Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
WAZIRI WA VIWANDA BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia wote nguvu na afya njema ili kuweza kujadili hii bajeti yetu kwa siku mbili. Hii ndiyo bajeti inayobeba Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wenye dhima ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Nawashukuru sana Wabunge wote mlivyojadili bajeti hii, napenda niseme mmeitendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee namshukuru Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa; yeye na Kamati yake kwa jinsi walivyoichambua bajeti yangu na kwa jinsi walivyosimamia Wizara yangu, mpaka kutupelekea kuandika hii bajeti ambayo kila anayeisikia, anaomba nakala halisi pamoja na kwamba iko kwenye mtandao.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba nimshukuru kipekee Waziri kivuli wangu, Mheshimwa Antony Komu kwa hotuba yake ya kufikirisha ambayo inakufanya ufikirie miaka mingi mbele, uende maili nyingi. Waziri Kivuli nakushukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na ushauri mzuri, uliotolewa na Kamati na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, Wizara na taasisi zilizoko chini yake imepokea pongezi nyingi kwa kuweza kutekeleza masuala ambayo wananchi wamekuwa wakiyatarajia. Hakika pongezi hizo zinatupa hali ya moyo ya kujibidiisha zaidi katika kubuni, kupanga na kuboresha mbinu za utendaji ili Taifa na Watanzania kwa ujumla wanufaike zaidi na matunda ya fursa zilizomo. Nami nawaahidi kuwa tutaendelea kujibidiisha na wala hatutawaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Waliochangia kwa kuongea moja kwa moja ni Waheshimiwa Wabunge 44; waliochangia kwa njia ya maandishi ni Waheshimiwa Wabunge 48; waliochangia Wizara hii kwa kina katika bajeti za Mawaziri wenzangu waliotangulia ni Waheshimiwa Wabunge 10, ujumla wake watu 101 wameiunda upya Wizara yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijitahidi kujaribu kuweka sawa kwa mujibu baadhi ya hoja, lakini ni kweli wataalam wangu wote wako hapa, wamejiandaa watatengeneza majibu ya kina; na kama nilivyosema, mtazamo wetu katika kujenga uchumi wa viwanda mmeujenga upya. Kwa maneno rahisi, mmeuimarisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la kwanza, the misconception, what is not, mawasiliano ya kati na ndani ya Serikali siyo mazuri; the misconception, siyo kweli. Mawasiliano ndani ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ni mazuri. Sina muda wa kuzungumza zaidi, nitawapa vielelezo. Serikali hufanya kazi kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni Taarifa ya Wizara yangu ambayo nimemwandikia Waziri wa Fedha baada ya yeye kunitaka kwa maandishi kwamba ni vivutio gani unavitaka ili wawekezaji wako waweze kuwekeza unavyotaka, iko hapa. Akaenda zaidi, ni kodi gani ziongezwe au zishushwe ili mambo yaende vizuri? Ndiyo hayo! Kwa hiyo, mawasiliano ni mazuri na Serikali inafanya kwa makaratasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, watu wasipate wasiwasi kwamba nchi hii inaingia vitani, hapana! Tunafanya kazi vizuri na nakumbuka, bahati mbaya simu zangu nimezifungia, mawasiliano ya mwisho alinipigia akiwa Marekani kwamba hakikisha andiko hili linapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimempa maelekezo Katibu Mkuu wangu anayeshughulikia biashara na uwekezaji, anayeshiriki kwenye chombo cha Kitaifa kinachopitia bajeti kabla ya kwenda kwa Mheshimiwa Waziri kwamba yale niliyoyapendekeza mimi msiongeze wala kupunguza chochote. Kama mnakataa, andika mmekataa, kusudi siku ya siku waje waone tunavyoshirikiana. Serikali hii ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi, nimeelezea hivyo, lakini nitatoa mifano mingine zaidi. Tunawasiliana!
Waheshimiwa Wabunge, zimekuwepo hoja na mmesema ukweli kwamba kasi ya kujenga uchumi wa viwanda inakwenda taratibu. Napenda nikiri na nitambue mchango wenu, lakini nyie sio wa kwanza. Kuna wakati mimi na Mheshimiwa Waziri Mkuu tulikuwa hatuangaliani machoni; nikawauliza Wasaidizi wake, vipi? Wanasema, haoni viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mama Samia kuna wakati aliniiita nyumbani kwake, akasema Mwijage nataka viwanda vya madawa! Bahati nzuri Mheshimiwa Ummy amekwenda kutafuta viwanda hivyo, hayupo hapa. Tajiri huyo ndio alikuwa hataki kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitambue mchango wa Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Kijazi, nikamwambia mzee nifanyaje? Akasema kama hawakuelewi andika! Nikaandika kitabu hiki kinaitwa strategy for fast tracking in industrialization in Tanzania. Yote mliyoyasema yako humu. Wakakipeleka kwa tajiri. Tajiri namba moja; wewe unalinda duka tu, tajiri ni mmoja tu! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilijuaje kwamba Mheshimiwa Rais ameona kitabu hiki? Tulipowaita wawekezaji, Mheshimiwa Rais alitamka kwamba wakati wa kuwekeza ni sasa na atakayetaka vivutio, aje aniambie. Nikajua ugonjwa umepata dawa. Nimewasiliana, Serikali inawasiliana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo ni vielelezo viwili kwamba the Government is coordinated; na kitabu hiki siyo changu tena, kimeshapelekwa kwenye Kamati ya Wabunge wote na kinakwenda kwenye Baraza la Mawaziri. Kwa hiyo, Serikali inawasiliana. Naweza kutoa ushuhuda, Mheshimiwa Mpina alizungumza nini, tulibishana nini kuhusu hii; na vile vikwazo vyote na gear zote za kwenda kasi, zimezungumzwa humu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikiano wa Sekta Binafsi na Serikali. Viongozi wa Sekta Binafsi wako pale; Tanzania Private Sector Foundation, CEO wao Dkt. Simbeye yuko pale. Jana mliona uwanja wote ulijaa suti za bei mbaya! Hao ni wawekezaji hao! Walikuwepo hata wale akinamama wa VICOBA, wote ni wawekezaji. Tungekuwa na mahusiano mabaya wasingekuja. Kwa hiyo, mawasiliano yetu ni mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi huu tukiwa Bungeni, mimi na Mheshimiwa Mpango tuliitisha mkutano wa wawekezaji wote, mliona; uwanja wa ndege wa Dodoma ulionekana mdogo, ulijaa ndege! Wawekezaji wa Madini walikuwepo; wa umeme walikuwepo, tukakutana, tukajadiliana; na tukawekeana maazimio. Tumekubaliana kila miezi mitatu tuitishe mkutano mkubwa. Sekta Binafsi na Serikali tunafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ngazi ya Kitaifa, Baraza la Biashara la Taifa ambalo Mwenyekiti wake ni Mheshimiwa Rais, tumekutana juzi. Wale mnaotumia mitandao, ndiyo ile clip ya Millard Ayo inayozungumza, ikichukua yale maneno matatu aliyoyasema Mheshimiwa Rais, wakati wa kuwekeza ni sasa. Atakayekukwamisha njoo uniambie. Ukitaka vivutio, nitakupa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Mheshimiwa Rais anasema ukitaka vivutio nitakupa, wewe unaogopa nini kumfuata? Si anaonekana! Amekwambia ukitaka vivutio atakupa. Nenda kamwambie sasa akupe, si yupo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namba tatu ni viwanda vilivyobinafsishwa. Mheshimiwa Devotha, wewe bado ni rafiki yangu. Usidhani urafiki wangu ulikufa kwa sababu ulifanya hivyo, hapana, bado ni rafiki yangu. Tatizo la Morogoro halipo tena. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, mnitendee haki. Msome kitabu changu, kina majibu ya kila kitu. Moro Canvas karibu mambo yake yatakwisha. Kutoa kiwanda kwenye ownership moja kwenda ownership nyingine kuna mambo ya kimikataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikwambie nimetumia nguvu zangu zote na muda wangu wote, mimi nina maslahi. Nimekwambia Mheshimiwa Devotha urafiki wangu na wewe hautakufa. Nilikasirika kipindi, sasa hasira zimekwisha, eeh! Kuna wakati alibadilisha mwelekeo wetu na mimi nikakasirika, sasa nimetulia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, MOPROCO inaanza mwezi wa Sita. Matatizo ya MOPROCO yamekwisha na nimeshaeleza kwenye kitabu changu kwamba pamoja na ku-crush mbegu ita-crush hata mashudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, MOPROCO inaanza, haina tatizo na Moro Canvas inaanza. Hivi vingine viwanda vya Ceramic, siyo tatizo, tutavishughulikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye viwanda vilivyobinafsishwa, nimeandika kwenye mambo nitakayoyafanya kwamba mfumo wa sasa wa kushughulikia viwanda vilivyobinafsishwa utabadilishwa. Lazima tumhusishe Mkuu wa Mkoa, tuhusishe Wizara ya Kisekta, tumhusishe kikamilifu Attorney General na lazima tuihusishe Wizara yangu kama anavyosema bosi wangu wa zamani, jeshi la mtu mmoja. Kwa hiyo, viwanda vilivyobinafsishwa ndiyo hatma yake.
Mheshimiwa Japhary rafiki yangu, Mheshimiwa Rais amekuja juzi anasema viwanda vya Moshi vifanye kazi. Kama Mheshimiwa Rais anasema, mimi nitapingaje? Juzi mtu mmoja amenipigia simu, anataka Kiwanda cha Viberiti. Kwa nini Kiwanda cha Viberiti kilikufa? Mlikuwa mnaagiza viberiti kutoka Pakistan vya bei rahisi wakati vya hapa mnaviacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza Waziri wa Mambo ya Ndani, atanisaidia kuhakikisha smuggled items haziingii nchini. Mheshimiwa Mwigulu nami itabidi niende lindo. Ni hilo naweza kuwaeleza kwenye viwanda vilivyobinafsishwa. Azma ya Serikali ndiyo hiyo, tunaongeza nguvu, kazi ya Treasury Registrer, Wizara za Kisekta, twende pamoja. Mama, viwanda vya Korosho ni chapter inajisimamia yenyewe; tutazalisha na ile kitu ambayo ukiiona unasema astaghfiru Allah. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namba nne; mazingira ya kufanya biashara. Mazingira ya kufanya biashara naomba nilizungumze hili na Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, unajua mtu akitusikiliza, lakini hiki ni kikao cha wakubwa, ndiyo maana hata mitandao mingine hairuhusiwi kusikiliza. Kwa hiyo, wakubwa mnaponyukana huko chumbani, mnanyukana mtu wa nje asisikie.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu akitusikiliza atadhani Tanzania hapafai kuwekeza, hapana! Ni kwa sababu tunakopataka siyo hapa. Kwa hiyo, muumini mkubwa wa mazingira mazuri ya kuwekeza ni mimi namba moja. Nikipata muda nitawasimulia. Niliwahi kupoteza kazi yangu nzuri kwa sababu ya mazingira mabovu ya uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma report ya dunia ya mwaka 2017, wepesi wa kufanya shughuli, Tanzania tuna nafasi ya 132, tulipoanza tulikuwa 139 katika nchi 190. Mzazi yeyote akipeleka mwanaye shule, hawezi kufurahi kwamba mwanawe awe wa 132; lakini siyo sababu ya kupiga kelele au ya kulalamika kana kwamba kuna mtu kafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie sababu moja inayofanya Tanzania kuwa ni sehemu ambayo siyo nzuri ya kuwekeza. Wale wanaotupima, wanaangalia wepesi wa watu kulipa kodi na ule mfumo wa kodi. Sasa watu wengi wanaojadili wanaangalia upande ule unaolipisha kodi, wanaangalia madhaifu ya TRA, lakini hawaangalii wepesi wa mtu kulipa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi nyingine zilizoendelea ambazo ziko better ranked, namba moja, namba kumi, mtu anadai risiti, anasema lazima unipe risiti, unioneshe kodi. Hapa, unamwambia andika kwamba hii bidhaa ya shilingi milioni moja, niandikie laki moja halafu, basi, basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wepesi wa kulipa kodi ni kigezo. Kwa hiyo kama ningekuwa mhubiri kama ambavyo mdogo wangu Bashe anaamini ningewaambia tujitazame, tuwe wepesi wa kulipa kodi na tuwaambie wapiga kura na ndugu zetu tuwe walipa kodi wazuri kusudi wawekezaji waje. Mwekezaji makini hawezi kuwekeza katika nchi ambako mmoja analipa kodi, mwingine halipi kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, rafiki yangu pale Mnyampala anasema, mbona makampuni yamekufa? Mbona biashara inakufa? Mbona maduka yanafungwa? Inaitwa paradigm shift. Kama ulizoea kuleta bidhaa yako hulipi kodi, sasa utaratibu ni kulipa kodi, uta-collapse. Kama ulikuwa unalipa chumba Kariakoo kwa kodi ambayo ni kubwa kuliko London, haiwezekani chumba Kariakoo kikazidi London, huo unaitwa uchumi bandia. Sasa ni uchumi halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hao wataondoka. Sasa tutahesabu shilingi kwa ya pili, tutajenga uchumi imara na mfanyabiashara atakayelipa kodi ataweza kustawi. Huo ni upande wa pili wa sisi walipa kodi. Upande mwingine ambao walio wengi na mimi nikiwa Mbunge tunausemea ni upungufu wa TRA. Nawaahidi, mimi ni sehemu ya Serikali, tutaishughulikia. TRA ina upungufu, tutaiboresha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma taarifa ya Wizara yangu aliyosimamia Profesa Mkenda, wepesi wa kufanya shughuli Tanzania, walipotu-rank Wazungu na sisi tukaji-rank; unajua mtu akikwambia wewe ni handsome boy, kajiangalie kwenye kioo, kweli wewe ni handsome au anakudanganya? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wazungu walipotufanyia ranking, nasi tukajifanyia ranking wenyewe. Tukatengeneza zoezi la wepesi wa kufanya biashara. Katika kitabu hiki alichokiongoza Profesa Mkenda, kimehusisha Watendaji wa Wizara zote za Serikali, wote wamehusishwa. Kwa hiyo, NEMC kama anakosea, tunasema anakosea; TBS ana makosa, ana makosa; TFDA, ana makosa, ana makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu hiki shangazi, kodi 25 za Kagera zimeandikwa. Rafiki yangu Gimbi anasema umefanya nini nyumbani? Nimepigana kodi 25 zitoke, ngoja aje Tizeba kesho. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma kitabu hiki kinaeleza kwamba kila Waziri aliyepewa mamlaka, yale mambo ambayo kutokana na regulations anaweza kuyabadilisha, ayabadilishe. Ndivyo inavyosema. Kwa hiyo, kero zote tutaziondoa moja baada ya nyingine. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, nashukuru mmepaza sauti. Mlitupa jukwaa kama lilivyo, tumeshughulikia. Tuliyoyaona ndiyo hayo, fast tracking of industrialization lakini vikwazo viko hapa, tumemaliza. Kilichobaki ni utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya point tatu hizi katika 25 nitakazozisema, Waheshimiwa Wabunge kwa point tatu nawaomba mjiandae kwa heshima na taadhima na bashasha na nderemo kunipitishia Bajeti yangu niende kuitekeleza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Viwanda. Hapana, kwanza niwaeleze viwanda ni nini? Halafu nije niwaeleze Sera ya Viwanda. Mheshimiwa Nape na Waheshimiwa Wabunge wengine wametaka kujua tafsiri ya viwanda. Shughuli yoyote, viwanda vina tafsiri mbili; ile tafsiri inayohusisha mambo ya construction, uzalishaji wa gesi kwamba ni viwanda, mimi siitumiii. Naitumia ile ya manufacturing, ya kuongeza thamani ya kuchukua mawese yakatoa mafuta, mbegu za alizeti kutoa mafuta, cotton kutoa suti nzuri kama niliyovaa leo hii. Hivyo ndiyo viwanda unavyovihesabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ngoja niwaeleze, kiwanda kidogo sana ni kiwanda kinachoajiri mtu mmoja mpaka wanne; na kiwe na thamani isiyozidi shilingi milioni tano. Kiwanda kidogo sana! Watu wanakwenda zaidi, wanasema ukiwa na vyerehani vinne ni kiwanda kidogo. Najua kuna Mbunge mmoja hapa alianza na vyerehani vinne, leo ana vyerehani 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Katani, amekuwa mkweli. Amesimama akawaambia, Mwijage alinielekeza nimekwenda, nimeona nimetekeleza. Waheshimiwa Wabunge, tuambizane. Kama kuna kasungura, umwambie na mwenzako.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyo ninayemsema Mheshimiwa Mbunge, alianza na vyerehani vinne, leo ana vyerehani 30 na cherehani kimoja ni shilingi milioni tatu, ninety million, anaajiri watu wa kutosha. Kiwanda kidogo kinaajiri watu watano mpaka 49 na kina thamani ya milioni tano mpaka 200. Hivyo ndivyo sisi Wabunge tunavimudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha kati kinaajiri watu 50 mpaka 99. Shilingi milioni 200 mpaka shililngi milioni 800 na hivi Wabunge tunavimudu. Ndiyo vile viwanda vya akina Mheshimiwa Captain Rweikiza vya kutengeneza nyanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye viwanda vikubwa, vinaajiri watu 100 na vinatumia shilingi milioni 800 na kuendelea, ndiyo viwanda vya akina Mheshimiwa Salum, vya Jambo, ndiyo viwanda vya akina La Cairo, vimo humu. Kwa hiyo, hivyo ndivyo viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwaeleze Sera ya viwanda ambayo nilizungumza mimi na Mheshimiwa Mama Lulida, shangazi yangu. Ni shangazi yangu kweli, tumetoka mbali shangazi Lulida na wengine waliochangia. Sasa niwaeleze, sifa ya Sera kama walivyosema Wabunge na nimshukuru mtangulizi wangu Mheshimiwa Mama Mary Nagu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera yoyote ina sifa moja kubwa, lazima iishi muda mrefu, lakini na nyie mmechangia, kwamba sera mbona zinabadilika? Kumbe mlisahau, mnataka sera inayoishi muda mrefu, sasa ya 1996 mpaka 2020 huu ni muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uzuri wa sera hii kuliko yote, inazungumza mambo mawili ambayo mmeyasema. Inasema viwanda visambae Tanzania yote. Nani hataki viwanda visambae Tanzania yote? Kama imepitwa na wakati, kwa hiyo, tuibadilishe viwanda vikae sehemu moja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia inasema kwamba mikoa ya pembezoni ipewe vivutio; kwamba pamoja na vivutio kwa wawekezaji wote, lakini mikoa ya pembezoni ipewe more incentives. Kuna ubaya gani? Huwezi kwenda kuwekeza Kigoma bila kupewa incentives za ziada! Ni mbali sana! Uipiganie ndugu yangu Wamugabwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo hiyo Sera ya Viwanda ya Mwaka 1996 mpaka 2020. Kutokana na Sera hii, tumetengeneza mkakati wa integrated au fungamanisho la maendeleo ya viwanda, kutokana na Sera hii tumetengeneza vision ya 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka wakati huo mimi nilikuwa officer, Mwenyekiti wangu wa Bodi Profesa Mwandosya akiwa yeye anashiriki kwenye timu iliyotengeneza vision ya 2025, tumetoka mbali. Nilikuwa nabeba mkoba, sera hii inatengenezwa. Sasa ni mimi, Mr. mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, msambao wa viwanda. Viwanda vina namna mbili. Sera inasema viwanda visambae; wawekezaji wanapokuja, Serikali au Waziri uwezo wangu wa ushawishi kiwanda kiende wapi ni mdogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wanaokuja siyo mbumbumbu, wawekezaji wanaijua Tanzania kuliko tunavyoijua sisi. Akija Mjerumani anajua madini yako wapi. Labda wamwondoe Profesa Muhongo mtaalam wa miamba, lakini mwingine anakuja anakuonesha dhahabu ziko hapa. Ndiyo maana kila mara wanakuja wanajidai kwenda kuangalia makaburi ya babu zao. Wanaangalia yake mambo waliyoyaweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, viwanda viko vya namna mbili, FDI, nina influence kidogo ya kueleza ziende wapi. Kuna LGI (Local Grown Industries), ndipo tunapokwenda kwamba unaanza na kiwanda kidogo sana, unakilea kinakwenda kuwa kiwanda kidogo, kinakuwa kiwanda cha kati na kiwanda kikubwa. Mdogo wangu Mheshimiwa Kitandula, ni mdogo wangu kabisa, tumefanya kazi wote, nimemlea, nimemfundisha kazi, tumefanya kazi wote. Pole sana na Tanga Fresh.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Kitandula angeniambia kwamba barua yake iliyokwenda Hazina hawakushughulikia ningeshakwenda mimi. Naomba anikumbushe nitakwenda Hazina huyo aliyekata aniandikie mimi, I am a Minister, kwa nini alinyamaza? Mimi nilisema mtu huyu hana hatia afunguliwe, yeye akakaa na barua akanyamaza. Angeniambia ningemwambia Mzee Mpango, huyu ni mtu wa Mungu anaelewa. Unajua Mheshimiwa Mpango watu hawamwelewi, unamtegea wakati anatoka kusali unamwambia shida yako, atakusainia tu. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, viwanda vidogo sana, vidogo na vikubwa ndivyo viwanda tutakavyokwenda navyo ila watu wanavidharau kwa neno la viwanda vidogo. Waheshimiwa kiwanda cha shilingi milioni 200 kinazaa sana. Angekuwepo Mheshimiwa Katani angewaeleza mchanganuo na namshukuru sana Mheshimiwa Katani hata usiku nimemuota. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Katani, amenikumbusha Profesa Aba Mpesha, Baba Mchungaji wa kutoka Michigan University aliyenifundisha biashara ndogo na viwanda vidogo, aliyefanya utafiti wa korosho, watu wa korosho, wanasiasa wa Mtwara ndiyo waliomwekea mtimanyongo. Kama mnamtaka naweza nikampigia simu akatoka Michigan akaja, lakini kama mmejirekebisha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaeleze, wawekezaji wanakuja kule kwenye Mikoa na Halmashauri mnawawekea mtimanyongo kama ile kesi yangu ya Tabora. Mwekezaji ametoka China yupo uwanja wa ndege watu wakapiga figisu, wakamwambia umekuja Tanzania hupaswi kwenda Tabora, Tabora siyo Tanzania, yule Mchina akashangaa akarudi kwao. Inabidi niwaambie kusudi mwelewe tunayoyapata. Nichukue nafasi hii kumwombea kijana wangu Mheshimiwa Heche apone vizuri aje afanye kazi, tunafanana sura lakini ana pilikapilika nyingi. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ngoja niwaambie suala la Heche limekwisha, wale wawekezaji watakuja, mkitaka taratibu nitasimamia mimi wawekeze Tarime. Yale yamekwisha na nikitoka hapa nakwenda Dar es Salaam nikazungumze naye, mwambie afanye kazi moja mambo yamekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwaeleze Wabunge kuwapata wawekezaji ni shida, msiwaseme neno baya na Tanzania si nchi peke yake ya kuwekeza. Mimi napoteza wawekezaji wanakwenda Zimbabwe, Mozambique, Ethiopia, Rwanda na baya zaidi wanakwenda kuzalisha Rwanda kusudi sisi tugeuke soko, msiniumize.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaeleza FDI na LGI, LGI ndiyo inaweza kusambaa nchi zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo wa Tawala za Mikoa, tutafanya nini? Nimewaahidi kwenye hotuba yangu tunamalizia mwongozo, Wakuu wa Mikoa tutawapa mwongozo. Hii imetokana na nini? Baadhi ya Wabunge wananilaumu kwamba mimi napendelea mikoa fulani na mingine naiacha, tarehe 28 nakwenda Tanga. Niwaeleze Wabunge wa Tabora, Mheshimiwa Mwanry ameshafanya booking kwamba nikapige kongamano kule. Mjiandae Waheshimiwa wa Tabora, tupige kongamano na nimemweleza Mheshimiwa Maige rafiki zake wa Geneva awaambie na wenyewe waje watuletee viwanda twende Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naleta mwongozo kwa sababu imekuwepo kutolingana kati ya mkoa na mkoa. Ukifungua Facebook ni Simiyu, WhatsApp ni Simiyu, sasa tunataka kuwaambia Wakuu wa Mikoa wote waingie kwenye Facebook na Instragram na mitandao yote.
Ndiyo, wawekezaji wanatafutwa, kwa hiyo, nitatoa mwongozo wa kuweza kutekeleza hilo. Kwa hiyo, mwitikio wa mikoa haulingani lakini haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tutaandika mwongozo, nitauweka dibaji mimi, ataweka dibaji Mheshimiwa Simbachawene na Mkuu yeyote ataweka dibaji twende mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kasi ya ujenzi wa viwanda, nimeilezea fast tracking. Jukumu la ujenzi wa viwanda linatafsiriwa katika ujenzi wa uchumi wa viwanda seti kubwa na ujenzi wa viwanda vya subset. Sekta binafsi ndiyo itajenga viwanda, Serikali inaweka mazingira wezeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaeleza katika kipindi ambacho Mheshimiwa Rais yupo madarakani, viwanda vya sekta binafsi kwa address humu yaani mpaka wenye viwanda nimewawekea simu zao, wamejenga viwanda kwa mtaji wa shilingi trilioni tano, una mashaka wapigie simu, lakini nimeweka picha na beacon za mahali walipo unaweza kwenda ku-trace. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda niwaambie mimi siyo saizi ya kuzalisha viwanda vya shilingi trilioni tano kwa mwaka mmoja, I want more, ndiyo maana nikaleta fast tracking, ndiyo maana nikazungumzia kuweka mazingira bora ya biashara. Kwa hiyo, nashukuru na nyie hamridhiki sio saizi yetu tunapaswa kukimbia. Hatupaswi kuwa soko la watu wengine, tunapaswa kuzalisha tuwauzie watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ulinzi wa viwanda. Niwashukuru Waheshimiwa wote waliozungumzia kuhusu ulinzi wa viwanda. Sitaki kurudi nyuma, nimeshampongeza Kivuli changu, unajua ukiona Kivuli kina mashaka hata na mtu mwenyewe ana mashaka, sasa Kivuli changu ni kizuri siwezi kusema zaidi, lakini Nunua Tanzania inaendelea. Mwaka jana ilipigiwa sana kampeni na Mheshimiwa Makamu wa Rais alipozindua 620GS1 lakini tulipokwenda kutoa award za Brand 50 mshindi akawa Alaska Rice, huyo mama Alaska Rice ni mke wa Mheshimiwa Bashungwa, Mbunge mwenzetu, anatengeneza branded product zinapendwa Dar es Salaam Supermarket zote. Hata pilipili, watu wanaokwenda kununua wanasema nataka ile pilipili ya Alaska, branded na Mheshimiwa Mbunge. Jamani Wabunge muwe mnaambizana tunaishi vipi siyo tunakuona unaendesha mtambo mkubwa hutuambii, tuambizane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ulinzi wa viwanda tunauzungumzia. Ulinzi wa viwanda upo chini ya TBS, Fair Competition na upo chini ya Polisi. Niwahakikishie taasisi zilizopo chini yangu zitafanya kazi sasa kuliko wakati wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimehakikishiwa niseme ninachopewa na mimi nimekwenda kuwaambia wakubwa, bidhaa feki inapita, nimezungumza wakaniambia sema unachotaka nimewaambia, kwa hiyo, tutafanya kazi. Niwaeleze wawekezaji wengi kwa mfano kwenye sukari walikuwa wanakataa kwa sababu ya sukari inayokuwa smuggled in, kwa sababu ya mchele ulikuwa smuggled in, sasa watu wana confidence baada ya ku-control. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Mwigulu tu-control zaidi bado, bado, bado. Kwa hiyo, vitu vya feki na quality tutalizungumzia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie fungamanisho la viwanda na sekta nyingine. Waheshimiwa Wabunge kuna fungamanisho kuliko maelezo. Ukisoma mkakati wa pamba mpaka mavazi ni fungamanisho. Ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mwigulu huwa ananiita pacha. Ni kwamba mimi ndiye niliyebuni mradi wa viatu wa Karanga lakini mwenye dhamana ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Nilijua tukitengeneza viatu Magereza vitasambazwa katika majeshi yote na yule mzalishaji anapata soko la kuanzia, kuna fungamanisho hapo. Soma mkakati wa pamba mpaka mavazi kuna fungamanisho, soma mkakati wa alizeti kuna fungamanisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maziwa, soma Ripoti ya SAGCOT inazungumzia mradi wa maziwa. Nikiri kwa masikitiko kwamba hatufanyi vizuri kwenye maziwa, lakini mambo ya Tanga Fresh tutayashughulikia na viwanda vingine vianze. Niwaeleze jambo moja, ASAS ana kiwanda chenye uwezo wa kuchakata lita 50,000 kwa siku lakini maziwa anayopata ni lita 12,500. Kwa hiyo, kuna haja ya kuweza kuwasaidia watu wa Nyanda za Juu Kusini kuweza kuzalisha maziwa zaidi na chini ya hapo atakuja aeleze Waziri wa Kilimo ndiyo tunakuja na mpango wa SAGCOT wa kuleta IFAD kutoka Ulaya kusudi waende kule. Sitaki kusoma hotuba ya mwenzangu ngoja aje aseme mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya kipaumbele, nitafika baba ikibidi nitaomba muda. Ipo hoja ameuliza Mheshimiwa Mbunge, jina lake nimelisahau kidogo ila ame- declare interest kwamba yeye ni mwana Tanga na mimi Tanga nakwenda tarehe 28, kwa hiyo, huenda tutakutana huko. Nakwenda kupiga, mnaita sound, kuhamasisha viwanda, anasema tuwe na kipaumbele. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Saruji cha Simba, kimeongeza uwezo kwa tani 750,000, ndiyo alichokizungumza Mwenyekiti wa Kamati yangu kwamba ile nafuu waliopaswa kupewa haijatoka. Mwenyekiti wa Kamati na wewe ni sehemu ya Serikali waambie watu wa Tanga walete karatasi zao tutakwenda Hazina wanieleze mimi kwa nini hawatoi. Kama mtu amewekeza na tani zinaonekana kwa nini msimpe? Halafu unajua watu sijui kwa nini, mkikwama huko mje kwangu, mimi ndiyo Waziri mwenye dhamana nitawapeleka huko mnakoshindwa kufika. Wanasema huwezi kwenda kwa Baba mpaka upite kwa Mwana, Mwana ni mimi. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukisoma mkakati wa fungamanisho la viwanda, Mheshimiwa Mbunge aliyesema hatuna kipaumbele, kwenye mkakati wa fungamanisho la viwanda imeelezwa na hicho kiwanda kingine cha Tanga kitazalisha tani milioni saba, kitawaajiri watu milioni nane na 60% ya saruji itauzwa nje ya nchi, sisi tutabaki na 40%. Kinawekwa jiwe la msingi, kwa sababu sina mamlaka ya kutamka kinawekwa jiwe la msingi mwaka huu, kitapata vivutio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa aliyesema kwamba hatuna vipaumbele asome mkakati wa fungamanisho la viwanda liko kwenye website yangu. Tutaweka kwenye viwanda vya sukari, Mkulazi tani 2000, Mbigiri 30,000, tutapanua Kagera Sugar na Kilombero. Juzi mbele ya Mheshimiwa Rais nimemueleza Mheshimiwa Zuma kwamba aisaidie Ilovo iongeze Kilombero One na Kilombero Two waache kutonunua miwa ya wananchi, kwa hiyo tumeyazungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hilo kuna pamba, mafuta ya kula ya alizeti, ngozi na bidhaa za ngozi na matunda. Kwa matunda ndiyo tunazungumza na Kiwanda cha Matunda cha Sayona. Nimewasikia Ndugu zangu wa Tanga, tunazungumzia Kiwanda cha Eveline lakini tunazungumzia Kiwanda cha Matunda cha Handeni, kwa hiyo, tunaendelea na imeainishwa. Tunazungumzia maziwa, tunaweza kuwa hatujatekeleza kama alivyosema Mheshimiwa Kitandula lakini ndiyo dhamira yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumziwa viwanda vya nyama, watu wa Manyara mwambie yule mwana mama aliyekuwa na matatizo ya kiwanda chake cha nyama, matatizo yake yameainishwa kwenye Ripoti ya Profesa Mkenda. Wale waliokuwa wanamkwamisha, sitaki kuwasema wasijisikie vibaya wakashindwa kula, dawa yao imeshapatikana aje tumpeleke wampe nyaraka zake. Unamkwamisha mtu na kikaratasi asitengeneze kiwanda cha nyama, ng’ombe wanakwenda Kenya wanarudi, ningependa tuwe wawazi tuambizane. Hicho ni kiwanda cha Chobo Investment kipo Mwanza, anachinja ng’ombe 600 kwa siku, kijana amejaribu. Matatizo yako yote watayasema kesho kwenye Wizara inayohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda vya chakula na katika hili niwaeleze, nimekuwa nikisema hapa Bungeni, nikiwaambia Waheshimiwa Wabunge hakuna sababu ya kutoa mahindi Katavi kuyapeleka Dar es Salaam, msage mahindi kule, mfanye packaging vizuri, muweke kwenye maroli mpeleke sokoni. Ndiyo maana nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Aeshi ametengeneza kiwanda kikubwa sana cha kusaga nafaka na zitakuja sokoni. Waheshimiwa tuambizane, kama umewekeza mwambie mwenzako wewe umepata wapi namna, tuelezane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na rafiki yangu mmoja Kenya nilipotaka kuingia kwenye siasa nikamuaga aliniuliza Mwijage utaziweza siasa. Nikamwambia nitaziweza, I can talk. Akaniambia politics is not about talking. Akaniambia ninyi Watanzania mna tatizo moja. Akaniuliza adui yenu ni nani? Nikamwambia umaskini. Akaniambia mbona mnaogopa utajiri? Ukikutana na mwanasiasa wa Tanzania ukimwambia wewe tajiri anasema mimi maskini bwana, hapana! Mheshimiwa Aeshi amejenga kiwanda cha mfano cha kutengeneza nafaka, tunataka hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanasema sembe nzuri inalimwa Ileje. Mheshimiwa Mbunge wa Ileje, jasiria, SIDO wanakuja weka kiwanda Ileje, mjini tunataka watu waondoke warudi shamba, zile by-product, mmetoa mfano mzuri wa pumba zibaki kule. Akinamama wapepete mahindi, wafanye packing, wakaangalie watoto wakimaliza pumba wawape mifugo, nazungumzia mifugo ng’ombe sizungumzii astaghfiru Allah. Unajua kuna wengine pumba wanamlisha astaghfiru Allah, hapana. Wamlishe ng’ombe akamuliwe maziwa, akikamuliwa maziwa mama auze na mtoto anywe. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maamuzi ya Serikali ni kwamba ziliko rasilimali ndiko vitajengwa viwanda. Ndiyo maana Mheshimiwa wa Simiyu, maamuzi yamefanyika kiwanda cha vifaa tiba vitokanavyo na pamba nimeandika kwenye ripoti kitajengwa Simiyu kitatumia pamba tani milioni 50 na kitatuokoa na aibu ya kuagiza vifaa pamba toka nje. Tuna aibu nyingi na tutazimaliza. Tunaagiza hata drip ile ya kumwekea mgonjwa kutoka Uganda, hizo aibu zote tunazifuta. Soma ripoti hiyo, mimi aibu zote nimezianika kusudi mnione halafu mnipange vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema yote haya ili Waheshimiwa Wabunge wasiwe na tatizo la kuangalia vifungu ila wakubaliane tupitishe moja kwa moja. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ni petrol chemicals. Petrol chemicals ni vile viwanda vya Mheshimiwa Muhongo. Kiwanda cha Ferrostaal Mheshimiwa Muhongo amekwenda zaidi mpaka ametaja tarehe ya kwenda Kilwa na mimi nimeshapata mwaliko kutoka Ujerumani, Profesa nitakuwa karibu na wewe. Unajua watu siku hizi wananichanganya na mimi wananiita Profesa, kwa hiyo, tutakuwa wote. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kiwanda Ferrostaal karibu kitaanza na kiwanda cha Helium kitaanza, kwa hiyo ni petrol chemicals zimeandikwa. Nawaeleza vipaumbele mvijue kwa sababu uwekezaji katika kiwanda cha mbolea utatuwezesha kuzalisha mbolea tani 2,600,000 katika viwanda viwili wakati mahitaji ya mbolea Tanzania mnatumia tani 400,000. Kwa hiyo, is a break through tutatumia mbolea zaidi, tutapata tija na viwanda vitafufuka. Ni kwa uwekezaji wa namna hiyo kuongeza tija ginneries zitafufuka, akina Manonga watafufuka pamba ikizalishwa kwa wingi na tukawa na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya uwekezaji, Kurasini Logistic Centre. Kama nilivyoeleza kwenye ripoti yangu inatengenezwa. Mheshimiwa Ngwali, Kurasini Logistic Centre haiwezi kufika mwezi Julai. Nichukue fursa hii kuwaeleza watendaji ninaofanya kazi nao, mimi huwa nasema wazi, nimeshamwambia Waziri Mkuu kwamba performance ya EPZ si nzuri kwenye Kurasini Logistic Centre.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewaandikia memo Makatibu Wakuu wangu kwamba I am not happy na speed ya EPZ on Kurasini, nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu baada ya hapo ni kwenda kwa tajiri. Naitaka Kurasini Logistic Centre ianze, namna nilivyokaangwa hapa na rafiki yangu Mheshimiwa Ngwali siwezi kukubali mimi ni mtu mzima. Kurasini Logistic Centre tutakuwa na nafasi nzuri kabla ya Bunge kuwaambia ni kitu gani kinafanyika, ikibidi kuitisha Bodi nitaitisha Bodi. Naitaka Kurasini Logistic Centre, mimi ni mtu wa Temeke nani asiyejua bwana, Mbunge wangu yupo hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bagamoyo Special Economic Zone, bandari ipo na itachimbwa na mwekezaji. Nimeulizwa kwa nini tumetaka private sector ilipe fidia? Mimi wazo hili nimelipeleka kwa wakubwa nikajenga hoja wakanikubalia. Wewe mtu umemthamini mwaka 2008 unamlipa kidogo kidogo huwezi kuona, tena Kamati yangu ndiyo iliniambia kwamba Mwijage itakuhitaji miaka 30 kumaliza, basi nikawaomba wakubwa tutafute private sector wameingia lakini malipo yote tutayasimamia sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze nimepata barua sasa hivi, kuna mwekezaji nguli kutoka China ananifuata hapa anataka nimpe eneo la kuweka Special Economic Zone. Nimeshawaeleza watu wote tunaofanya kazi pamoja, watu wa EPZA, Makatibu Wakuu mnahusika, huyo Mchina hata asiponiona mimi mpelekeni Bagamoyo, mpelekeni Kibaha, ninazo hekari 5,000 Kibaha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze watu wa Pwani, Mheshimiwa Subira Mgalu na Wabunge wote sijawahi kuona ukarimu kama wa Pwani. Mkuu wa Mkoa anachosema ndicho anachosema Diwani. Unajua ngoja niseme niokoke na nitakayemsema msimchukulie hatua yoyote. Watu wa Morogoro waliniangusha na nimemwambia Mzee Mbena. Nimemleta mwekezaji toka Singapore amefika pale Madiwani wanatokea huku wanakwenda huku, tumepoteza viwanda vitano kutoka Mauritius juzi vyenye kuweza kuajiri watu 7,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwaambia nina kiwanja Morogoro, wakienda Morogoro wanatokea hapa wanaingia hapa, mara umeme mara nini. Umeme hauwahusu, umeme mniambie mimi, mimi Mzee Muhongo naongea naye wakati wowote, substation ni shilingi bilioni tatu, mbele ya kuingiza wawekezaji watano wanaozalisha ajira 7,000 ni kitu gani?
Mheshimiwa Devota nisaidie hilo, acha longolongo na mambo ya master plan tunataka eneo lile. Kwa hiyo, Bagamoyo itatekezwa na watu watalipwa haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TAMCO Kibaha, tunaendelea kutekeleza. Maeneo ya mikoani, Kigoma na Songea kwenye bajeti nimewaweka. Kwenye bajeti inayokuja naomba mnitendee haki msome vitabu vyangu. Mheshimiwa Special Economic Zone, nimesaini kwa mkono wangu Special Economic Zone nane za sekta binafsi, kwa hiyo, Serikali inapenda sekta binafsi. Nitambue nafasi ya Waheshimiwa Wabunge walioniahidi kunipa maeneo, Mheshimiwa Bashe taratibu, kama sikuwekeza leo na kesho ipo, wewe niombe nibaki kwenye nafasi hii. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwezesha SME, SIDO, TBS na TanTrade wamekuwa wakiwezesha SME. Ninachotaka kuwaambia hatutalegeza viwango hasa kwa wale watengenezaji wa chakula, TFDA atashirikiana na TBS hatutalegeza viwango. Ila katika maelekezo ya Serikali za Mikoa mnapotenga maeneo wale akinamama, watu wamehoji nimesema nini kwa akinamama, akinamama muwajengee mabanda ambayo TBS atawapa mafunzo. TBS atakupa mafunzo na certificate na gharama za certificate atalipa yeye mpaka utakapokuwa mjasiriamali mwenye nguvu. Nimetoa maagizo na mamlaka inaniruhusu kufanya hivyo, akinamama niwapende zaidi ya hapo niwapende namna gani? (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuongeza hisa kwenye makampuni. Jambo ambalo nimekuwa na ushawishi nalo ni Urafiki. Mwekezaji wa Urafiki amekubali kupunguza hisa zake alikuwa na hisa 51. Majadiliano yanaendelea, wanafanya valuation na tumeshapata wawekezaji wa Tanzania. Kwa hiyo, hicho ndicho naweza kusema kuhusu Urafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TANALEC, sina mamlaka nayo ila mimi nawashawishi TANALEC waende kwenye Dar es Salaam Stock Exchange. Hata hivyo, katika kulinda uchumi wa viwanda Mheshimiwa Muhongo alishasema na kwenye tenda zake amesema transformer na cables zote zote kwenye REA Awamu ya Tatu zitanunuliwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, orodha ya viwanda ni kubwa, kuna kiwanda kimejengwa Tanzania cha kutengeneza waya, kina uwezo wa kutengeneza kilometa 100 za waya kwa masaa nane kiko Mwenge. Viko vitatu kimoja kiko Nigeria, kingine kiko Mwenge na kingine kiko South Africa, ni kijana mdogo ukimwona hutaamini.
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya makaa ya mawe. Mheshimiwa Profesa Muhongo amezungumza lakini mojawapo ya faida ya kutumia makaa ya mawe ya Tanzania yamechangamsha uchumi. Pale wanapopita wenye malori, mama ntilie anapika lakini spea na mechanic wanatengeneza Watanzania. Naomba mtuelewe, tumefanya hivyo kwa nia nje lakini hali hiyo imefanya wenye migodi waone kwamba kuna soko wamefungua migodi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie korosho. Maelezo aliyozungumza comrade Mwambe, unajua ukiwa comrade hata ukijipaka matope mtu akikuangalia tu michango yako ni ya ki-comrade tu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, michango yake Mheshimiwa comrade na mchango wa Profesa Masawe wa Naliendele tutaufanyia kazi na tutamuunganisha na COSTECH kusudi zile bidhaa zinazotokana na korosho tuweze kuzitumia. Suala ni research na Profesa Masawe amefanya research, kuna bidhaa nyingi, brake lining na kile kinywaji ambacho wewe ukikiangalia unasema astaghfur Allah lakini kinaingiza pesa. Kwa hiyo, vyote hivyo tutavishughulikia na naomba tuendelee kufanya kazi wote. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kipekee kuna faida kwa kuchambua korosho hapa ndani tunaposhughulikia viwanda vilivyobinafsishwa. Kama alivyosema Mheshimiwa Kitandula zile export levy, mabilioni yale, tutakaa tuwaulize wenye dhamana kama tunaweza kuchukua viwanda vya kuanzia kusudi msimu unaokuja tuweze kuanza na baadhi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la CBE. Mheshimiwa Mwita ameleta suala la CBE akalipitisha kwa Mheshimiwa Ngwali akaona haitoshi akalipitisha kwa Mheshimiwa Mwambe akaona haitoshi, ikanipa shida. Nikaenda kutafuta Ripoti ya CAG.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Waitara ni kwamba waliokwenda kukagua CAG hakukagua Dar es Salaam. Nakala niliyo nayo iliyowekwa lakiri na CAG anasema yeye CAG alikagua Dar es Salaam, lakini kwa mamlaka ya kiutawala, Waziri nikishapata ripoti, siruhusiwi kufanya lolote kwa watendaji napitia kwenye Bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waitara najua yeye amesoma sayansi mambo ya utawala hayajui. Ukiingilia moja kwa moja watendaji bila kupitia kwenye Bodi akienda mahakamani anakushinda. Kwa hiyo, mimi nimepata ripoti yangu nitaiandikia Bodi na itachukua action isipochukua action ndio mimi kwa mamlaka niliyonayo au kwa mamlaka ya uteuzi naweza kuchukua hatua. Nimhakikishie I have the report anaweza kuisoma, nimemshikilia kwa sababu imeandikwa siri na yeye siyo mmoja wa siri, sisi ndiyo watu wa siri, kwa hiyo mambo ndiyo hayo CBE Dar es Salaam ilikaguliwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, naomba nihitimishe kwa kuwashukuru kwa namna ya kipekee Waheshimiwa Wabunge na kupitia kwenu Watanzania wote ambao tunawawakilisha kwa ushirikiano mnaotupa katika kuendeleza sekta yetu na hususan ujenzi wa uchumi wa viwanda. Wizara daima itaendelea kuwa sikivu, kupokea mchango wa mawazo na ushauri katika kuboresha utendaji wa Wizara na sekta kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe kuendelea na ushirikiano huo katika kuhakikisha kuwa rasilimali tunazozipata zinatumika kwa umakini mkubwa ili mipango na mikakati ya sekta iweze kuleta matokeo chanya katika kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025. Ni dhahiri kuwa ushiriki wa sekta binafsi na uthubutu wao ni nyenzo muhimu katika kuleta mageuzi na matokeo yenye ushindani utakaotokana na juhudi za uendeshaji na uanzishwaji wa viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo, biashara ndogo pamoja na uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu letu tukiwa ndiyo wawakilishi wa wananchi wetu kuwajengea ufahamu wa mipango, sera, mikakati mbalimbali ya kisekta ili kuwaongoza ipasavyo katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.