Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kupata fursa hii niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi pia niungane na Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanyia nchi yetu katika sekta ya viwanda. Kama kweli kila mtu amesoma vizuri kitabu hiki, na mimi ni mara chache sana nasoma vitabu vya Wizara, lakini katika wizara hii nadhani kwa sababu nilikuwa najua kwamba nitachangia nimesoma vizuri sana; kusema kweli nia njema ya Serikali yetu baada ya kusoma kitabu hiki ya kuhakikisha kwamba inatuvusha kwenda uchumi wa kati na uchumi wa viwanda, nina hakika tutafikiwa hasa kwa takwimu ambazo zimesheheni katika kitabu hiki cha Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu nikianza na sekta ya viwanda, katika nchi yetu. Sekta ya Viwanda ni ya kimkakati, kwa nini nasema ni ya kimkakati? Si tu inaenda kupeleka nchi yetu katika uchumi wa kati lakini inakwenda kutatua changamoto nyingi ambazo nchi yetu na wananchi wetu wamekuwa wakipigia kelele sana, nikianza na migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na wafugaji. Kama tutazingatia maelekezo ya nia ya Serikali yetu katika kutupeleka kwenye viwanda, nina hakika wafugaji wetu wanakwenda kuachana na matatizo ya kuhangaika kugombania ardhi, kunyanganyana ardhi na wakulima kwa sababu azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaenda kujenga viwanda vya nyama, ngozi, pamoja na maziwa.

Kama tutapata viwanda hivi na mazao yote yanayotokana na mifugo nina hakika kwamba wakulima wetu wanakwenda kupunguza mifugo yao maradufu na matatizo ya kuhamahama na mifugo kuhakikisha kwamba nchi yetu sasa inafuga kwa namna ambayo wana uwezo wa kupata kunufaika kwa mifugo yao na nina hakika migogoro hiyo itapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwa wakulima. Wakulima wetu wamekuwa na matatizo makubwa ya kukosa masoko. Hamasa kubwa ya mkulima ni kumuhakikishia soko. Kama viwanda vyetu vitakwenda kuchukua malighafi ya kilimo nina hakika kwamba wakulima wetu watahamasika vilivyo, watalima kwa bidii, tena kwa ubora unaotakiwa ili malighafi ambazo zitatumika katika viwanda vyetu hivi vitokane na mazao ya kilimo. Kwa hiyo, nina hakika kwamba hata umasikini wa kipato ambao bado umekidhiri baina ya watanzania, umasikini pamoja na MKUKUTA I, II, III uliokuwepo bado umebaki palepale. Tutakapogusa sekta inayowaajiri watu wengi ambayo ni kilimo na ufugaji nina hakika umaskini utapungua maradufu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nirudi kwenye point yangu ya kusema kwamba viwanda ni mkakati maalum wa kuvusha nchi yetu kuondokana na matatizo mbalimbali. Tutakuwa na biashara ya uhakika, tutakuwa tumepunguza umasikini kwa jinsi nilivyoeleza, kwa sababu sekta inayogusa watu wengi ni ya kilimo na ufugaji. Tutakuwa tumehamasisha pia vijana kujiunga na kilimo kwa hivyo tutakuwa tumeongeza ajira kwa wananchi wetu, lakini pia tutakuwa tumepunguza migogoro ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo kuhusu biashara ya utalii. Katika biashara ya utalii nchi yetu bado haijanufaika kadri ambavyo inalingana na maliasili tuliyonayo, rasilimali tulizonazo katika sekta hii. Tunayo mapori mazuri sana katika nchi yetu ambayo hayapo kule duniani, tunao wanyamapori wazuri ambao hawapo katika nchi mbalimbali, lakini nchi yetu bado haijanufaika kwa jinsi ambavyo tuna maliasili hiyo niliyotaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo amekuwa mbunifu ameona kama tutakuwa na maliasili ya aina hii, tuwe na mapori mazuri, wanyama wazuri, lakini kama watalii hawaji kwetu kuja kuangalia maeneo haya, bado hatutakuwa tumenufaika. Kwa hiyo, amekuwa mbunifu, na biashara ni ubunifu na viwanda ni mbunifu. Amenunua ndege ambazo atahakikisha watalii wetu watakuja Tanzania, watakuja kutembelea mapori niliyoyataja kwa ajili ya kuona wanyama wetu na hivyo uchumi wetu utakwenda kasi na kuhakikisha kwamba tunanufaika na sekta hiyo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kambi ya Upinzani Bungeni ukurasa wa 23 imebeza ununuzi wa ndege. Kubeza sikatai kwa sababu ni kazi yao, lakini wabeze kwa takwimu. Mimi nimeeleza kwamba huo ni mkakati kwa sababu hata Biblia inasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hayo ni maarifa ya kuhakikisha kwamba tunawaleta watalii nchini mwetu ili tunufaike na sekta yetu ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweze kutoa ushauri kwa Serikali. Tozo katika sekta hii bado ni tatizo. Watalii wakisikia kwamba Tanzania wanatoza VAT kwenye huduma za utalii, bado kuna hatari ya kupunguza manufaa tutakayopata kwa sababu atakwenda katika nchi nyingine na sisi tutabaki kulalamika. Ninaomba Serikali yangu kama si tatizo kubwa iondoe tozo la VAT kwenye huduma za utalii ili tuweze kunufaika maradufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu Benki ya Rasilimali (TIB). Benki hii iko Dar es Salaam, biashara ni mikopo, tunaomba Benki ya Biashara ifungue matawi yake katika mikoa mbalimbali ili wananchi wetu waweze kukopa, wakulima waweze kukopa ili waweze kupata mitaji ya kutosha kuweza kuendesha biashara zao. Ninaiomba Serikali yangu iweze kufikiria jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sasa Mkoa wangu wa Manyara. Mkoa wetu wa Manyara uko pembezoni na mkoa huu uchumi wake uko chini, lakini cha kushangaza ni kwamba tunayo mazao mengi ambayo mengine pia hayapo popote pale Tanzania. Kwa mfano zao la pareto, linalimwa kwa uchache sana kule kusini lakini mazao mengi ya pareto yanaozeana kwenye godown kwa sababu hakuna soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iweze kuangalia uwezekano wa kuanzisha kiwanda kule Bashnet ambako tunalima sana zao la pareto. Pareto ni zao zuri sana, dawa ya mbu ambayo ni very effective kuliko dawa zote, inaitwa expel inatengenezwa kutokana na pareto. Kwa hivyo, tunaiomba Serikali iweze kutujengea kiwanda katika Mkoa wetu wa Manyara hususan Bashnet. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunalima vitunguu saumu. Vitunguu saumu ni zao ambalo kwa kweli ubora wake sina haja ya kueleza, lakini wakulima wanalima kwa kutumia zana duni, wakulima hawanufaiki kwa sababu, masoko bado yako chini. Ninaiomba Serikali yangu katika harakati hii ya kuanzisha viwanda hasa kujenga mkoa wetu wa Manyara ambao upo pembezoni na uchumi wake uko chini lakini una rasilimali nyingi iweze kutujengea kiwanda kule Mbulu ambako tunalima zao la vitunguu saumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inashangaza kidogo, maeneo ambayo yana mifugo mingi kanda ya kaskazini mkoa wangu wa Manyara, Wilaya ya Mbulu inaongoza kuwa na mifugo mingi, Wilaya ya Kiteto, Simanjiro na Hanang, lakini cha kushangaza kiwanda cha nyama kipo Arusha. Tunaiomba Serikali na sisi Manyara iweze kutujengea kiwanda cha nyama Mkoa wa Arusha ili wananchi wetu wafugaji waweze kunufaika kutokana na mazao yao ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa msisitizo kabisa mikoa ya pembezoni kama Manyara ni mikoa ambayo inalimwa mazao mengi kama mahindi, maharage na mazao mengine ndiyo maana bodi nyingi za mazao yameanzishwa, bodi ya korosho, bodi ya katani, lakini sisi hatuna bodi huko. Lakini tunaomba recognition ya Serikali kuona kwamba mkoa wetu unazalisha mazao mengi ya biashara, tunaomba viwanda vielekezwe kule ili na sisi tuweze kunufaika na sekta hii ya viwanda na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza haya naomba kuunga mkono hoja, na nashukuru kwa kunisikiliza.