Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuunga hoja mkono. Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi ambapo kama zitatumiwa vizuri katika viwanda vyetu zitaleta manufaa makubwa sana katika Tanzania yetu. Hata hivyo, changamoto kubwa inayovikabili viwanda nchini ni ukosefu wa mitaji, teknolojia, umeme, malighafi zisizokuwa za uhakika pamoja na ukosefu wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto niliozitaja hapo juu bado hakuna vivutio vizuri kwa wawekezaji kutoka nchi za nje na mlolongo wa kodi nyingi ambazo zinawavunja moyo wawekezaji wa ndani na nje. Ningeshauri Serikali kwa changamoto ambazo nimezitaja hapo hasa za ukosefu wa umeme, teknolojia na maji ni vema sasa Wizara ya Viwanda ikakaa pamoja na kuwa na mikakati ya pamoja na Wizara ya Nishati, Kilimo na Maji ili kuunganisha nguvu kwa pamoja na kuwa na mkakati mmoja kwa kuwa Wizara nilizozitaja hapo juu zina mahusiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mlolongo wa kodi ni vema sasa Serikali ikawa na chombo kimoja ambacho kitakuwa na mamlaka ya kutoza kodi ambacho kitasimamia utozaji wa kodi zote kwa wawekezaji. Mkoa wa Singida ni mkoa unaosifika kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Mazao ya biashara ni alizeti, vitunguu, pamba, ufuta, karanga na choroko. Mazao ya chakula ni mahindi, mtama, viazi vitamu na uwele, lakini bado hakuna viwanda vya kutosha. Pia Singida ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo. Mazao yote niliyotaja hapo juu yangeweza kuwa malighafi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika viwanda mbalimbali ambavyo vingeanzishwa Mkoa wa Singida. Mkoa wa Singida ni maarufu kwa ukulima wa alizeti, alizeti inayozalishwa Singida ni maarufu Afrika Mashariki na Kati. Singida ina jumla ya viwanda 126 vya alizeti, kikubwa kimoja, vitatu vya kati na vidogo vidogo 122. Hivi vidogo vidogo vinategemea mitaji kutoka SIDO.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeishauri Serikali yangu kuona uwezekano wa kuwaongezea uwezo SIDO, ili waweze kuwakopesha viwanda vidogo vidogo mitaji ya kutosha. Kwa sasa SIDO inakopesha shilingi milioni sita. Iwapo itaongezewa uwezo angalu kuwakopesha wajasiriamali wa viwanda vidogo vodogo milioni ishirini itakuwa ni jambo jema sana. Kwani wajasiriamali wadogo wadogo hawana uwezo wa kwenda kukopa kwenye benki na taasisi mbalimbali za fedha kwa kuwa wanatoza riba kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningeomba Wizara hii kuuangalia Mkoa wa Singida kwa jicho la pekee kwa sababu kila Wilaya/Halmashauri tayari kuna maeneo kwa ajili ya kuanzisha viwanda, kinachokosekana ni mitaji, hivyo iwapo Serikali itapata mitaji itasaidia sana kuweka miundombinu ya viwanda kwa kuwa malighafi si za kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri wa Viwanda Mheshimiwa Mwaijage kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuleta mageuzi katika viwanda yeye pamoja na timu yake, nawatia moyo waendelee kukaza buti kazi ni nzuri na yenye tija.