Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tumbatu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa shukurani zangu kwako kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia katika hotuba ya Wizara hii ambayo ni miongoni mwa Wizara muhimu katika Taifa letu.
Pili, natoa pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Waziri, pamoja na watendaji wake wote kwa matayarisho ya kitaalam ya hotuba ya Wizara hii. Nawaomba wazidi kushirikiana ili kufanikisha malengo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba hii, napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta binafsi ni sekta muhimu katika nchi yetu. Sekta hii inawagusa wananchi wa kipato tofauti wenye azma ya kujiendeleza kiuchumi. Sekta hii inakabiliwa na matatizo kadhaa, kama vile upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji ambayo huwa yanawakatisha tamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iwaondolee urasimu huu ili kuwawekea mazingira rafiki ili iwe kama ni vivutio kwa sekta hii. Aidha, Serikali iwapunguzie tozo ambazo hazina ulazima. Tozo nyingi huwa zinaidaiwa kwa sekta binafsi mapema kabla ya mwekezaji binafsi hajaanza kazi. Ni vyema tozo (tax) zidaiwe baada ya uwekezaji kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa viwanda nchini; naipongeza Serikali yetu kwa azma nzuri ya kujenga viwanda, ujenzi wa viwanda utaongeza tija katika nchi na kuongeza nafasi za uajiri. Ujenzi wa viwanda unahitaji matayarisho mengi kabla ya kuanza. Kwa mfano, huwezi kujenga kiwanda mahali ambapo hakuna umeme, maji na miundombinu ya barabara. Naiomba Serikali kuchukua juhudi za makusudi kuimarisha miundombinu hii ambayo itawashawishi wawekezaji wa nje na ndani kuwekeza katika Sekta ya Viwanda. Aidha, naomba Serikali ipunguze baadhi ya kodi kwa wawekezaji wakubwa wa nje na ndani ili pia iwe ni kivutio kwa wawekezaji wa aina hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu matayarisho ya rasilimali watu; Serikali ina azma nzuri ya kufikia na kukuza uchumi kwa kupitia Sekta ya Viwanda. Sekta ya Viwanda ni ya kitaalam ambayo inahitaji weledi wa kupanga na kuendesha sekta hii. Naishauri Serikali kuchukua juhudi za makusudi kuanza kuwatayarisha Watanzania kwa kuwapatia mafunzo ya kila ngazi ili kujiweka tayari kuendesha sekta hii. Aidha, ni vyema kuwafundisha na kuwapa kipaumbele wazawa na kuepuka kabisa kutumia wataalam kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.