Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Ahmed Juma Ngwali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ziwani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza mimi nioneshe masikitiko yangu makubwa kwa Wizara ya Viwanda. Kimsingi niseme tu kwamba Kamati ya Bunge ambayo inasimamia viwanda na biashara ni Kamati ambayo inatakiwa imshauri Rais kuhusu mambo ya viwanda lakini kamati hiyo haijawahi kwenda hata gerezani kukagua viwanda wala haijawahi kwenda Kenya, China wala India; sasa sijui inamshauri vipi Mheshimiwa Waziri na viwanda vyake. Kwa hiyo, mimi nioneshe tu masikitiko yangu kwamba jambo hili si sahihi kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hasa nilitaka kuzungumzia maeneo kama mawili ama matatu na hasa nataka kuongelea Tanzania and China Logistic Centre ya Kurasini. Mara ya kwanza mradi huu ulizungumzwa katika ile China-Africa Corporation mwaka 2009 kule Cairo. Mradi huu mwaka 2012 ulianza kuingia katika Bunge na kuwashawishi Wabunge. Katibu Mkuu wa Viwanda sasa Dkt. Meru alikuwa wakati huo mimi nikiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara alikuwa haondoki katika Kamati kama vile yeye ni Mjumbe wa Kamati na kuishawishi Kamati ikubali huu mradi wa Kurasini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulianza kutathmini ile thamani ya wale watu ambao wanatakiwa kulipwa fidia, uthamini ule. Uthamini wakati huo ukawa shilingi bilioni 60, tukashawishiwa kwamba lazima tufanye uthamini haraka haraka ili muda usije ukaongezeka huyu mwekezaji akakimbia. Hata hivyo tukakaa kwa miaka mitatu baadaye, tulipokuja kulipa shilingi bilioni 60 tukaambiwa fedha zimeongezeka shilingi bilioni 40 tena. Kwahivyo, tumelipa shilingi bilioni 101 badala ya shilingi bilioni 60; lakini baadae tukaambiwa mradi huo haupo, mradi huo umekwenda wapi ooh yule mbia kaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna shilingi bilioni hizo zote zimelipwa wala huo mradi wenyewe haupo na tukashawishiwa kuambiwa kwamba mradi huu utaingiza ajira za moja kwa moja milioni 25 na ajira indirect zaitakuwa laki moja. Kwa hiyo, sisi tukaingia katika malumbano makubwa na Serikali kwenye jambo hili kutaka EPZA wapewe pesa ili huu mradi uweze kwenda. Mheshimiwa Mwijage mradi uko wapi? Mradi huna. Ukisoma huu mpango wa mwaka mmoja huoni hasa kipi ni kipi na Serikali ya China wakati ule ilisema kwamba itatoa shilingi bilioni 600 tukilipa shilingi bilioni 60, jambo ambalo mmetudanganya, hakuna kitu kinachoendelea baada ya miaka minne. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwijage nataka ujibu hasa, usije ukatuambia maneno ya ajabu ajabu, uje ujibu hasa kwa nini mradi huo haupo na fidia imetolewa na fedha zimeongezeka na lini mradi huu utaanza na upo katika mpango wa mwaka mmoja, sidhani kama katika mpango huu tunaweza kuona jambo hilo, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia Mini Tiger Plan ambao mimi nina interest kwa sababu mradi ule ikiwa utasimama basi na Zanzibar itafunguka kiuchumi. Kwa hiyo, huu ni mradi kila siku nilikuwa ninauombea dua, ulikuja nao mwaka 2002. Ule mradi ukasema kwamba una awamu mbili; awamu ya kwanza ni kulipa fidia hekta 2500 lakini tufanye kwa ujumla, mpaka sasa kumelipwa shilingi bilioni 26.6; zinahitajika kulipwa shilingi bilioni 51.1 lakini mradi haupo na baadhi ya watu 1700 wamelipwa fidia na wengine hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujua kwamba huu mradi upo? Ukitizama kitabu chenu cha Mpango wa Maendeleo ya mwaka mmoja utakuta kwamba hata huyo mwekezaji hayupo. Wakati ule tulikuwa tukiambiwa Oman na China wapo watakuja, na lakini Mheshimiwa Rais pia mwenyewe kasema kwamba hiyo sio priority yake. Pale palikuwa pana mradi wa bandari na viwanda lakini humu ndani mnasema kwamba mtajenga barabara katika eneo hilo la Bagamoyo, reli, umeme na maji. Ni reli gani itakayokwenda kule kwa mwaka mmoja? Jamani tuwe realistic katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, Mheshimiwa Mwijage utujibu, na huu mradi upo? Isije ikawa kama tulivyofanyiwa Kurasini, watu walikuwa wana deal yao wakalipwa fidia na baada ya kulipwa fidia mradi ukapotea na huku mnataka muwalipe watu fidia halafu mradi upotee kama ambavyo mmetufanyia huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, milioni 400 CBE zimetafunwa na Mkurugenzi wa Fedha pamoja na Mkuu wa Chuo. Jambo hilo alilisema Mheshimiwa Waitara mwaka wa jana hapa, lakini hakuna ripoti yoyote. Badala ya kwenda kufanya ukaguzi Dar es Salaam ambapo ndiko zilikoliwa ninyi mkaenda mkafanya ukaguzi Dodoma na Mwanza, inawezekanaje? Fedha zimeliwa kwa wengine mnakwenda kufanya ukaguzi kwa wengine…

T A A R I F A . . .

MHE. AHMED JUMA NGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea taarifa hiyo kwa upendo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende sasa katika misamaha ya kodi. Nakubaliana na alichosema jana ndugu yangu Mheshimiwa Serukamba kuhusu misamaha ya kodi na kodi ambazo zinasumbua hasa upande wa Tanzania Investment Centre. Lakini ukija sasa kwenye maeneo ya uwekezaji SEZ misamaha ya kodi ambayo ipo haina haja ya kuongezwa tena, ni mingi sana. Naomba nisome baadhi ya misamaha ya kodi ambayo inawavutia wawekezaji katika eneo la uwekezaji la SEZ. Msamaha wa malipo ya kodi ya ushuru kwa mashine, vifaa, magari ya mizigo, vifaa vya ujenzi na bidhaa nyingine yoyote ya mtaji mkubwa itakayotumika kwa madhumuni ya maendeleo ya miundombinu ya uwekezaji katika maeneo maalum ya SEZ, huo ni msamaha wa kwanza. Lakini msamaha wa pili ni msamaha juu ya malipo ya kodi kwenye kampuni katika kipindi cha miaka kumi, msamaha wa tatu ni msamaha juu ya malipo ya kodi ya zuio la kodi, gawio na riba kwa miaka kumi, msamaha juu ya malipo ya kodi ya malipo kwa miaka kumi, msamaha wa ushuru wa forodha, kodi ya ongezeko la thamani na kodi nyingine; msamaha wa malipo ya ushuru wa stamp kwenye vyombo vyote vinavyofanya hivyo na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upendeleo ya uhamiaji hadi wa watu watano katika kipindi cha mwanzo cha uwekezaji na baadae wakizingatia masharti wataongezwa; msamaha wa malipo ya VAT. Kwa hiyo, kuna misamaha katika SEZ ambayo ni mingi sana EPZA, hakuna haja ya kuongeza misamaha kwenye eneo hilo. Tuangalie zaidi kwenye TIC tujue ni namna gani tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kuhusu PVoC; tunazungumza ile Pre-shipment Verification of Conformity. Eneo hili ilipitishwa programu ya kuzuia bidhaa bandia kuingia ndani ya nchi, tukapitisha hiyo na TBS ikapitisha. Lakini jambo la ajabu toka mwaka 2012 bidhaa bandia zimezagaa katika Tanzania, TBS, FCC na FDA wapo. Sasa namna gani bidhaa zinazagaa? TBS aidha hawafanyi kazi yao vizuri kwa sababu kwanza kuna tatizo, tatizo lililopo ni kwamba TBS wanazuia sub-standard lakini hawana uwezo wa kuzuia fake kwa sababu substandard na fake ni vitu tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikiwa chini ya kiwango na kitu fake vinatofautiana kabisa, kwamba ikiwa chini ya kiwango maana yake ni kwamba kile kitu sio halisia lakini halisia, unaweza kitu original kimetengenezwa na Kampuni ya Sony akakitengeneza mtu katika eneo vile vile kuliko kile lakini hicho kikawa ni fake na si sub-standard.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bidhaa bandia Mheshimiwa Mwijage kila kona ya Tanzania inatusumbua. Mkiulizwa kila siku mnasema mnawafanyakazi kidogo na kuna vituo vingi, maana kuna vituo 38 au 48 lakini mnadhibiti vipi bidhaa fake? Hiyo ndio issue yetu tunataka. TBS wamekwenda mbali Tanzania mpaka tunaingiza mafuta machafu, TBS wanakwenda kukagua wanaruhusu mafuta machafu yanaingia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi leo nilikuwa na hayo lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mwijage… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ngwali.