Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Kujenga Taifa ni la Watanzania wote na inapotokea Kambi ya Jeshi inapokuwa katika kata au jimbo au vijiji naona ni fursa na faraja kwa jamii inayopakana na kambi hizo. Hali imekuwa tofauti kwa mahusiano kati ya Chita JKT ndani ya Jimbo la Mlimba, Wilaya ya Kilombero na Kata ya Mngeta, Kijiji cha Ikule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya wananchi wa Kijiji cha Ikule inasikitisha. Ni kwa miaka mingi wananchi wa kijiji hicho wanaishi na kufanya shughuli zao za kilimo kwa maisha yao yote. Hivi nichangiapo hapa na Waziri anajua wananchi wale wamenyang’anywa maeneo yote ya kilimo. Kibaya zaidi hata mazao yao ya chakula, mahindi, ndizi, mihogo, viazi, miwa, mpunga na kadhalika vyote vilifukiwa na trekta na baadhi ya wanajeshi na kuzuia kabisa kufika huko wakidai ni maeneo ya jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ingawa wananchi na viongozi wa Serikali ngazi ya kijiji waliopo na waliopita wanasema na wako tayari kuongea popote kuwa hawajawahi kuidhinisha mashamba yao waliyokuwa wanalima miaka yote kabla hata ya kambi hiyo kuwepo hapo kuwa walikubaliana katika Mkutano wa Kijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi kwamba wameridhia kukabidhi hiyo ardhi kwa jeshi. Hivi niwasilishapo, tokea mwaka 2016 Desemba hadi leo, wananchi na viongozi wa kijiji, kata akiwemo na Diwani wa Kata hiyo wapo mahabusu kwa madai mbalimbali na hawajui hatma yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuundwe Tume huru kwenda kijijini hapo kutafuta ukweli wa masuala mbalimbali yanayoendelea huko, kwani inasemekana katika vurugu za kugombania mashamba, yuko mwanajeshi aliyeuawa. Pia zipo taarifa kwamba wananchi wengi nao wameuawa (habari ambazo hazijathibitishwa) na hali ya kijijini hapo si shwari hata kidogo, kwani wakati wowote wanajeshi huingia kijijini na kukamata na kupekua nyumba, hata wakati wa usiku na kuleta mashaka kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kusema uwepo wa Kambi ya Chita ni faraja kwetu na uhakika wa kiulinzi kwa raia, isipokuwa manyanyaso ndiyo karaha kwa majirani wa Kijiji cha Ikule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipate majibu ya Serikali. Ahsante.