Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kupongeza Wizara hii kwa jinsi ambavyo kwa kweli wameandika vizuri, kama tungelipata muda mrefu wa kuweza kusoma hiki kitabu, nafikiri michango yetu ingepungua kwa sababu kimeandikwa vizuri sana na maeneo yote yameguswa, na ukisoma unaona kweli Serikali imedhamilia kutuingiza kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo leo kazi yangu kubwa hasa ni kushauri, lakini kabla sijaanza kushauri pia niipongeze Serikali jana nilitoa taarifa hapa kwa Waziri wa Kilimo kwamba kuna paka ameingia kule Ilula, amejeruhi zaidi ya watu saba na alikuwa anajeruhi sehemu ambazo anazijua yeye, jana timu imetumwa na kazi imefanyika, kwa hiyo, naipongeza hii Serikali kweli hapa kazi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mimi nitaenda kwenye ushauri, ukiangalia dhana nzima ya Serikali yetu tumejikita kwenye uchumi wa viwanda, walioteuliwa wataalamu kwenda kwenye Wizara ile wote ni makini, lakini kitu ambacho ninaomba ni kimoja nitatoa mfano, Wahehe mimi natoka Iringa, Mhehe na Mgogo, Mhehe akiongea Kihehe, Mgogo anaelewa na Mgogo akiongea Kigogo, Mhehe anamuelewa, tatizo linakuwa Mhehe anapotaka kuongea Kigogo na Mgogo anataka kuongea Kihehe wanapotea njia. Maana yangu ni nini, mwanasiasa ninyi wataalam wa Wizara hii ongeeni kitaalam, msianze kwenda kwenye siasa mkiongea kitaalam sisi wanasiasa tutajua mnachozungumza na sisi wanasiasa hatuwezi kuingilia kwenye utaalam wenu tutaongea kisiasa mtatuelewa, lakini tatizo linakuja pamoja na mipango mizuri tukiingiza siasa mtataka kuwa wanasiasa, mkiashaingiza siasa mipango yote mizuri itaaribika.
Kwa hiyo, naomba mjikite Mheshimiwa Mwijage nakufahamu vizuri, ulipokuwa unasoma Tosamaganga ulikuwa unaitwa kijiko cha jikoni hakiogopi moto, sasa huo moto wako kweli upeleke. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajenga viwanda, mwanzo ni ujenzi wa viwanda, unapojenga viwanda kuna vitu ambavyo unatakiwa uwe navyo ni pamoja na malighafi. Watu wa Mchuchuma ndugu yangu pale amezungumza sana tunajenga viwanda tumejitayarisha? Sasa ilikuwa ni wakati muafaka kuhakikisha chuma chetu kile tunakiandaa ili tuweze kukitumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati sasa wa kutumia malighafi nitatoa mfano mzuri, tupo kwenye ujenzi wa Makao Makuu ambapo kiasi kikubwa cha mbao zinatoka Wilaya ya Kilolo, mimi naomba Mheshimiwa Rais najua anasikiliza na anafuatilia, asilimia 75 zinatoka Kilolo na Mufindi, lakini miundombinu ya Wilaya ya Kilolo barabara siyo rafiki?
Sasa Wizara ya Viwanda naomba utoe ushauri kwa Wizara ya Miundombinu wahakikishe ile barabara inaweza kutengenezwa ili iwe rahisi kusafirisha mbao ambayo ni malighafi ya kujenga viwanda na itasaidia kupunguza gharama. Bila kufanya hivyo utakuwa hujatutendea haki. Mimi ninaomba tu Mheshimiwa Rais huko aliko anasikia siyo mbaya akiamua kuahirisha sikukuu moja zile fedha zikaenda zikajenga barabara ya kutoka Iringa mpaka Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ambalo ningependa kulisemea ni Ilula Wilaya ya Kilolo tumejenga Kiwanda cha Nyanya, lakini kiwanda cha nyanya kile nyanya tunalima sehemu oevu ambayo maji yanatuama ili tuweze kupata mazao vizuri, leo hii imekuja tafsiri mbaya sana wanasema kwamba wananchi wasilime kwenye vyanzo vya maji. Sasa tafsiri ya vyanzo vya maji Mheshimiwa January Makamba upo mimi nakuomba Jumapili nipo tayari hata kukuchangia hata mafuta uende, tatizo ni kubwa, sivyo vile ambavyo unafikiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu sasa hivi wananyanyasika tunaita kilimo cha vinyungu, Mheshimiwa Chumi amepiga kelele, Waheshimiwa wa Wilaya ya Mufundi wamepiga kelele na mimi napiga kelele, tusaidie kwa sababu tukilima nyanya ndizo ambazo tutapeleka kwenye kiwanda. Sasa hatujatengeneza miundombinu mizuri ya kuwawezesha watu wa Kilolo na sehemu nyingine waweze kuzalisha ili wapeleke kwenye kiwanda sasa hatujatengeneza miundombinu mizuri ya kuwawezesha watu wa Kilolo na sehemu nyingine waweze kuzalisha ili wapeleke kwenye kiwanda, bila kufanya hivyo uchumi utatoka wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwijage shirikiana Mheshimiwa January Makamba nami namuomba ikiwezekana kama haiwezekani toa kauli waache kuwasumbua wananchi tuweke mipango kwanza. Shirikiana na watu wa kilimo watengeneze miundombinu ya umwagiliaji lakini leo unavyosema chanzo cha maji Wilaya ya Kilolo au Mkoa wa Iringa ambao unasifika nchi hii kwa kutunza vyanzo vya maji, sasa leo unavyokwenda kuwabugudhi ni sawa sawa ukiwa na kuku anayetaga mayai ya dhahabu ukimsumbua utakosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba utusaidie katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine ambalo ningependa kulizungumza Mheshimiwa ni mpango wa SIDO. Kwa kuwa tunakwenda kwenye viwanda, tujikite sasa kuhakikisha kwamba kila Wilaya angalau tunawatayarisha watu kwa kuwa na SIDO, kama usipowatayarisha watu ambao wanakwenda kwenye utekelezaji wa viwanda usitegemee kama tutapata chochote, lakini Mheshimiwa ninakusifu, ukiangalia na ukitaka kujua kazi nzuri ya Wizara yako ukienda ukurasa wa 107 kwenye malengo mambo yote mazuri yamezungumzwa humo kwa hiyo tujikite pake tusome na wengine wanabeza hapa wanasema viwanda havipo. Nenda kwenye ukurasa wa 167 utaona orodha ya viwanda, ukishaona orodha ya viwanda ambavyo viko kila mkoa nenda kwenye Mkoa wako kaulize.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho kinatusumbua Mheshimiwa Waziri ni tafsiri ya viwanda, unaposema viwanda una maana gani, ndipo hapo ambapo kuna kuwa na ukakasi kidogo. Pia Mheshimiwa Waziri Mwijage, hivi viwanda ambavyo tunanaza kuna vingiine ambayo wanaweza kuanzisha Watanzania, leo hii ukienda pale kuna Wachina wanauza juice, wanauza ice cream wewe kama Waziri unasemaje, maana yake ni viwanda watakuambiwa ni viwanda vile. Kwa hiyo, utusaidie Mheshimiwa Mwijage vile viwanda ambavyo vinaweza kuanzishwa na Watanzania basi vianzishwe na Watanzania wenyewe bila kujali mambo yanakwenda vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la kilimo, Mheshimiwa Rais, anatuletea trekta nimesikia zaidi 2000 shirikiana na Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kuna trekta zile ambazo zilitolewa mwanzo lakini leo hii wananchi wanaanza kunyang’anywa tena, hii haipendezi, tuweke tu mkakati mzuri kwamba wananchi wanazitumia zile trekta ili tuende kwenye kilimo.
Kiwanda cha ngozi mmezungumza vizuri, kwamba leo hii wafugaji nyama haina thamani, ngozi hazina thamani, ngozi ilikuwa inauzwa shilingi 4000 leo hii kwa kilo ngozi ni shilingi 2000 hazina thamani tena, sasa tusipoelekeza nguvu yetu kwenye viwanda kama hivyo matokeo yake tutaendeleza ugomvi wa wakulima na wafugaji wakati suluhu unazo wewe Mheshimiwa Mwijage.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie habari ya migogoro ya wakulima na wafugaji, mtu ambaye anaweza akatusaidia ni Waziri wa Viwanda kwenye jambo hili, ukishirikiana na Waziri husika, tukatenga maeneo haya ni ya viwanda, haya ni ya kilimo, haya ni ya mifugo ugomvi hautakuwepo na kutoa thamani kwenye mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Nyuzi, kwa mfano Kiwanda cha Pamba huwezi kujenga Iringa na ndiyo maana nilisema siasa, unaweza ukafanya siasa kikajengwa Iringa, leo hii pale sisi Ilula mmetujengea kiwanda cha nyanya lakini bado tunahitaji kiwanda kwa ajili ya vitunguu, tunahitaji kiwanda kwa ajili ya juice na mambo mengine ili wananchi wale wapate ajira, lakini ukisema tu viwanda vijengwe halafu havina muungozo itakuwa ni shida. Pia kuna athari za viwanda kwa sababu kuna mambo ya hali ya hewa lazima kuzingatia, kwa sababu unaweza kukuta baadae tumefika mwisho hali ya hewa, mazingira yanachafuka na watu wanaanza kupata athari mbaya, sasa hilo pia uzingatie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ambalo ningependa kuzungumza ni kwamba tuangalie kwamba kiwanda hiki kinajegwa wapi na hiki kinajengwa wapi ili tuende sambamba na ukuaji wa uchumi kwa kutumia viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.