Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, huwezi ukatenganisha viwanda na umeme. Umeme, tuna siku mbili; wiki ijayo, Alhamisi na Ijumaa, tunzeni maswali yenu yote, hebu leo tushughulikie viwanda tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje. Kama unalipenda Taifa lako, ni lazima utapiga marufuku makaa ya mawe na gypsum yaani jasi isitoke nje. Twende kwa takwimu; ni kwamba tulikuwa na mtaalam mmoja tu, bahati mbaya amefariki Dkt. Semkiwa, alifanya Ph.D yake University ya Colon Ujerumani, Profesa wake alikuwa wa kutoka Australia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa wakati huo miaka ya 1990 wamepiga mahesabu kwamba tuna mashapo deposit ya bilioni tano ya ‘B’, ya baba. Miaka mitatu nyuma alivyoendelea na utafiti akasema, tunaweza tukafika bilioni kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unayesema turuhusu makaa kutoka nje, nawe tupatie takwimu za kuonesha kwamba hatuna makaa ya kutosha, lakini bila takwimu, msimamo wa Serikali ni kwamba bado tutazuia makaa yasitoke nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi, Ngaka walikuwa wanayumbayumba, wanazalisha tani 80,000 kwa siku; Magamba wanazalisha tani 1,000 kwa siku; Kabulo ambayo ni ya STAMICO wameanza tarehe 30 mwezi wa Nne sasa hivi wana tani 500. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, kama kuna mtu ana kiwanda cha saruji anakudanganya kwamba makaa hayapo, mwambie aje Wizarani kwangu aende Ngaka, aende Magamba, aende Kabulo, makaa ya mawe tunayo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu wa Lindi na Mtwara wamelalamika kwamba hakuna viwanda huko. Sehemu pekee kwenye Taifa hili kwa miaka kumi au ishirini inayokuja ambayo itaendelea kwa kasi, nasi wote tutahamia huko, ni Lindi na Mtwara. Mikoa mingine itabaki ni Mikoa ya kizamani; ya pamba, korosho, na dhahabu, mikoa ya kizamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Lindi hakuna uwekezaji mkubwa ambao umeshafanyika wa kihistoria kama ambao utafanyika Lindi wa LNG; ni bilioni, bilioni, bilioni tena ya ‘B’; bilioni 30 ambayo ilikuwa inazidiwa na reli ya TAZAMA ikafuata bomba hili, inalofuata ni pale Likong’o Lindi. Utasemaje kwamba Lindi imesahaulika ina uwekezaji wa bilioni 30. Haiwezekani!

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua viwanda vikubwa vikubwa, hivyo vidogo namwachia Mheshimiwa Mwijage ndio anaviweza mwenyewe. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda cha Mbolea kitajengwa Lindi tena mmoja nadhani sikuwepo, alitoa kauli mpaka Balozi wa Ujerumani amenipigia simu jana anasikitika sana, sijui alipata wapi taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaeleze, tuna viwanda viwili vitajengwa; cha mbolea cha Kilwa kitajengwa na Kampuni ya Ferrostaal. Hizi ni kampuni za Kimataifa na kile cha Mtwara kitajengwa na kampuni ya Helium nayo ni ya Ujerumani. Hayo ni makampuni ya Kimataifa, eeh! Sikiliza sasa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba, hii ya Kilwa Ferrostaal Balozi huyu aliyemaliza muda wake kabla hajaondoka tunataka kwenda kuzindua groundbreaking ceremony. Siyo kuweka nini; ile tunaenda kabla ya tarehe 1 Julai, uwekezaji wake ni bilioni 1.92. Bilioni ‘B’! Utasemaje kwamba Lindi na Mtwara imesahaulika? Itazalisha mbolea Urea tani 2,200 kwa siku; Ammonium tani 3,850 kwa siku ya Urea. Utasemaje Mbeya wamesahaulika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu wa Mtwara, nitamwachia ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage aongee ya cement ya Dangote, lakini kuna kiwanda kingine cha mbolea cha Helium, haya ni makampuni makubwa! Nenda u-search u-google mwenyewe utayaona. Ni uwekezaji wa bilioni ya ‘B’ siyo milioni 1.26 na itazalisha tani 3,700 kwa siku. Utasemaje Lindi na Mtwara imesahaulika? Lindi na Mtwara ndiyo Mikoa mipya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme nimesema tuonane wiki ijayo. Nakuja suala la Liganga. Bado nina dakika tano! Niongeze speed eeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni wakati tunafanya utafiti, hatukujua namna ya kutenganisha iron, titanium na vanadium. Ph.D alifanya Profesa Mahinda, mimi nilikuwa bado mwanafunzi Dar es Salaam Chuo Kikuu, tulikuwa tunapigania chuma tu, lakini dunia sasa imebadilika, hii chuma haina thamani kubwa kuliko titanium na vanadium.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huyu mwekezaji kazi moja kubwa anayoifanya ni ya kutenganisha iron from titanium, from vanadium. Hiyo inataka muda, inataka vivutio; na hivi vivutio vinataka sheria zije humu zibadilishwe. Huwezi ukaweka vivutio kwa ajili ya Liganga na Mchuchuma peke yake, kwa hiyo, inamaanisha tupitie vivutio vyote; hata vivutio vilivyopo vya TIC uwekezaji wa umeme unahesabika sio strategic.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu tukubali kwamba hatujachelewa na hii itafanyiwa kazi. Kingine ambacho ni muhimu ilikuwa ni mchuchuma, yaani kwenye makaa ya mawe. Wenyewe wakati wanatengeneza mradi, tulikuwa na matatizo ya umeme wakataka wauze senti 13 kwa unit moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mahesabu yao yote ya kuchimba chuma na makaa kuzalisha umeme, yalijikita kwenye senti 13. Kwa kuwa tuna umeme mwingi, huo sasa hivi tunauita umeme wa bei mbaya. Kwa hiyo, inabidi waje kwenye model ya senti saba au nane kwa unit. Hiyo model nayo inataka muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msiseme kwamba vitu havifanyiki. Ameshafanya experiments kubwa sana za kujaribu kutenganisha iron, titanium, vanadium, lazima aje na model wa senti saba mpaka nane wa kuzalisha umeme wa Liganga. Kwa hiyo, Waheshimiwa ni kwamba kazi zinafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaoneshe, wenyewe tunataka kuzalisha tani milioni moja; vile vile tunabadilisha mawazo. Mawazo yalikuwa kuzalisha chuma kusafirisha nje ya nchi, lakini sisi ni kama wachezaji, ni kama tunachezea njugu. Wapo wasafirishaji wakubwa. Kwa hiyo, lazima tubadili concept hiyo. Kwa mfano, Australia mwaka 2016 chuma iliyozalishwa duniani, ilikuwa tani bilioni 3.4. Imewatosha?

Haya ahsante. Jamani hili la Liganga Mchuchuma, mwache, ni mambo ya kitaalam, linaenda vizuri. Ahsanteni. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Profesa Muhongo, ulikuwa unataja hapo hizo bilioni. Ni dola au ni hela za Kitanzania? Zote tu ulizotaja hayo mabilioni ni hela za Tanzania ama ni dola?

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawahi kuwaeleza, miradi yangu yote huku ni dola.