Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, viongozi hawa wameutendea haki Mkoa wa Pwani. Kwa nyakati mbalimbali wamefika kutufanyia shughuli mbalimbali za uwekaji wa jiwe la msingi, ufunguzi na hata ukaguzi wa viwanda mbalimbali vinavyoendelea kujengwa katika Mkoa wetu wa Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoto ya Mheshimiwa Rais ambayo imeelezewa kinagaubaga kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwangu mimi naiona ina mwelekeo mzuri wa kutimia. Kwa nini nasema hivyo, ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri na ninampongeza sana kwa kazi nzuri kama nilivyotangulia kusema, katika ukurasa wa 16, tofauti na hotuba ya mwaka jana ameeleza kinagaubaga miradi ya viwanda tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa huo wa 16 mpaka 29 katika moja ya aya kwenye hotuba yake, ameeleza viwanda vikubwa 393 vyenye jumla ya mtaji wa dola za Kimarekani milioni 2000, kama shilingi trilioni 5,000 na ameeleza; ukisoma hotuba yake na ukisoma viambatanisho vyake, majedwali kuanzia 7(b), 7(c) na 7(d) utaona kabisa ni aina gani ya kiwanda, mwekezaji, ajira ngapi zitatekelezeka na ni investment ya kiasi gani. Kwa hiyo, mimi nadhani kwa maelezo yale inatosha kabisa kutoa dira kwamba sera hii ya uchumi wa viwanda inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, naomba nimpongeze Mkuu wetu wa Mkoa wa Pwani, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi kwa kuandaa mazingira wezeshi ya viwanda vyetu. Hapa naomba nisemee viwanda vya chuma vilivyopo Kibaha, cha Kilua, Kibaha Mjini na Mkuranga na ninaomba pia nijielekeze kwenye viwanda vya usindikaji matunda vilivyopo Mboga ambacho kinakaribia kukamilika, Bagamoyo pamoja na Mapinga.

Vilevile naomba nijielekeze, na nipongeze naweka kumbukumbu kwenye Hansard na mimi mwenyewe binafsi baadhi nilivitembelea, Kiwanda vya Vigae kilichopo Mkuranga ambacho ni kikubwa sana, kinatarajia kutoa ajira 4,500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ninaomba nijielekeze kwenye eneo letu la viwanda la TAMCO na nimeona nia ya Serikali ni njema, na ukiangalia hata bajeti ya maendeleo ya Wizara hii imeongezeka. Mwaka wa jana tulilalamika hapa zilitengwa shilingi bilioni 40, lakini Serikali imeonesha dhamira, imetenga shilingi bilioni 82, ni zaidi ya mara mbili ya pesa ambazo imetengwa mwaka wa jana. Ndani ya pesa hizi zimetengwa kwa ajili ya eneo la viwanda la TAMCO, Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, eneo lile kama ambavyo limeelezwa na Kamati yenyewe, kama ambavyo Serikali imeeleza namna gani eneo lilivyopangwa, upembuzi yakinifu umekamilika, ramani yake imekamilika, tunatarajia viwanda vya nguo, kuunganisha magari, dawa za binadamu pamoja na viwanda vya aina mbalimbali. Pia ninaiona dhamira ya Serikali, hasa kwa kutumia mifuko ya hifadhi ya jamii kujenga viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulizoea mifuko hii kujenga nyumba mbalimbali ambazo tunaziona sasa hazina soko, lakini dhamira ya kutumia mifuko hii, tumeona ni namna gani mifuko hii inavyoshirikiana ikajenga kiwanda kikubwa cha sukari Mkulazi, naunga mkono. Vile vile tumeona namna gani mifuko hii inayoshirikiana na MSD, TIRDO, Tanzania Investment Bank kujenga viwanda vinavyotumia mazao ya pamba. Kwa hiyo, unaiona dhamira ya Serikali kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba niulize; Wilaya yetu ya Rufiji ina maeneo ambayo tuliyatenga kupitia RUBADA na kuna maeneo yalikuwa yanatolewa na tulikuwa tunatarajia kujenga viwanda vya sukari, Mheshimiwa Waziri sijaona mahali popote alipotaja juu ya ujenzi wa viwanda hivi katika Wilaya yetu ya Rufiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, pia Wilaya ya Kisarawe tulipima eneo (Kisarawe Industrial Park), lipo tayari na tulijitahidi kama Halmashauri na Serikali Wilayani mpaka miundombinu, lakini pia sijaona litajwe popote. Lile eneo lipo sehemu nzuri, limepitiwa na reli ya kati, limepitiwa na reli ya TAZARA, lipo karibu na viwanja vya ndege Dar es Salaam na pia lipo karibu na bandari. Kwa hiyo, unaona mkoa wetu umekaa kama mkoa wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali, mwekezaji yeyote atahitaji athibitishiwe usalama wake, lakini pia anahitaji vivutio mbalimbali. Nina imani baada ya mkutano wa Mheshimiwa Rais na Baraza la Biashara pamoja na sekta binafsi, nina imani majadiliano yatakayoendelea ndani ya Bunge hasa itakapofika wakati wa Finance Bill, vikwazo mbalimbali vya kisheria, vya kodi na vya vivutio nadhani vitapatiwa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeeleza kwenye mchango wangu kwamba wawekezaji wetu hasa wa Mkoa wa Pwani wanahitaji ulinzi wa mali zao. Naiomba Serikali, pamoja na jitihada mbalimbali zinazoendelea, lakini kuimarisha ulinzi wa maeneo yetu. Naamini wawekezaji pamoja na nia waliyoonesha, lakini kwa matukio yanayoendelea pamoja na kazi nzuri ya Serikali, yanaweza kabisa kufifisha jitihada hizo za uwekezaji katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote haya yanakwenda sambamba na namwomba Mheshimiwa Waziri, kama ambavyo ameonesha kushirikiana na Waziri wa Wizara ya Maji, basi Wizara ya Kilimo na Mifugo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Sheria na Katiba, Wizara ya Miundombinu na Wizara nyingine za kimkakati zijitahidi kufanya kazi kwa pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ili kuonesha yale mambo yanayotegemeana na viwanda ili yaweze kufanyika kama inavyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani sisi kama Wabunge, binafsi mimi ninayetokea Mkoa wa Pwani, naamini wajibu wangu ni kuhamasisha wananchi wa maeneo haya kutumia fursa ya viwanda vizuri. Viwanda vyetu vitahitaji rasilimali, niwaombe vijana, wanawake na wananchi wa Pwani kutumia fursa ya viwanda vizuri. Tulime kilimo ambacho kitaleta tija, tujitoe kufanya kazi katika hivyo viwanda ili ajira inavyosemekana, nimepiga mahesabu, ajira katika viwanda vyote vinavyotarajiwa Mkoa wa Pwani ni kama 10,000 zile za moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo ajira chache. Fursa hii isije ikaonekana kwamba viwanda vinajengwa lakini ajira nyingi zinakwenda nje; sitarajii kwamba iwe za Pwani tu peke yake, lakini wote ni Watanzania, tuzitumie fursa hizo lakini wenyewe pia wa Mkoa wa Pwani tuzitumie fursa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimalizie kwa kuomba Wizara ya Viwanda na Biashara ulipaji wa fidia. Mheshimiwa Mbunge wa Bagamoyo amezungumza leo na hili jambo kwa kweli katika maeneo yale; na maeneo haya ya kimkakati kwa uwekezaji yanasaidia mno, ni maeneo maalum. Tulitembelea eneo maalum la Benjamin Mkapa (Special Economic Zone), tumeona viwanda vya nguo vilivyo pale, tumeona ubora wa bidhaa wanazozitengeneza, tumeona namna gani hata viwanda vile vilivyopo pale Benjamin Mkapa (Special Economic Zone) havijaweza kukidhi soko. Zaidi ya asilimia 30 bado halijakidhi soko la nje. Kwa hiyo, nina imani Serikali ikilipa fidia katika maeneo yote yaliyotengwa nchi nzima na kwa wakati na wawekezaji wakapatikana, uwezo wa kuzalisha bidhaa na kuzisafirisha nje ya nchi upo na masoko yapo.

Mheshimiwa naibu Spika, nimalizie kwa kuunga mkono hoja. Nashukuru sana kwa kazi nzuri inayoendelea kufanywa na naendelea kuamini Sera ya Viwanda, Uchumi wa Viwanda itawezekana. Naendelea kuamini changamoto zilizopo zinaweza zikatatuliwa mezani; na naendelea kuamini Mheshimiwa Rais ana nia njema na ipo siku tutashuhudia mapinduzi makubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.