Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Tunduma
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kuwasilisha hotuba nzuri ambayo imetoa ushauri wa kutosha na tumemshauri sana Mheshimiwa Mwijage kwamba ajitahidi sana kutumia hotuba hii ili aweze kutekeleza malengo ya Serikali ya Viwanda katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho nataka kukizungumza hapa, kwanza nianze kabisa na mazingira mabaya kabisa ambayo yako katika nchi yetu kwa ajili ya kuendeleza biashara katika nchi hii. Wote tunafahamu na wote tunajua kwamba katika nchi yetu kumetokea na wimbi kubwa sana la wafanyabiashara kufunga biashara zao yakiwemo maduka, mahoteli, lakini pia na wanaoendelea kuuza biashara zao hizo, wanafunga na hawafanyi tena biashara kutokana na mazingira magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tunauliza sana ndani ya Bunge kwamba Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inanusuru tatizo hili ambalo linajitokeza la wafanyabiashara kufunga biashara zao? Sababu kubwa ni nini? Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanalalamika kwamba mazingira ni mabaya, Serikali inawabana tofauti na jinsi inavyotakiwa. Wajibu wa Serikali siku zote ni kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingira mazuri ya wafanyabiashara kuendelea kufanya biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa inatoa majibu ndani ya Bunge inasema kwamba kuna watu wanafunga, lakini kuna watu wengine wanafungua. Hayo majibu hayawaridhishi kabisa Watanzania. Hivi ni kweli Serikali inataka kwenda kwenye Serikali ya Viwanda, inaona biashara zinafungwa na inasema kwamba wacha zifungwe, nyingine zitafunguliwa. Kwa hiyo, tafsiri ni kwamba biashara nyingine zifungwe na nyingine zifunguliwe! Naona tunafanya biashara ya sifuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sana Serikali hii ikagundua na ikashughulikia matatizo ya wafanyabishara. Lazima tuzungumze hapa ndani ya Bunge hili, kwamba mazingira ya kuanzisha viwanda katika nchi hii, kama wafanyabiashara wa ndani wanashindwa kufanya biashara na biashara zao zinafungwa, ni mwendawazimu gani mfanyabishara kutoka nje anaweza kuja kuwekeza na kufanya biashara katika nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima kwanza tuangalie mazingira mazuri ya kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu ndani ya nchi hii wanafanya biashara vizuri na biashara zao zinaendelea, ndipo watu kutoka nje watakuja kufanya biashara ndani ya nchi hii. Kama hatuwezi kuangalia matatizo ya wafanyabiashara wetu ndani ya nchi, halafu tukafikiria kwamba kuna wawekezaji watatoka nje waje kuweka biashara zao hapa, hili jambo tulisahau, halitaweza kutekelezeka hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliane kabisa kwamba nchi hii kumekuwa na matamko mengi sana ya vitisho. Juzi nilikuwa nasikiliza Taarifa ya Habari, wanasema kwamba hata wakulima sasa hivi wanaopata mazao mengi ni lazima waanze kulipa kodi. Nashangaa sana, yaani wanataka kutuambia kwamba wakulima hawa hawalipi kodi. Hakuna Mtanzania yeyote katika nchi hii ambaye halipi kodi. Tunalipa kodi katika njia tofauti tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima hawa wanalima mazao haya kwa kutumia fedha zao na Serikali haiwasaidii hata kidogo. Tumeendelea kuzungumza kuhusiana na pembejeo za kilimo hapa, zinafika kidogo; lakini leo Serikali inafikiria kwamba ni lazima iwakamue wakulima hawa, eti hawalipi kodi. Hilo siyo jambo la kawaida. Ni kwamba kodi zinakusanywa katika maeneo mbalimbali, siyo lazima ukachukue kodi kwenye yale mazao, lakini kodi zinakusanywa. Yule mkulima akishalima anakwenda kuuza, analipa kodi. Bado pia yule mkulima anakwenda mbele zaidi, anakwenda kununua mizigo ambayo tayari imeshalipiwa kodi, anakuwa ameshachangia Taifa lake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba sana, ni lazima Serikali iwe inafika mahali, inapotaka kuanzisha jambo fulani lazima ifikirie. Tunajiuliza sana kwamba mahusiano kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Fedha, kuna mahusiano gani hapa? Maana tunaona sana kwamba Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na watendaji wake wa Serikali wamejipanga sana kuhakikisha kwamba nchi inakuwa ya viwanda; lakini Wizara ya Fedha inakwamisha kutokana na sera na mipango mbalimbali ambayo inafika mahali inakuwa inapingana na dhana nzima ya kuanzisha viwanda katika nchi hii. (Makofi)
Kwa hiyo, ni lazima Wizara ya Viwanda na Wizara nyingine zinazofuatia na Wizara ya Fedha lazima wakae pamoja kupanga na kukaa, kuangalia ni namna gani wanaweza wakapunguza kero ambazo zinasababisha viwanda visianzishwe katika nchi hii.