Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipatia afya na kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Pia, niipongeze Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya. Niipongeze pia Wizara hii ya Viwanda Biashara na Uwekezaji kwa kazi nzuri na jitihada zake katika kuijenga Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuanzisha programu ya kuwapa vijana 1,000 elimu ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi kutoka katika Chuo cha DIT Mkoani Mwanza na tayari 90 wamehitimu wiki iliyopita na wengine wanaendelea kujiunga na kozi hiyo. Pamoja na pongezi hizo bado ipo haja ya wanafunzi hawa kutafutiwa viwanda ambapo wataweza kufanya internship.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali yangu, kipo kiwanda ambacho kilikuwa chini ya Mwanza Tanneries cha kutengeneza bidhaa za ngozi ambacho kilibinafsishwa na mwekezaji yule hajulikani hata alipo, lakini hata mashine zilizomo mle ndani zimeshatolewa. Nipende kuiomba Serikali yangu sikivu iweze kukirejesha kile kiwanda kwa Serikali, ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kufanyia practicals, na vile vile lakini waweze kupata sehemu ya kufanyia internship na kuajiriwa kama ikiwezekana. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya uwekezaji nchini si rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje, hivyo ipo haja ya Serikali kutengeneza mazingira mazuri. Mimi binafsi na-declare interest kwamba ni mmiliki wa kiwanda cha mavazi na taulo za kike. Ninapoongea hapa ninaongea kutokana na kile ninachokifahamu, ni ukweli kwamba hatutaweza kuijenga Tanzania ya viwanda kama hatutakaa na kupitia hizi kodi na tozo mbalimbali ambazo ni nyingi na zimekuwa zikiathiri uwekezaji ndani ya nchi hii. (Makofi)



Mheshimiwa Naibu Spika, tozo hizi na kodi zimesababisha bidhaa zetu kuwa za gharama kuliko hata zile zinazotoka nje. Haiwezekani leo mfanyabisahara ambaye ananunua pamba kutoka kwa wakulima inafika hatua ana- prefer kuuza nje ya nchi kwa sababu hatalipa VAT. Pamba hiyo hiyo ikienda nje inatengenezwa nguo, nguo zinaingia ndani bila kulipa VAT, sasa inakuwaje kwamba, viwanda vyetu viuziwe kwa wafanyabiashara wale watalipa VAT na sisi pia huku ndani tuuze na tulipe VAT? Ina maana hatutaweza ku-compete na masoko ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri tunauona kwamba hata mbolea inayotoka Kenya leo hii ni ya bei ndogo ikifika nchini kuliko ile mbolea ambayo tunazalisha hapa. Kwa namna hii hatutaweza kutengeneza Tanzania ya viwanda. Suala hili liangaliwe kwa umakini kwa sababu sasa limeanza kuhamasisha wawekezaji wa ndani ya Tanzania kwenda kuwekeza katika nchi za jirani kwa sababu wanajua wakiwekeza kule wataleta bidhaa zao nchini na hawatalipa VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mashaka na kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake wote, lakini kama tunavyofahamu kwamba Wizara hii ni mtambuka na inahitaji cooperation kutoka katika Wizara mbalimbali kama ya Afya, Kilimo, Fedha, Nishati na nyinginezo. Hata hivyo bado inahitaji ushirikiano kutoka Taasisi mbalimbali za Kiserikali kama TFDA, EPZA, TIC, NDC, SIDO, NEMC na nyinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo langu hapa ni urasimu mrefu. Kumekuwa na urasimu mrefu sana katika uwekezaji wa Tanzania ambao umekatisha tamaa viwanda vingi. Kwa mfano, mwekezaji wa kiwanda cha dawa atahitaji kwenda TFDA, NEMC, atahitaji kupitia kwa Msajili wa Kampuni, ataenda TRA na kote anakokwenda kunakuwa na muda mrefu wa kusubiria matokeo ambayo anataka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuishauri Serikali kuliangalia hilo kwa ukaribu kwa sababu imesababisha sisi



kupoteza wawekezaji wazuri na wameenda kuwekeza katika nchi nyingine. Kwa mfano kiwanda cha Omnicane ambacho kilitaka kujengwa hapa Tanzania, lakini kutokana na urasimu huu na changamoto hizi nilizotaja hapo awali kimeenda kuwekeza Mauritius ambapo leo kimeajiri wafanyakazi 1,472 lakini kinazalisha umeme kutokana na makapi ya miwa gigawatts 717 ambayo ina-produce katika community inayowazunguka, lakini pia, kwa siku kina-produce sukari tani 8,500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tulicheza karata mbovu kwa kweli, kwa sababu sisi ndio tungekuwa tunanufaika na haya. Tuki-compare kwa haraka haraka viwanda vyetu vikubwa ambavyo ni Kilombero na Mtibwa kwa mwaka vinazalisha sukari tani 80,000 ambayo ni production ya siku tatu ya Kiwanda cha Omnicane. Cha kushangaza zaidi pamoja na ukosefu wa sukari ya kutosha ndani ya nchi yetu na experience hiyo ambayo nimeitoa kutokana na kiwanda cha Omnicane bado tunaendelea kuweka mazingira magumu kwa viwanda ambavyo vinataka kuanzishwa hapa vya sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri ni kule Tarime. Tarime kuna mwekezaji ambaye yupo tayari kufungua kiwanda cha sukari, lakini kumetokea vita iliyoanzishwa na Mbunge wa Tarime Vijijini ili kukwamisha kiwanda hiki kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hicho kikijengwa kitanufaisha wananchi wa Tarafa za Ingwe na Inchage ambavyo ni ambavyo ni vijiji vinne vya Biswalu, Mrito Matongo na Kijiji cha Wegita…

T A A R I F A . . .

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo siipokei kwa sababu hata wiki iliyopita wananchi wa vijiji hivyo vinne vya Biswalu, Mrito, Matongo na Wegita kijiji wanakotokea wanangu mimi Bhoke na Ryoba walikuja hapa Dodoma na mabasi mawili, wamekuja kuandamana na kuja kuonana na Waziri wa TAMISEMI. Na mimi nimekaa nao, nimepata taarifa hiyo, hata taarifa ya habari ilionesha hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki kitakapojengwa pale kitanufaisha tarafa za Ingwe na Inchage katika vijiji hivyo vinne ambavyo ni Biswalu, Mrito, Matongo na Wegita, kijiji ambacho wanangu wanatokea Bhoke na Ryoba. Pamoja na hayo yote kiwanda hiki kikijengwa kitatoa ajira kwa wananchi 15,000 lakini kitapunguza changamoto ya ukosefu wa sukari ndani ya nchi hii. Vilevile pia kitaongeza maendeleo katika vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuiomba Serikali yangu kuwa makini na suala hili iweze kuingilia kati na kusimamia, ili kiwanda hiki kiweze kuanzishwa kule Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo yote naomba niunge mkono hoja asilimia mia moja.