Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu kabisa katika ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kama Waheshimiwa Wabunge wengine, ambavyo wamempongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo kwa kweli inaonesha matumaini ya hili suala tunalolizungumza juu ya Serikali ya viwanda inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ya kipekee kwa kutambua umuhimu wa kuwa na viwanda ambavyo ndiyo unaweza kuwa msingi wa wakulima wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ufahamu huu tulionao wote, lakini pamoja na hii ambayo ndiyo kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais kwa sasa, bado tunayo kila sababu ya kuhakikisha vyuo vyetu vya VETA na mitaala tuliyonayo inatambua umuhimu wa Serikali hii au Taifa hili kuwa na viwanda ili viweze kuchukua sehemu kubwa sana ya vijana kama ajira lakini ya uzalishaji mali na mazao ambayo yatakuwa yanatumika zaidi kwa wananchi hawa wanyonge lakini na kuuza nje ya nchi kama ambavyo tunatarajia kupata kipato kikubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua, nami leo nitajikita sana kwenye viwanda ambavyo, pamoja na utaratibu huu tunaoufikiria sasa wa kuwa na viwanda vipya au ujenzi wa viwanda vipya katika maeneo mbalimbali ya nchi hii lakini nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba tunayo kila sababu viwanda hivi tunavyovijenga kwa sasa ni lazima tuwe na kipaumbele na viwanda tunavyovihitaji kwa ajili ya maslahi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu muda wa miaka mitano ni mchache sana; tukisema miaka hii mitano tunaondoka na viwanda 100, 200, 3,000 au mia ngapi, bado tutakuwa tunajidanganya, tutakuwa na ma-carpenter wengi, hatutakuwa na SIDO nyingi halafu tunahisi tuna viwanda vikubwa ambavyo vinaweza vikasaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona mfano; tunapozungumzia uhaba wa sukari nchi hii, tunazungumzia moja kwa moja uzalishaji hafifu wa viwanda vyetu tulivyonavyo hapa nchini. Pamoja na uhafifu huo, tunayo mifano; Kenya, Uganda na nchi nyingine zinazotuzunguka, nataka tufikirie kuwa na viwanda vyenye vipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uchache huu, leo Mheshimiwa Waziri anaweza akajinadi na ana kila sababu ya kujisifu; hata bei ya sukari tunayolalamika sisi iko chini, huwezi kulinganisha na nchi za majirani zetu kama Uganda na Kenya. Sasa maana yangu ni nini? Unapokuwa na viwanda vya sukari vyenye kuweza kuzalisha zaidi, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo tulikuwa tunazungumza naye pale, wamekamata sukari ya Kilombero inaingizwa Kenya kule kwa magendo; na sababu ni moja tu; inawezekana uhaba huu tulionao bado sukari yetu inavushwa nje. Sasa maana yangu ni nini? Nataka tuwe na viwanda vyenye vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukiwa na viwanda yenye vipaumbele kwa miaka hii mitano, tutajikuta tunafanya kitu ambacho kitakuwa kinaonekana kwa Watanzania kuliko kubaki na historia ya ujenzi wa viwanda lukuki ambavyo havina vipaumbele kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine; nimesema mbali ya kuwa na viwanda vya kipaumbele, lazima sasa tuangalie, tunapiga hatua 100 mbele kufikiria viwanda vipya, tuna mawazo gani juu ya viwanda tulivyokuwanavyo toka zamani na leo tulivibinafsisha na haviwezi kufanya kazi yake sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mwanza tunavyo viwanda vya Tanneries, tunacho kiwanda cha MWATEX lakini tunavyo Viwanda vya Samaki. Kiwanda cha MWATEX ambacho toka mwaka 1995 kilibinafsishwa, wafanyakazi zaidi ya 1,720 ambao waliachishwa kazi na mpaka leo hawajalipwa, lakini kiwanda kile pamoja na mambo yake mengi, hivi tunavyozungumza, uwezo wa kiwanda hiki kuzalisha hata asilimia 30 ya yale yaliyokuwa yanazalishwa miaka karibia 12 iliyopita, hakijafikia malengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha MWATEX kila mmoja anafahamu, kila mmoja anajua umuhimu wa viwanda hivi; ni wakati gani tuko tayari kurudi kwenye viwanda hivi na tushughulike navyo viweze kuzalisha kama zamani? Mbali ya ajira kubwa ya zaidi ya watu 2,000, lakini vilikuwa na uwezo wa kuzalisha na tutasafirisha nje kwenye nchi za majirani na kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeongelea Kiwanda cha Tanneries. Kiwanda cha Tanneries kimebinafsishwa. Kiwanda hiki sasa Mheshimiwa Jenista pamoja na Wizara yake wameanzisha mafunzo muhimu kutoka nchi nzima vijana wanapelekwa pale zaidi ya 1,000. Hawa vijana wakimaliza kujifunza pale wanakwenda kufanya kazi wapi? Kiwanda hiki tangu kibinafsishwe hakijawahi kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba na hiki na chenyewe tukiangalie. Hawa vijana wanaotoka DIT kwenye mafunzo ya utengenezaji wa mikanda, viatu na mikoba, kiwanda hiki ikiwezekana kama siyo kurudishwa; na Mheshimiwa Rais aliahidi, tuangalie uwezekano wa kurudisha kiwanda hiki kije; vijana wanaotoka kujifunza hawa badala ya kwenda mtaani, watakuwa wanazalisha mali zilizokuwa na ubora. Wafanye kazi kwenye kiwanda hiki, wazalishe mali zenye ubora, tuuze ndani na nje ya nchi kwenye majeshi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni viwanda vya samaki. Tuna viwanda saba vya samaki. Hii ni lazima Mheshimiwa Waziri akubali kuungana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili waweze kuona. Miaka minne iliyopita kiwanda kimoja peke yake kilikuwa kinakata shift nne, watumishi zaidi ya 1,400, kikiwa kinakata tani 280 za samaki kwa siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kiwanda kimoja kinaitwa Vicfish kimeshafungwa; na hivi vilivyopo kimoja kina uwezo wa kuzalisha tani sita mpaka 12 kwa siku, kimepunguza wafanyakazi kutoka 1,400 mpaka 300 mpaka
150. Tafsiri yake ni nini? Tunaongeza Machinga, tunaongeza wafanyabiashara ndogondogo, ajira hakuna na kumbe tunaweza kushirikiana tukatengeneza ajira nyingi zaidi kama viwanda hivi vinaweza vikaboreshwa upya. Kazi inayofanyika ni nzuri, lakini lazima tunapokwenda mbele tukumbuke na tulikotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mpango wa sasa, viwanda tutakavyovijenga Mwanza, vinategemea kuzalisha ajira 1,004. Hawa tunaozungumza viwanda vilivyokufa, zaidi ya ajira 2,900 zimepotea. Tafsiri yake, tunahitaji viwanda hivi viangaliwe upya na ushirikiano kati ya Wizara mbili au tatu ni lazima uwe wa karibu ili kujenga msingi wa viwanda tunavyozungumza viweze kufikia malengo yake tunayoyatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda lazima akubali kushirikiana. Watumishi hawa ambao miaka 12 hawapo, leo wapo mtaani, wengine wameshakuwa wazee, tunahitaji kujua ni lini watalipwa mafao yao ambayo hawajawahi kuyapata miaka 12? Tukifanya hivyo itatusaidia, tutakwenda mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. Mungu akubariki sana.