Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Newala Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nipate kuchangia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Newala Mjini. Mimi nataka kutangulia kusema naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza vijana wangu wa Young Africans Sports Club kwa kuchukua ubingwa wa nchi hii kwa mara ya tatu, kama nilivyowaagiza vijana, nataka mje Dodoma, mcheze mpira hapa Dodoma lakini mje na kikombe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka pia niwapongeze vijana wetu wa Serengeti Boys kwa kazi nzuri waliyoifanya jana kuifunga Angola. Nataka niwashukuru Watanzania wote waliochangia Serengeti Boys kufika mpaka pale na mimi nina imani watafika mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mkulima wa korosho, kwa hiyo nitazungumza masuala ya korosho. Kwanza, nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wakulima wote wa korosho katika nchi hii kwa sababu mwaka huu zao…
T A A R I F A . . .
MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo nimeipokea na ninawaagiza vijana wa Yanga wakashinde mechi iliyobaki ya Mbao ili mjadala wa mezani usituhusu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimesema nawapongeza wakulima wa korosho nchi nzima, mwaka huu limekuwa zao la kwanza kwa kuingiza mapato mengi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, leo mimi nina furaha sana, hakuna mjadala wa Wizara ya Kilimo ninaouchangia kwa raha kama leo kuliko mwaka wa jana. Kuna sehemu moja tu sijaridhika na nitawaambia, lakini nataka nianze kuipongeza Serikali kwa kutufanyia yafuatayo wakulima wa korosho. Kwanza Bodi imeundwa upya, juzi tulikuwa na mkutano wa wadau, ulikuwa mzuri, nawapongeza, hatujawahi kuwa na mkutano wa wadau mzuri kama wa mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nikupongeze ndugu yangu Waziri kwa kuvunja ule uongozi wa Mfuko wa Uendelezaji wa Zao la Korosho, pale palikuwa pananuka rushwa. Watu waling’ang’ania pale, kila mwaka ni hao hao, ukitaka uwabadili haiwezekani, walikuwa wanafanyaje, wanajua wao. Na tumeona matunda sasa kwamba ule mfuko umekuja kwenye bodi mwaka huu, nitaeleza baadaye matunda yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza tena Serikali, juzi mmetutangazia, na ninataka wakulima wote wa korosho Mtwara, Mkinga, Pwani, Lindi mjue kwamba Serikali yenu juzi imetutangazia mwaka huu tutagaiwa sulphur bure, hiyo ndiyo neema ya Serikali ya Awamu ya Tano, tutagawiwa magunia bure, Mungu akupe nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nataka kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuondoa kero, mimi sitaki kurudia, lakini nataka kutaja zinazonihusu mimi mtu wa korosho. Kero ya unyaufu, mtunza ghala, task force, usafirishaji, ushuru wa chama kikuu; ninaiomba tu Serikali mkishafuta haya mhakikishe kwamba mikoani kule inatekelezwa kama mlivyoagiza. Kwa sababu msimu wa mwaka jana kuna mikoa ilipindisha baadhi ya maagizo ambayo mliyatoa, watu kule wakatozwa unyaufu, wakatozwa task force. Mheshimiwa Waziri, mimi naomba maagizo yatekelezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue nafasi hii kupongeza sana Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Sisi kule Mtwara, Lindi, tunasema Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ndiyo mkombozi wetu. Tumepata bei nzuri ya korosho mwaka huu, kubwa sana. Na hii imetokana na ushindani, siku zote wananunua India peke yake, mwaka huu wamekuja Vietnam, ushindani ule ndio umetufanya tupate bei nzuri. Wapo watu wanasema wao ndio wameongeza bei ya korosho, kama wewe umeongeza bei ya korosho, je, nani ameongeza Lindi, nani ameongeza Mkinga?
Mheshimiwa Naibu Spika, korosho mwaka huu tumepata bei nzuri kwa sababu ya ushindani katika mtindo wetu wa stakabadhi ya mazao ghalani kwa sababu ya ujio wa watu wa Vietnam.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkitaka kujua Watanzania kwamba kweli mwaka huu tumenufaika na korosho, mwaka jana wakulima wa korosho tuligawana shilingi bilioni 203 tu basi, lakini msimu huu uliomalizika tumegawana bilioni mia nane na tisa, kutoka shilingi bilioni 203 mpaka shilingi bilioni 809, hii ni hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nihame hapo niende kwenye ushirika; hapa ndipo niliposema, nimesema na kusema. Mheshimiwa Waziri ushirika una misingi yake, Rochdale Principles za Cooperative Unions. Rochdale Principles za Cooperative Unions zimekuwa ndizo zinazofuatwa na International Cooperative Alliance. Moja inasema democracy ndani ya vyama, Serikali ihakikishe kwenye ushirika kuna democracy. Sisi kule Mtwara tuna chama kinaitwa TANECU, kina vyama 55 Newala na 124 Tandahimba, jumla vyama 179, hawawezi kusimamia hawa, kama ingekuwa kompyuta unasema computer overload, ndivyo ilivyo TANECU, Newala, uongozi unashindwa kwenda chama kwa chama.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka miaka mitatu iliyopita, wameomba vyama Newala kwa muhtasari, Tandahimba kwa muhtasari, tunaomba mkutano mkuu union tugawe chama hiki, Mrajisi akaandika barua akasema gaweni, Mrajisi aliyekuwepo amehudhuria mikutano yote, agizo lake la kusema gaweni halikujadiliwa hata siku moja. Naomba Serikali kwa madaraka ya Mrajisi gaweni TANECU kwa sababu ndiyo matakwa ya watu wa Tandahimba na Newala. Mwaka jana, mwaka huu Council ya Newala, Council za Tandahimba wameomba kugawa TANECU ili pawe na ufanisi. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri, mimi na wewe tunapatana kweli, tunakosana katika hili moja tu basi, hili ukilimaliza basi! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka kusema hayo, lakini neema ya hela iliyoingia mwaka huu Mtwara imesababisha watu wengine kujitokeza uhodari wa wizi hasa kule Masasi, wizi mkubwa kwenye vyama vya msingi, mmekagua mmekuta shilingi bilioni tatu zimeliwa mmewabana wamerudisha, sasa bado shilingi bilioni 1.4 hazijarudi. Mimi naiomba Serikali, viongozi na watendaji walioshirikiana na vyama vya ushirika kutuibia hela yetu ya korosho wote washughulikiwe na vyombo vya dola, wote, msibague, msishughulike na vingozi wa vyama vya msingi peke yake, tazameni nani alishirikiana nao na yeye aende akasimame mahakamani. Hapo ndipo watu wa Mtwara na Lindi tutafurahi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niseme ushirika wa TANECU umeandikishwa kama ushirika wa mazao, lakini wananunua korosho peke yake. Naomba Waziri, Vyama vya Ushirika vinunue na mazao mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa ushirika, nasema moja ya misingi ya ushirika niliyosema (Rochdale Principles) inasema corporate social responsibility, chama kikitengeneza faida kirudishe kiasi cha hela ile kwenye jamii, watengeneze barabara, wasaidie shule, wasaidie hospitali, vitanda vya wagonjwa; TANECU tangu imetengenezwa faida miaka nenda rudi, tumewasema, juzi ndiyo wameanza kutoa mifuko kumi ya saruji kwa ajili ya sekondari. Hivi hela inayotengenezwa TANECU unatoa mifuko kumi, si aibu? Mbona mifuko kumi mimi naweza kuitoa hata ukiniamsha usingizini? Kwa hiyo, wasimamieni, waulizeni kuhusu corporate social responsibility wanafanya nini.
Sasa mimi nataka kurukia kwenye suala la mihogo. Mimi nimeshukuru Serikali yetu imesaini mkataba na China, sisi Mtwara ndio wakulima wakubwa wa mihogo, mwaka 1974 nchi hii ilipata njaa, wakati National Milling inanunua mihogo tumelisha mikao kumi, mihogo iliyokuwa imenunuliwa na National Milling Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtwara tuko tayari kupeleka mihogo China, Mheshimiwa Waziri tuambie lini inahitajika, tumeacha kulima mihogo kibiashara (commercially) tunalima tu ya kula sisi wenyewe, tumefurahi kusikia neema hiyo ya China.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, naona kengele kama inapiga, sisi kule pia tunalima soya, soya ile imesimama kwa sababu haina soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho, naomba ndugu yangu simamia vile viwanda viwili vya korosho Newala vifufuliwe, wale watu walionunua, kimoja kinafanya kazi kwa robo na kingine hakifanyi kazi kabisa. Ahadi ya Rais alipokuja Newala ilikuwa kwamba viwanda hivi tutavifufua ili wananchi wa Newala wapate ajira…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. KEPT. MST. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nampongeza sana mdogo wangu Waziri, ameanza vizuri aendelee vizuri pamoja na Naibu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.