kwa wastaafu kwa utaratibu unaotakikana mara kwa mara ili kupunguza kadhia ya hii kubwa wanayoipata wastaafu wetu katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo lingine lilikuwa Serikali iweke utaratibu wa pensheni ya wazee wote hata wale ambao hawakuwa wakifanya kazi katika sekta rasmi. Agizo hili Serikali imelipokea na agizo hili limewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rasimu ya andiko la Mpango wa Pensheni kwa Wazee wote na Watu Wenye Ulemavu imekwisha kukamilika. Hatua inayofuata kwa sasa ni ushirikishwaji wa wadau na taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mpango huu ili mara tutakapokuwa tumekubaliana na wadau wote tuanze sasa kujipanga ndani ya Serikali na kulipa pensheni hii kwa wazee wetu kama ilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi pia walishauri elimu ya hifadhi ya jamii itolewe ili watu wengi zaidi wajiunge na mifuko hiyo. Naomba niwahakikishe Waheshimiwa Wabunge kwamba wigo wa hifadhi ya jamii katika nchi yetu ya Tanzania umeendelea kupanuka ingawa siyo kwa speed kubwa. Mpaka sasa takribani asilimia 8.8 ya nguvu kazi ya Taifa imeshajiunga katika Hifadhi ya Jamii ingawa asilimia hiyo bado ni ndogo. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 ya SSRA kazi kubwa nyingine ambayo imekuwa sasa ikifanywa na SSRA ni kuhakikisha inachukua jukumu hilo la kuanza kutekeleza mpango mkakati wa kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii nchini yaaani Social Security Extention Strategy. Hii ni pamoja na kuweka mkakati wa mawasiliano yaani Social Security Communication Strategy kwa makundi mbalimbali kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili kufikia lengo hilo. Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba Watanzania wengi na hasa vijana waliopo katika sekta isiyo rasmi wanaingia katika mfumo huu wa pensheni ili kuweza kuwaandalia maisha yao ya baadaye kwa namna moja au nyingine.
Serikali iliwezesha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi kushughulikia masuala ya wafanyabiashara wadogowadogo wakiwemo bodaboda, akina mama lishe na wajasiriamali. Sheria ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi ilitungwa mwaka 2004 na Sera ya Baraza hilo ilitolewa mwaka 2004. Kwa sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshazindua mpango mkakati wa utekelezaji wa kazi za Baraza hili lakini vilevile ameshazindua uanzaji wa utekelezaji wa shughuli hizi za Baraza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi Baraza limeshaanza kutengeneza programu kupitia NSSF na Baraza lenyewe na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa waendesha bodaboda katika SACCOS 16 za bodaboda katika Mikoa ya Dae es Salaam, Arusha, Mbeya, Dodoma, Kigoma, Tanga, Rukwa, Mara na Geita lakini kazi hii itaendelea katika mikoa mingine. Naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi anayesimamia sekta hii Dada Beng‟i Issa kwa kazi nzuri anayoifanya na jinsi alivyojipanga kuhakikisha anatusaidia kujibu tatizo la ajira kwa vijana kupitia mpango huu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kukuarifu kwamba kwa sasa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania, limeanza pia kutoa mafunzo maalum kabisa kwa vijana wetu wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Tunafahamu vijana wetu wengi pia wanajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa na wanapomaliza mafunzo yao wengi wamekuwa wakikosa kuajiriwa. Baraza limeshaanza kuwafundisha viongozi katika makambi mbalimbali ya Majeshi yetu ya Kujenga Taifai ili wanapowafundisha vijana wetu katika mafunzo ya kijeshi wawafundishe jinsi ya kuunda vikundi na kupatiwa mikopo ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wote wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini kwa ushirikiano mkubwa na jinsi walivyopokea wito huu wa kuwasaidia vijana wetu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza pia linasimamia mpango wa akiba na mikopo kupitia VICOBA na SACCOSS. Niendelee kuwaomba vijana wengi wajiunge kwenye mipango hiyo ya akiba na mikopo lakini na VICOBA ili tuanze kuwaweka katika mifumo ya kukopesheka na kuwasaidia kujiajiri na kuwaajiri wenzao pale wanapoanza kufanikiwa katika mipango tuliyojiwekea. (Makofi)
Mchango mwingine ulihusu miradi ya MIVARAF katika nchi yetu ya Tanzania. Mchango huu uliletwa na Mheshimiwa Edwin Ngonyani na Wabunge wengine. Naomba niwathibitishie kwamba mradi wa MIVARAF utafika katika maeneo yote ambayo yamekwishapangwa. Naomba niahidi mbele ya Bunge lako Tukufu tutawashirikisha Wabunge wote wanaohusika na mradi huu ili wajue miradi inayofanyika katika maeneo yao na watupe ushirikiano wa kuifuatilia na kuitizama inavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni hoja iliyotolewa na Kamati ya Mapambano dhidi ya UKIMWI, ikiomba Serikali kutenga fedha ya kutosha kwa Tume ya Kudhibiti UKIMWI na Dawa za Kulevya. Agizo hilo limezingatiwa na kama mlivyoona Serikali imeanza sasa kuweka fedha kwenye Mfuko Maalum wa kisheria katika mapambano dhidi ya UKIMWI. Takribani Watanzania 670,000 kwa sasa wanaishi kwa kutumia dawa lakini waliopimwa na kugundulika wanaishi na Virusi vya UKIMWI, ni takribani Watanzania 1,500,000. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba tunafanya kazi ya kutosha katika eneo hilo. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa pia ni Wajumbe wa Kamati za UKIMWI katika Halmashauri zetu basi tushirikiane kuangalia fedha zinazotengwa katika eneo hilo zinatumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyotolewa ni kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini, lilitolewa pia na Kamati hiyo hiyo ya UKIMWI. Kamati ilitutaka tuhakikishe kwamba tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunapambana na tatizo hili la dawa za kulevya nchini. Naomba niwathibitishie sheria tuliyoitunga mwaka 2015 imeanza kuchukua mkondo wake na tayari adhabu kali zimeanza kutolewa kwa wale wote ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania. Sheria imetoa adhabu kali sana kwa makosa ya kujihusisha na matumizi ya biashara hiyo ambayo ni kifungo cha maisha. Sheria hiyo pia imetoa adhabu kali kwa wale wote wanaowahusisha watoto katika suala zima la matumizi ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuhakikishia Serikali inahamishia Makao Makuu Dodoma na hasa kwa kutunga sheria. Naomba niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sheria ya kuhamishia Makao Makuu ya nchi Dodoma imeshaandaliwa na imeshaanza kupita katika vikao vya kisheria vya kiutaratibu ili hatimaye tuilete katika Bunge lako Tukufu iweze kujadiliwa na kupitishwa. Tutashirikiana na Wabunge kuhakikisha kwamba zile kero ambazo zimekuwa zikitokea Dodoma kwa namna moja ama nyingine zinazohusu sheria basi zitarekebishwa kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Manaibu Waziri wangu wakijibu maswali, walizungumzia mambo mengi yanayohusu wafanyakazi, lakini vilevile yanayohusu walemavu, naomba niwathibitishie tumejipanga vizuri kukabiliana na changamoto zote za wafanyakazi katika nchi yetu ya Tanzania, kuboresha maisha yao, kuangalia sheria zile ambazo zimekuwa zikitumika kuwakandamiza katika maeneo ya kazi, tutazisimamia ili kuhakikisha sheria za kazi zinatekelezwa. Tumejipanga kuhakikisha kwamba suala zima la walemavu tunalipa kipaumbele katika Ofisi ya Waziri Mkuu, tutalisimamia na kutoa ushirikiano na hivyo kuhakikisha dhamira njema ya Serikali katika kuwajali na kuwahudumia walemavu katika nchi yetu ya Tanzania inafikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza kutoa majibu haya ya awali na kumpisha Mheshimiwa Waziri Mkuu aweze kumalizia majibu mengine yaliyobakia, nitumie nafasi hii kuwatakia wafanyakazi wote maandalizi mema ya sherehe za Mei Mosi ambazo zitafanyika Kitaifa katika Mkoa wa Dodoma. Sisi kama Serikali tunawahakikishia kwamba tupo pamoja nao, tutashirikiana nao na tutaendelea kufanya kazi nao kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi yetu kama vile tunavyofahamu wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba kwa heshima na taadhima nichukue nafasi hii tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nikirudia kuanza na Wabunge Wajumbe wa Kamati zote mbili lakini na Wabunge wote waliochangia hapa ndani ya Ukumbi wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja.