Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada zake za vitendo kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya viwanda. Napongeza kazi nzuri inayofanywa na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ya kufufua na kujenga viwanda, huku akihamasisha wawekezaji kuingia nchini na kufanyika kwa biashara ya kiushindani kwa maendeleo ya wananchi wetu. Natoa pongezi za dhati kwa Wizara hii kwa jinsi wanavyojitoa kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni wakulima bora na wazalishaji kwa ziada kubwa na kuchangia chakula kwa Taifa letu. Mkoa wa Rukwa tuna viwanda vidogo vinavyoendeshwa na sekta binafsi na tangu 2015 hadi sasa tuna viwanda 137 vyenye ajira ya 411 (mpya).

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamekuwa wanapata mfumuko wa bei ya unga pamoja na kuwa na mahindi ya kutosha. Hivi sasa bei ya unga Mkoa wa Rukwa sokoni kilo moja ni Sh.1500, kilo tano ni Sh.8,000/= na kilo 25 ni Sh.37,000/=. Naomba Serikali kuwawekea mazingira bora hawa wenye viwanda hivi vidogo kuzalisha kwa wingi na kupelekea kuteremsha bei ya unga. Pia mahindi yaliyomo ndani ya maghala ya Taifa ya miaka iliyopita yatolewe na kuuziwa wenye viwanda vya unga (sembe) kuliko kuharibika. Tunaomba wawekezaji waelekezwe Rukwa tupate ajira kwa vijana wetu na kuteremsha mfumuko wa bei ndani ya soko kwa maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu wengi wanakimbilia kufanya biashara mbalimbali ila hawana uelewa wa uendelevu wa biashara zao. Tatizo ni upungufu wa rasilimali watu katika maeneo yetu, Maafisa Biashara kuwa wahusika na leseni za biashara badala ya kuwainua wafanyabiashara kuwa na biashara zenye tija. Naomba Serikali kutoa ajira kwani tunao vijana waliohitimu kwenye vyuo vyetu vya CBE ili tupate wataalam wa kukidhi mahitaji, tupate wafanyabiashara watakaoendana na ushindani wa kiulimwengu na wa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri kwamba kwa kuwa tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, ni vema maeneo kama Rukwa tuhakikishe tunawaimarishia Chuo cha VETA na kuboresha Kituo cha SIDO.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Waziri wa Viwanda kutuangalia sisi wa mikoa ya pembezoni kwa bidhaa kadhaa kuwa na bei za juu mfano sukari kilo moja ni Sh.2,200/=, sementi mfuko ni Sh.14,000/=. Kutokana na maeneo ya ujenzi wa viwanda yapo, tunaomba kuelekezewa wawekezaji wa kujenga viwanda hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.