Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Nami nichukue fursa hii, kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tupo katika enzi ya viwanda na uchumi wa kati, lakini kiukweli kabisa ni kwamba yanahitajika maandalizi thabiti. Sasa ni maeneo mengi ambayo tumekusudia kuyafanyia kazi. Jambo la kwanza kabisa ili tuwe na viwanda vya uhakika, ni lazima vilevile pia tuwe na umeme wa uhakika. Sasa ni mara nyingi tumekuwa na tatizo la umeme. Mheshimiwa Waziri atakapokuja naomba atuthibitishie, ni kweli tutakuwa na umeme wa uhakika? Kwa sababu viwanda bila umeme inakuwa ni kama kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Tanzania sisi ni wa tatu wa idadi kubwa ya mifugo; kama sikosei, baada ya Ethiopia na Botswana ni sisi tunaofuatia Tanzania. Ukiangalia wenzetu wa Botswana, ng’ombe anapoingia katika kiwanda cha kuchakata nyama, hakuna kinachotoka. Ngozi ina shughuli yake, nyama ina shughuli yake, pembe ina shughuli yake na kwato zina shughuli yake. Sisi Watanzania pamoja na mifugo tuliyokuwa nayo, bado hatujaweza kuitumia mifugo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, tutafute wawekezaji wenye uwezo wa kujenga viwanda vya kusindika nyama. Vilevile pia wenzetu wa Ethiopia, kwa mwaka 2016, wamepata takriban Dola 186,000 kutokana na ngozi peke yake. Wanatarajia mwaka 2017 kupata vilevile Dola za Kimarekani kuongeza idadi ya Dola 90,000,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, mpaka 2017 ikimalizika watapata zaidi ya Dola 276,000,000. Sisi Watanzania badala ya kuitumia mifugo vizuri, imekuwa tunazalisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine iliwahi kutokea hapa kwamba Maafisa wa Wanyamapori, wakagombana na wafugaji, ng’ombe wakapigwa risasi, wafugaji wale wakadhalilishwa, hadi kupelekea baadhi ya Mawaziri kujiuzulu katika Serikali ya awamu iliyopita. Kwa hiyo, naishauri Serikali tutumie mifugo vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Watanzania tumekuwa tunashindwa na baadhi ya nchi ambazo zimekuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe. Tukumbuke Ethiopia waliwahi kuwa na vita na Djibout, lakini baada ya kumaliza vita, wamekaa wamepanga mambo mazuri namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, ng’ombe pia wanazalisha maziwa, lakini Watanzania tumeshindwa kuyasindika. Matokeo yake tunaagiza maziwa ya kopo kutoka nje. Tunaagiza Nido, Lactogen, Nan; hali ya kuwa maziwa ya ng’ombe yangepakiwa vizuri, yangeweza kuwasaidia wananchi wetu. Kwa hiyo, naishauri Serikali itafute wawekezaji wa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye suala zima la viwanda; tuna matunda. Kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Tanga, Lushoto ni wazalishaji wa matunda na mboga mboga za aina nyingi. Muheza kuna kilimo kikubwa cha machungwa, lakini pia unakuta tunaagiza juice za Ceries kutoka South Africa na Saud Arabia ambayo ni nchi iko jangwani. Inakuwaje sisi ambao tunazalisha machungwa by nature lakini tunashindwa kuyachakata tunaagiza juice kutoka nje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali tutafute wawekezaji wa uhakika. Tusizungumze suala la viwanda kisiasa; tuwe na dhamira ya dhati na ya kweli. Viwanda hivyo vitakapojengwa wananchi wetu watapata ajira lakini vilevile Serikali pia itapata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nililotaka kuzungumza, moja ya matatizo yanayofanya wawekezaji wasije Tanzania, ni mifumo mibovu ya kodi, umeme usiokuwa wa uhakika, lakini vilevile pia kuna kitu kinaitwa urasimu. Mtu akitaka kuwekeza kiwanda Tanzania, atahangaishwa, itafika miaka miwili. Wenzetu Uganda ndani ya masaa 48 ukitaka kuwekeza unapata kila aina ya msaada unaotaka na Serikali inakwambia, kama unataka kuongezewa mtaji pia iko tayari, lakini Tanzania hilo hatulifanyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwanza inaweka miundombinu rafiki, mifumo mizuri ya kodi, lakini tuondoe urasimu. Vilevile pia nataka kuiambia Serikali…

(Hapa kengelee ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)