Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata nafasi, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu nilianzia kwnye bajeti ya Waziri Mkuu nikatoa 50 percent, nikazungumzia suala la tangawizi ka ulimwengu, nikazungumzia suala la tangawizi kwa Afrika na nikasema nusu nitazungumzia suala la tangawizi kwa Tanzania na ninaanza hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakapozungumzia tangawizi Tanzania moja kwa moja utaigusa Wilaya ya Same, upande wa Mashariki mwa Wilaya ya Same ambao wao wenyewe katika nchi hii wanalima takribani asilimia 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna asilimia 40 iliyobaki, asilimia 40 sasa hivi inalimwa na Songea Vijijini ukienda Jimbo la Madaba wanalima tangawizi sana, ukienda Mkoa wa Kigoma wameanza kulima tangawizi sana kwa hiyo, ukiangalia vizuri Tanzania sasa hivi zao la tangawizi linakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuzungumzie safari ya maendeleo. Maendeleo ni safari ambayo ina misuko suko sana, hasa niongelee maendeleo yanayotupeleka kwenye viwanda na uchumi wa kati. Tusitegemee tufike kwenye viwanda, tufike kwenye uchumi wa kati kwa lele mama ni lazima tukutane na misukosuko mingi. Sasa mimi naomba niizungumzie hii hii tangawizi ya Same Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilianza kuwa Mbunge mwaka 2005 Same Mashariki, niliwakuta wananchi wanalima tangawizi. Mwaka 2007 mimi ndiyo nikaasisi wazo la kujenga Kiwanda cha Kusindika Tangawizi pale Same Masharuki. Tulianza kwa misukosuko mingi, lakini nakumbuka mwaka 2008 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyepita Mheshimiwa Mizengo Pinda alikuja akaweka jiwe la msingi, tukajenga, tukahangaika mimi na Halmashauri na wananchi wakati huo tulikuwa na wana ushirika 613, wao walichangia shilingi 6,000, mimi kama Mbunge pamoja na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne tulifanya fund raising tukapata shilingi milioni 301; Halmashauri ikachangia shilingi milioni 45, lakini na Serikali ikatujengea godown lenye thamani ya milioni 287 na safari ikafikia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nizungumze kitu ambacho kinanipa nguvu sana leo na ninaomba Waheshimiwa Wabunge mfurahi pamoja na mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais amekuja na kauli ya Tanzania ya viwanda, lakini Mheshimiwa Rais kazi anayofanya ni kuchochea na kuwavuta watu, kuivuta mifuko ya jamii iwekeze kwenye viwanda kwa sababu by principle Serikali haijengi viwanda, lakini ina-facilitate. Sasa nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na nashukuru kwamba yupo hapa. Leo nazungumza jambo ambalo limenifariji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani zangu za pili, tena hizi ni shukrani za unyenyekevu na moyo uliopondeka sana nipeleke kwa Bodi ya Wadhamini wa LAPF, nipeleke shukurani zangu za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa LAPF Ndugu Eliud Sanga kwa sababu LAPF imekubali kuingia ubia na kile kiwanda nilichokijenga miaka ile. Leo tunazungumza LAPF inakwenda Same Mashariki, inakwenda Miamba, inakwenda kuingiza zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye kile kiwanda, sasa hapo unazungumzia ile ndoto niliyokuwa naiona kila siku. Nilikuwa natamani tupate kiwanda kama cha Kaduna, Nigeria kwasababu gani sasa mimi nimepata furaha? LAPF inadhania imefanya kitu kidogo, hapana, imefanya mambo matatu makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, LAPF kwa kuingia ubia na Kiwanda kile cha Same Mashariki cha Tangawizi cha Miamba inepanua kilimo cha tangawizi Tanzania kwa sababu wakulima wa tangawizi wa nchi nzima watakuwa na uhakika wa kupata soko. Kiwanda kile kinajengwa na watu wenye uwezo wa kifedha, kinapanuliwa lakini walima tangawizi wote wa nchi hii, walima tangawizi wa Madaba, Wilaya ya Same, Kigoma wote watakuwa wana mahali pa kuuza tangawizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, inatuweka kwenye nafasi nzuri ya sisi kuingia kwenye export. Nigeria wenyewe kupitia kiwanda chao cha Kaduna kinachoitwa Kachia wana-export asilimia tisa yaani katika soko la dunia ile tangawizi iliyoko kwenye soko la dunia kuna asilimia tisa kutoka Kaduna. Hii ni kwa sababu wana Kiwanda kikubwa cha Tangawizi cha Kachia ambacho kiko kwenye state ya Kaduna ambapo wananchi wa Nigeria wanaolima tangawizi wote wanauzia pale na kile kiwanda kina-export 92 percent ya tangawizi ambayo inasindikwa pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi ninakiona Kiwanda cha Miamba, hiki ambacho LAPF sasa inaingia ubia pale kama ni pacha wa hiki Kiwanda cha Kaduna cha Nigeria. Hivyo hapo lazima tukubali kwamba LAPF imemuunga mkono Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais anazungumzia viwanda kwenye nchi hii, anachochea viwanda kwenye nchi hii, LAPF ilipokwenda kuingia ubia na kile kiwanda cha tangawizi imemuunga mkono Mheshimiwa Rais, ninawashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu ambalo si dogo; hakuna kitu kinachomuumiza mkulima kama alime halafu hana soko. Mimi ninalima tangawizi si kwamba ninaihubiri tu, mimi ni muanzilishi wa kile kiwanda, nalima tangawizi. Kule Same nimekosa nafasi kwa sababu ardhi ya Same yote imejaa tangawizi kwa hiyo imebidi nitafute makazi, mimi nina makazi yangu Madaba kwa Mheshimiwa Mhagama, nalima tangawizi, nimeanza na hekari 20, kuanzia Julai navuna. Hata hivyo siri ya tangawizi si lazima nivune Julai, naweza nikaiacha kwa mwaka mzima, itategemea kama nina soko. Tangawizi unaweza ukaiacha chini ya ardhi kwa mwaka mzima na ikakusubiri upate soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba niseme ukweli kuwa wakulima wa tangawizi ambao tuko Madaba na tuko wengi tunalima tangawizi kwa wingi na sisi hiki kiwanda ni faida kwetu kwa sababu kile kiwanda kitachukua tangawizi ya nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine lazima tujifunze, hiki kiwanda kikubwa kilichoko Nigeria ni mali ya Serikali. Ni Serikali ya Kaduna imekijenga sasa lazima sisi tujipe big up, tumeanza wananchi, mimi kama Mbunge nimetoa lile wazo, wananchi 613 wakachangia shilingi 6,000, Rais Kikwete akaniunga mkono kwenye fund raising tukapata shilingi milioni 301, Halmashauri ikaniunga mkono na sasa LAPF inakuja inatuunga mkono hapo ni lazima tuone kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inafanya vizuri. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia, sitaki kuogongewa kengele. Kwa moyo uliopondeka na kwa unyenyekevu mkubwa niishukuru LAPF, nawashukuru sana na huko walipo wajue wameitendea nchi, hawakumfanyia mtu, wameifanyia nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa nakushukuru kwa dakika ulizonipa, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI amesaidia hili kuwezekana namshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.