Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa kutoa masikitiko yangu katika maeneo mawili tu. Moja ni suala la kutumia vibaya Jeshi letu la Ulinzi (JWTZ). Si sahihi hata kidogo kwa jeshi letu kutumiwa kuvuruga shughuli za kidemokrasia nchini hasa chaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya na ya kutisha Zanzibar. Binafsi nilipata fursa ya kuwa Zanzibar wakati wa uchaguzi mdogo wa marudio Jimbo la Dimani. Nilishuhudia malori ya JWTZ yaliyobeba “mazombi” watu waliovalia sare za jeshi na soksi usoni (wakijificha) walioshikilia silaha juu yakienda na kurudi barabara ya Fumba. Kwa hakika nilishtushwa sana na tukio hili na kwa heshima kubwa namwomba Mheshimiwa Waziri akomeshe vitisho hivi na matumizi mabaya ya jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili linalonisikitisha ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kushindwa kujitegemea kiuchumi na kulisaidia Taifa. Hili ni jeshi lenye makambi karibu nchi nzima na nguvu kazi ya kutosha ya vijana wetu wanaokwenda huko karibuni muda wote. Jeshi lina mashamba makubwa, miradi ya mifugo, ujenzi na kadhalika. Ni vipi Jeshi hili lishindwe kuendesha kilimo cha kisasa na chenye tija? Waziri kwa kweli alifanyie kazi suala hili ipasavyo. Kwa wataalam wa fani mbalimbali waliojaa JKT ni aibu kubwa kuwa na jeshi la aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine dogo ninalopenda kuchangia kwa leo ni kuomba Bunge kuipa Wizara hii hadhi yake stahiki yaani kuwa Wizara ya Muungano. Kwa hadhi hii Wizara hii inastahiki kupewa muda wa kutosha kwa Wabunge kuchangia kwa nafasi badala ya kupangiwa siku moja tu ambayo inaanza kwa kipindi cha maswali na majibu. Nililisema Mkutano wa Bunge la Bajeti ya mwaka uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano na siyo la Tanzania Bara. Imekuwa ni tabia/ mazoea ya Bunge hili kutumia muda mwingi (mpaka siku tatu) kujadili masuala ya Tanzania Bara tu (Kilimo, TAMISEMI, Afya na kadhalika) badala ya masuala ya Muungano (Ulinzi, Mambo ya Nje, Ofisi ya Makamu wa Rais na kadhalika).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Waziri mhusika aipitie vizuri hotuba ya Kambi ya Upinzani, kwa uadilifu na bila hiyana kwa maslahi mapana/ya jumla ya nchi yetu na maslahi mahsusi ya walinzi wetu (wanajeshi) wa majeshi yote mawili –JWTZ na JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru na naunga mkono hotuba ya Kambi ya Upinzani na kumtakia kila la kheri Waziri wa Ulinzi kwa jukumu nyeti na muhimu alilopewa na nchi yetu.