Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mgeni Jadi Kadika

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MGENI JADI KADIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuweza kusimama na kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano, imejipanga katika uchumi wa viwanda; na ina nia nzuri tu ya kutoa ajira kwa Watanzania. Nchi yetu kama mtajenga viwanda vingi kama utitiri, lakini ikiwa havina usimamizi na wataalam waliobobea kiuweledi mkubwa, basi viwanda hivi vitakufa kama vilivyokufa vilivyokuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nichangie ujenzi wa Viwanda vya Minofu ya Samaki katika Ukanda wa Pwani. Nchi yetu inayo maeneo makubwa ya bahari, lakini hakuna kiwanda hata kimoja. Viwanda vyote vinaelekezwa kwenye Ukanda wa Ziwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali ijenge viwanda kwenye eneo la bahari kama vile Dar es Salaam, Tanga, Lindi, Mtwara, Pemba na Unguja. Ujenzi huu utatoa ajira na utainua maisha ya wavuvi na kupunguza umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakuja kwenye Viwanda vya Mabati. Viwanda hivi vinazalisha mabati chini ya kiwango katika baadhi ya viwanda, yakiwemo mabati ambayo yanaingia kutu haraka, mabati mengine yanachakaa haraka na pia yanavuja siku za mvua. Pia bei ya mabati hayo iko juu, kulingana na bei ya saruji ambayo kwa sasa imeshuka. Kwa hiyo, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia ubora wa viwango vya mabati na pamoja na kudhibiti bei? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bidhaa feki zimezungumzwa na wenzangu wengi hapa, lakini nami nataka nizungumzie kuhusu bidhaa feki. Kuna bidhaa feki nyingi zinazoingizwa katika nchi yetu. Maziwa ya watoto yana madhara makubwa juu ya kutumia maziwa haya. Nyaya za umeme zinaunguza majumba yetu, zinapelekea maafa. Matairi kupasuka kwa muda mfupi tu na kusababisha ajali nyingi barabarani. Vipodozi vinaharibu ngozi za akinamama na wengi wanapata kansa. Je, Serikali inatuambiaje kuhusu suala hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli wanawake wengi tuko ambao huwa tunatumia vipodozi na tunaharibika ngozi na wengi wanapata kansa, wengine wanakufa, uzuri wao umepotea. Kwa hiyo, hili suala linatakiwa lishughulikiwe kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nazungumzia kuhusu viwanda. Vimo viwanda vingi tu, SIDO, lakini hata vikiwekwa viwanda vikubwa kwa kuwaboreshea wakulima mazao yao, itakuwa ni bora zaidi. Nashauri kila kiwanda kiwekwe kila mkoa ili wazalishaji waweze kutumia viwanda hivi kwa kuyaokoa mazao yao; kama vile mananasi,maembe, machungwa, mazao kama nyanya na mazao mengine mengi tu yanaharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naona muda wangu umekwisha, naunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani.