Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu na mimi nichangie bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Msemaji aliyenitangulia mimi amesema sana, lakini mimi naomba niseme ukweli kwamba Wizara hii inafanya kazi sana. Tuseme ukweli Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inachukua asilimia 75 ya Watanzania wote, lakini bajeti yao si asilimia 75 ya bajeti yote, hili lieleweke hivyo pia. (Makofi)
Kwa hiyo kidogo ambacho wanapata kinatufikia vijijini lakini hakitoshi, si mapungufu ya Wizara hii, ni mapungufu ya hali halisi ya uchumi wa nchi. Nina uhakika Mheshimiwa Rais akifanikiwa katika malengo ambayo anataka kutupeleka tukapata hela za kutosha ataangalia kundi kubwa hili la asilimia 75 ya Watanzania wanaoishi vijijini. Kwa sasa twende kama tulivyo. Hata hivyo tusahihishe makosa ambayo tunafikiri tunayoweza tukayasahihisha ili kuweza kuleta ufanisi zaidi kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na kero za asilimia 75 ya Watanzania wote wanaoishi vijijini ambayo ni mbolea au pembejeo za wakulima, lakini pia vyama vya ushirika na tozo kwenye mazao ya wakulima. Nimesoma sana hotuba hii na yote nimemaliza. Ingawa tumeipata leo lakini sikupumzika mchana. Yako mambo ambayo tunaweza tukayasahihisha, yako mambo tunaweza kusema okay,
twende nayo mpaka hali itapopendeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la mbolea. Mimi nimegombana, nimepigana sana kupata zile vocha za ruzuku lakini hazisaidii, mbolea haifiki kule, vocha zinafika, wazee wale wasiojua kusoma wanasainishwa vocha lakini mbolea hawakupata, wanapewa hela kidogo na wanaosambaza hizi mbolea za ruzuku wanachukua hela. Lakini nimeona leo Serikali inakuja na mfumo mzuri ambao nillikuwa sikuutegemea kabisa. Mfumo huu tuliutumia kwa ubunifu mkubwa kwenye ununuzi wa mafuta kwa pamoja na EWURA wakasimamia. Sasa naambiwa tutanunua mbolea kwa pamoja (bulk procurement) halafu Shirika la Mamlaka ya Uboreshaji wa Ubora wa Mbolea lisimamie ununuzi huu. Hii pekeyake ndiye mkombozi wa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila treni bora ina kasoro yake isije ikatokea usimamizi ukalegalega na hili shirika la usimamizi wa ubora wa mbolea sasa lisimamie usimamizi wa ununuzi wa mbolea bora. Neno ununuzi liongezeke pale ili tuweze kupata bei nzuri na wakulima waweze kununua mbolea kwa hela yao. Sasa hivi haiwezekani mbolea mimi nimekwenda Ulaya kufuatilia bei za mbolea mfuko mmoja wa mbolea dola 25 na hapa tunasema imepunguzwa bei dola 42, 43 mara mbili/mara tatu zaidi. Lakini mbaya zaidi kampuni inayoagiza mbolea iko moja tu, kwa mfano NPK na sitaki kuitaja kampuni hiyo. Hiyo ndiyo inayogawa mbolea kwa wauzaji wengine halafu nayo ina-bid kwenye tender hiyo. Cha kushangaza wale walionunua mbolea kutoka kwake wanakwenda kuuza, yeye anauza ghali ana-bid bei ya juu, haiwezekani. Mimi nauza vitu nawagawia wenzangu wanakwenda ku-bid, mimi na-bid bei ya juu kuliko ninaowauzia mimi, haiwezekani lazima kunaujanja fulani sasa hii itakoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi sana, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kubuni mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la tozo, tozo imekuwa ndiyo sumu kubwa sana ya kuchukua mapato ya wakulima. Niongelee wakulima wa tumbaku, ambako ndiko natoka. Tozo imekuwa kubwa kiasi kwamba wakulima hawaoni faida yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku- declare interest, nimetembea nchi tano za Ulaya kutafuta wanunuzi wa tumbaku kwa gharama yangu. Nimekwenda Uturuki, Greece, nimekutana na Wakorea kutafuta wanunuzi wa tumbaku. Kwa gharama yangu! Nimeshindwa kupata mnunuzi hata mmoja! Sababu ni nini? Bei ya tumbaku ya Tanzania ni ghali sana kuliko bei zote duniani; na matokeo yake mimi nina bei ya wakulima waliouza Uturuki mwaka 2016. Ubelgiji imeuza Uturuki kilo 34,967,318, kilo milioni na kitu, wakati Tanzania imeuza Uturuki kilo 32,000. Mnaweza mkaona tofauti yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewauliza kwa nini hamnunui kutoka Tanzania? Sababu kubwa wanasema bei iko juu sana. Bei iko juu kwa sababu ya tozo hizi! Tozo ambazo nimeziona katika hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri, itatusaidia kupunguza bei ya tumbaku ya Tanzania nje. Kwa hiyo, wanunuzi hawa watauza tumbaku nyingi na hivyo watanunua tumbaku nyingi kwa wakulima. Naomba, imesahaulika tozo moja muhimu sana; tozo ya unyaufu, ambayo ndiyo peke yake inayowasaidia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale ambao hamjui maana ya unyaufu ni kwamba, wakulima wakiuza tumbaku leo, aliyenunua haji kuichukua. Akija kuichukua kutoka kwenye ghala anaipima tena, anakuta imepungua kilo 400, mia ngapi, wanamkata mkulima. Kwa nini wasinunue na kuichukua tumbaku yao ile? Wanasema kama tungeweza kuiuza kwenye center moja, basi gharama ya center watalipa wao. Gharama ya kuibeba watabeba wao wenyewe lakini suala la unyaufu halitakuwepo tena. Naomba Mheshimiwa Waziri afute tozo ya unyaufu na atusaidie kuanzisha masoko ya pamoja. Hii itasaidia moja kwa moja kupunguza gharama na kuongeza bei ya mkulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine ambalo linanisumbua sana, nalo ni ushirika. Vyama vya Ushirika Mheshimiwa Waziri anisaidie sana. Nimemwomba mara nyingi sana kwamba Sheria ya Ushirika ina kasoro nyingi sana; ilitungwa ile Sheria na Wanunuzi. Sheria inasema, bei ya tumbaku itapangwa na wanunuzi na wakulima. Wakulima darasa la saba, wanunuzi wana degree tatu. Kutakuwa na ukweli hapo? Matokeo yake wamekuwa wakulima wanaitwa kwenye mikutano mikubwa, wanapewa posho, halafu bei wanapanga wanunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja kusema hapa, alete sheria hii. Bunge linatengeneza sheria hapa, turekebishe kipengele kinachosema Serikali hairuhusiwi kabisa ku-discuss bei, bei itapangwa na wakulima na wanunuzi. Wanunuzi wana degree tatu, wakulima darasa la nne. Inawezekana kweli! Nyie Wanasheria humu ndani mnaona balance iko kweli pale! Wala haruhusiwi hata mtu mmoja nje ya mkulima na mnunuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Waziri Mkuu. Waziri Mkuu amesikia maneno mabaya na mambo mabaya, madudu ya Tabora kule kuhusu tumbaku. Waziri Mkuu amevunja Bodi ya Tumbaku jambo ambalo nimekuwa nikimwambia kila siku kwenye mikutano ya mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwambia Waziri wa Kilimo vunja Bodi ya Tumbaku, ilikuwa ngumu, lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu amevunja Bodi ya WETCU, Chama Kikuu cha Ushirika, ambacho wamekuwa wanaogelea kwenye mihela kama vile baharini. Zitakuja na mfumo mzuri wa ununuzi wa tumbaku pamoja na bulk procurement ya mbolea, kwa sababu hawa ndio wanaotangaza tenda ya kununua mbolea. Nafikiri atawashirikisha kwenye bodi mpya, wapate Bodi nzuri ambayo itawasaidia wakulima wangu kule Uyui. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, kuna kituo kinaitwa OXEN Training Center kituo cha ku-train Maksai pale Upuge kilifunguliwa na Mwalimu Nyerere. Mwalimu amefariki amekwenda mara mbili kuangalia kituo kile. Baada ya kufariki Mwalimu, kituo kimekufa. Hamna aibu! Land Mark ya Mwalimu mmeiua! Mile Stone ya Mwalimu mmeiua! Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aniambie future ya kituo cha kufundishia wanyama kazi pale Upuge.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote nawaachia wenzangu waongee. Naunga mkono hoja hii na kabisa kabisa namuunga mkono Mheshimiwa Rais. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.