Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kusimama kwenye Bunge lako Tukufu kwa ajili ya kuchangia mjadala wa Wizara ya Ulinzi na Usalama. Kwanza nilipongeze Jeshi letu kwa kazi ambazo linazifanya, kwa kweli ni kazi zilizotukuka na zinastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite moja kwa moja katika suala la ulinzi na usalama. Mimi natoka Ludewa ambako Ziwa Nyasa lipo na kama kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani kwenye ukurasa wao wa 14 na 15 walizungumzia juu ya mgogoro wa Ziwa Nyasa. Labda tu nipende kuweka vizuri taarifa yao kwamba Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu; limezungukwa na Tanzania, Malawi na Msumbiji. Kwa hiyo, katika hali ya kawaida Malawi hawezi ku-demand eneo la Msumbiji, analo-demand ni eneo la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulinzi na usalama eneo lile ni pana hasa eneo la upande wa Ludewa. Eneo la upande wa Ludewa bado ninaendelea kusisitiza kwamba lina urefu wa kilometa zisizopungua 250 around the shore of the lake, lakini kiusalama na kiulinzi bado limewekwa nyuma. (Makofi) (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukijaribu kuangalia eneo lote hilo lenye urefu huo mkubwa bado hakuna vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vipo huko. Napenda kuchukua tu fursa hii kuliomba jeshi, kuiomba wizara na kumuomba Mheshimiwa Waziri kwamba kuna haja ya kuweka mkakati wa makusudi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumza hivyo? Nazungumza hivyo kwa sababu eneo lile halina mawasiliano ya simu; eneo hilo halina miundombinu ya barabara kwa urefu wote huo niliokua nimeuzungumza. Kwa hiyo basi, ifike mahali sasa kwa sababu ya haya mambo yanayoendelea hapa sasa hivi inakuwa ni ngumu sana incase ikitokea kitu chochote wananchi kuripoti, incase kuchukua kitu chochote, wananchi hata kukimbia basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ikizungumzwa kwamba hapa pana mgogoro na ilifika mahali kipindi kile yanachimbwa mafuta, unakuta ndege ya Malawi inakuja Tanzania na wananchi hawana facilitation yoyote ya kusema kwamba wanaweza wakaripoti. Kwa hiyo, ina maana kuwa kama litatokea janga lolote uwezekano ni mkubwa sana kwenda hayo maeneo na ukakuta kwamba mambo yameshaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napende tu kuisihi Wizara ikiwezekana sasa na kama itakuwa imeruhusu basi kuwepo na vyombo vya kiulinzi ambavyo vina-patrol, angalau kuwepo hata na marine boats ambazo zitakuwa zinazungukia kule kwa ajili ya kuimarisha usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naweza kulizungumzia ni juu ya Uwanja wa Ndege Sagalu, uwanja ule ni wa Jeshi lakini kwa mara ya mwisho inaweza kuwa ni miaka 30 iliyopita, ule uwanja umeshakuwa ni pori. Sasa kwa sababu kuna ujio wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga naamini kabisa facility ya uwanja ni muhimu. Labda twende kuliuliza Jeshi kwamba incase kama utakuwa hauna matumizi kwa sasa, turudishieni Halmashauri ili tuweze kuandaa mazingira ya kufanya kazi nyingine yoyote ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kusema hivyo basi naamini; tuna kambi moja ya Jeshi pale Manda ambayo ipo mpakani kabisa mwa Mto Ruhuhu. Sasa ukiangalia lile eneo lote mpaka unakuja unaigusa Kyela hakuna chombo chochote cha ulinzi, hakuna mawasiliano ya simu na hakuna mawasiliano ya miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, nichukue tu nafasi hii kuishauri Serikali kwamba ipeleke vyombo vya usalama kule angalau basi hata wananchi wafarijike incase kama kitatokea kitu chochote waweze ku- accommodate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho ningependa kukizungumzia hapa ni juu ya dhana ya viwanda kwa Jeshi. Ifike mahali sasa Jeshi letu lijiendeshe kisayansi, kwa sababu ninaamini kwamba Jeshi letu lina multi professionals, lina madaktari na ma-engineer. Kwa hiyo nalo lipange mpango mkakati na ifike mahali jeshi lenyewe kama Jeshi lijitegemee na lisiwe inategemea ruzuku tu peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ninaamini kabisa jeshi lina uwezo wa kujiendesha kisasa kama ilivyoanza ule Mradi wa Nyumbu bado unaweza likaanzisha miradi mingine yoyote ambayo inaweza ikaliingizia kipato japo kwamba litaendelea kupata ruzuku kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache mimi niishie hapo, ila napenda tu kwa dhati ya moyo wangu, eneo lile la Ziwa Nyasa sasa hivi lipewe kipaumbele kwani wananchi wameamua kulima barabara wenyewe. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara ya Ulinzi maeneo ambayo ni magumu basi tutakapoomba baruti watuletee, na maeneo ambayo yana madaraja ikiwezekana basi tupate hayo madaraja. Kuna baadhi ya maeneo Jeshi huko nyuma lilishaweka madaraja; sasa bahati nzuri maeneo yale imeshapita barabara yale madaraja yanakuwa sasa hivi ni kama hayana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tungeomba sisi tutakapokuwa tunaomba yale madaraja basi tuletewe kwa ajili ya kufanya facilitation ya wananachi wetu kule ili paweze kupitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.