Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu kuyapa uwezo wa kifedha mashirika ya Nyumbu, Mzinga na SUMA JKT. Nikiwa mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama nilitembelea Nyumbu na wajumbe wenzangu na kujionea kazi nzuri inayofanywa na shirika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Shirika lingeweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kama lingekuwa huru hasa kwa mujibu wa sheria. Ilivyo sasa shirika hili kwa mujibu wa sheria liko chini ya Msajili wa Hazina hali hii inasababisha si tu mgongano wa kimaagizo, lakini pia utekelezaji wa mipango na maono (vision) ya shirika unachelewa kwa sababu ya mlolongo wa kiutawala, kwa mfano kuna nchi zilionesha nia ya kushirikiana na Shirika la Nyumbu tangu mwaka 2007, hata hivyo uamuzi haukutolewa kwa wakati kutokana na sababu za kisheria na kiutawala na hivyo kupoteza fursa hiyo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nashauri Serikali ione uwezekana wa kuleta mabadiliko ya sheria ili Shirika la Nyumbu liwe chini ya Wizara/Jeshi kwa asilimia moja. Ninaamini uchambuzi wa kina ulifanyika, itathibitika kuwa mabadiliko ya sheria yataleta tija kwa Shirika na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikufanikiwa kutembelea Mzinga kama ilivyokuwa kwa wenzangu, lakini uhalisia ni kuwa kuna fursa za wazi za kiuchumi na kimapato ikiwa Mzinga itawezeshwa, ninaamini kuna soko kubwa nje ya nchi kutokana na bidhaa zitakazozalishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu SUMA JKT, binafsi nimetembelea kila mwaka maonesho na huwa sikosi kutembelea mabanda ya SUMA JKT. Pia nimefanya ziara binafsi ya mafunzo katika Kambi ya Ruvu nikiwa na baadhi ya vijana kutoka Jimboni. Hakika iwe ni katika kilimo,ufugaji, ufundi na kadhalika, SUMA JKT inafanya kazi nzuri mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ulinzi tumeshauri mara kadhaa kuwa maeneo yote ya Serikali na taasisi za umma ulinzi ufanywe na SUMA JKT, lakini pia Serikali ihakikishe wote wanaodaiwa wanalipa kwa wakati, ikibidi fedha zao za OC zikatwe zikalipe deni. SUMA JKT ipewe wigo mpana katika kushiriki suala la kuelekea uchumi wa viwanda hasa viwanda vidogo vidogo. Hili litawezekana tu ikiwa itawezeshwa kifedha kwa namna (mechanism) ambayo Serikali itaona inafaa; kwa mfano kuidhamini kwa mikopo ya riba nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mafunzo ya vijana - JKT; katika ukurasa wa tano wa kitabu cha Taarifa ya Kamati imeeleza kuwa ikiwa fedha kiasi cha shilingi bilioni nane zitatolewa JKT itaweza kukarabati makambi na hivyo kuongeza vijana wa kujiunga na JKT. Mpaka tunajadili bajeti
hii ni kiasi kidogo cha shilingi bilioni moja tu kimetolewa. Suala la mafunzo ya JKT kwa vijana wetu ni muhimu sana kwa sababu linaongeza uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo wengi wao wanaingia katika ajira na kujiajiri. Ushauri wangu, katika wakati huu ambapo matumizi ya mitandao yamekuwa yakichangia kumomonyoa maadili ya vijana, mafunzo haya ni muhimu katika kujenga Taifa la kesho linalojitambua. Ninaamini kila kijana anayepitia JKT anajenga ushawishi (influence) kwa vijana wengine na wasiopungua 100 katika kijiji au mtaa anaoishi na kwa ushawishi huo wapo vijana waliohamasisha vijana wenzao kujiunga katika vikundi vya kuzalisha mali. Naomba kuwasilisha.