Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na naomba nimshukuru Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama tena ili niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasahau, naomba nitangulie kuunga mkono hoja iliyowasilishwa na mkwe wangu, Mheshimiwa Dkt. Tizeba, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Kwa kweli nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa hotuba yake nzuri aliyoiwasilisha hapa Bungeni. Kama tutakuwa wakweli, tutaona kwa vitendo kile ambacho Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni alikiahidi Tanzania nzima wakati anazunguka; lile jambo la kuondoa tozo za kero na ushuru mbalimbali wa kero kwa wakulima. Jambo hili watu wengine walikuwa wanadhani ni ndoto, sasa limekuwa kweli kwa sababu leo Mheshimiwa Waziri ametuletea orodha ndefu sana ya tozo mbalimbali ambazo zimefutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukombe, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza jambo hili, kama kawaida yake, mambo mengi ambayo ameyaahidi yamekuwa yakitekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Bukombe wanashukuru sana kwamba Wizara hii kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tumejengewa soko kubwa sana la kisasa kwa ajili ya wakulima wa muhogo ambalo liko Namonge. Soko hili litasaidia sana wananchi wa Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita na nchi jirani, kwa sababu ni soko kubwa sana, linawasaidia hawa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, ile mbegu ya mihogo inayoitwa mkombozi, inazalishwa kwenye Wilaya ya Bukombe, multiplication yake inafanyika kwenye Wilaya ya Bukombe ambapo Kata nne na vikundi 52 vinafanya kazi hii. Kazi nzuri sana hii imefanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe. Tunawashukuru sana, kwa kweli hili jambo litatusaidia kwa sababu mihogo tuliyokuwa nayo mbegu yake ilikuwa imechoka, isingeweza kuwapatia tija wakulima wa Wilaya ya Bukombe na Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani nizungumze kidogo juu ya zao la pamba. Tanzania tuna potential ya kuzalisha pamba takriban tani milioni moja, lakini kwa sasa kwa taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri amewasilisha hapa, tunazalisha pamba kwa mwaka mzima tani 122,000 peke yake. Kwa hiyo, pamba kwa kweli ambalo lilikuwa ndilo zao muhimu sana kwa wananchi walilokuwa wanalitarajia sana kubadilisha maisha yao, limeanguka na kila mwaka ukiangalia graph ya trend inashuka kila wakati. Kwa mfano, msimu wa mwaka 2012/2013 tulipata pamba tani 350,000; mwaka 2013/2014 tukapata pamba 249,000; mwaka wa 2015/2016 tukapata tani 149,445; na mwaka huu 2017/2018 Mheshimiwa Waziri ametuonesha dhahiri pale tumepata tani 122,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tumefika hapo? Tumefika hapo kwa sababu tunaona kama zao hili limetelekezwa na wananchi wengi wamekata tamaa ya kulima pamba. Ukienda kwenye Mkoa wa Geita, kwa mfano, msimu wa mwaka 2015/2016 jumla ya ekari 119,701 zililimwa, lakini msimu uliopita pamba imeshuka. Wakulima wengi wamehama kulima pamba, wamelima ekari 73,546 peke yake. Wananchi wamekata tamaa kwa sababu yako maudhi madogo madogo ambayo naomba Mheshimiwa Waziri ayaangalie kwa haraka ili tuweze kuyatatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, mbegu ya pamba tuliyonayo (UK 91) ni mbegu ya zamani sana, ya miaka 24 iliyopita, bado iko kwenye circulation, matokeo yake mbegu hii haiwezi kuhimili magonjwa, haiwezi kuhimili mabadiliko ya tabianchi na mbegu hii haitupi tija. Sasa hivi Tanzania ekari moja tunazalisha pamba kiasi kidogo sana ukilinganisha na wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano; wastani wa kuzalisha pamba duniani kwa heka, ni tani 2.2. South Africa wanazalisha tani tisa; Burkina Faso wanazalisha tani 1.2; Syria tani 4.9; Egypt tani 2.9; na Tanzania 0.7 na Mheshimiwa Waziri anafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningekuwa naruhusiwa na Kanuni za Bunge, nikasema Wabunge wote ambao wamesoma kwa pamba wasimame hapa na wapige kelele, waseme ndiyo! Utapata kazi sana kuwanyamazisha. Kwa sababu wengi waliomo humu wameishi na wamesomeshwa kwa zao la pamba. Hata hivyo kwa sasa zao hili limekuwa yatima! Kuna kiongozi mmoja kule Wilaya ya Bukombe aliwahi kuwaambia wananchi kwenye mkutano wa hadhara, kwamba achaneni na pamba limeni viazi kwa sababu hakuna mtu anayehangaika nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atuhangaikie zao letu la pamba. Mauzo ya nchi kwa mujibu wa taarifa ya BOT yameshuka. Hata hayo yenyewe, utaweza kuona kwa taarifa ya mwezi wa Nne iliyopita, mauzo ya pamba tumeuza dola milioni 43 peke yake, wakati mwaka uliopita tu tuliuza 53.1. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na mkakati wa kuwasaidia wakulima juu ya upatikanaji wa pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kujiuliza, hivi kwa nini mkulima huyu asiingizwe kwenye value chain ya pamba? Tujenge ginnery hizo, mkulima aende akauze pamba yake pale; akiwa pale auze sufi, mbegu, achukue mashudu yake akafanyie kazi nyingine. Hivi inakuwaje mkulima anabeba pamba, humo ndani ya pamba anauza na byproduct nyingine zote zinakwenda nje ya nchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa pamba yote inayozalishwa Tanzania 70% inakwenda nje ya nchi. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tunapeleka ajira nje ya nchi, tunapeleka uchumi kwa watu wengine. Saa imefika Mheshimiwa Waziri tuje na mkakati, hizi ginnery, tupeleke pamba yetu kama mkulima anavyopeleka alizeti kule Singida. Mashudu yawe ya mkulima, mafuta yawe ya mkulima na mbegu iwe ya mkulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, mbegu hii tunayotumia ya UK 91, hapa leo atuambie tunaachana nayo lini? Tunahitaji mbegu ya UK M08 ambayo imethibitishwa kitaalam ambayo GOT yake ni 44%. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri hili na lenyewe tuliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo lingine limezungumzwa hapa kuhusu habari ya ushirika. Ushirika ndiyo ilikuwa dawa ya kumsaidia mkulima wa Tanzania. Ushirika umekufa kwa sababu ya wajanja wachache. Kipindi kilichopita Serikali ilipeleka fedha kwa ajili ya kufufua ushirika, ikapeleka management kwa ajili ya kuinua ushirika. Leo ushirika huu badala ya kuwasaidia wakulima na wao wamebadilika kuwa wanunuzi wa pamba kama ginneries wengine. Nyanza ananunua pamba kama ambavyo sijui shirika gani linanunua pamba; haiwezekani kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wana shida ya pembejeo. Ndiyo maana msimu uliopita wakulima walipatiwa mbegu ya pamba ambayo haikuota, wakulima wakapatiwa madawa ambayo hayakuua wadudu, lakini ikashangaza ginners bila aibu wakaenda siku ya kununua pamba wanahitaji kukata fedha kutoka kwa wakulima kwamba walichukua madawa na mbegu. Madawa gani ambayo hayakuua?

Mheshimiwa Naibu Spika, nani alikwamisha? Kwenye mlolongo mzima wa kuagiza pembejeo ni mrefu mno! Kuna producer huko juu, kuna agent hapa katikati, kuna mtu mwingine ni quality assurance ambaye ni TPRI. TPRI wakati ule tuko kwenye mgogoro wa madawa, tulihangaika naye sana. Bodi ya Pamba wanaonesha kwamba TPRI hajawahi kuleta majibu, kwa nini mbegu haioti? Kwa nini madawa hayakuua wadudu?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri awaonee huruma wananchi hawa, wananchi hawa walisomesha watoto wao kwa pamba na benki yao iliyokuwepo pekee kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na hasa Mkoa wa Geita na Wilaya ya Bukombe kila shilingi waliyokuwa wanaipata walikuwa wananunua mifugo. Mifugo kwa sasa na yenyewe ina changamoto yake. Sasa hivi kila mtu anayezunguamza anaiona kama jambo baya, jambo ambalo ni laana, mharibifu wa mazingira mkubwa. Wafugaji hawajasaidiwa, kwa namna gani waweze kufuga kisasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wanazungumza, punguzeni mifugo; hivi wanapunguza vipi mifugo wakati hata viwanda vya kuchakata nyama hatujavijenga? Namwomba sana Naibu Waziri atusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia ni kuhusu matrekta...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.