Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii. Nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujalia uzima. Nielekeze shukrani zangu kwa mtoa hoja Mheshimiwa Waziri Dkt. Charles Tizeba na Msaidizi wake ndugu yangu, Mheshimiwa William Olenasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ilibahatika kuwa na wataalam wenye kuijua Sekta yao. Nampongeza sana pia Katibu Mkuu upande wa Uvuvi, ndugu yangu Dkt. Yohana Budeba ambaye kiasili naye ni mvuvi kama mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa huzuni kidogo kwa sababu haya nitakayoyazungumza leo, kwa kiasi kikubwa sana ndiyo kilio cha wananchi wa Mafia. Kuna Taasisi ya Serikali inaitwa Hifadhi ya Bahari na naamini wapo hapa. Taasisi hii imekuwa ni kero kwa wananchi wa Mafia. Lazima nianze kusema mapema kabisa, hakuna mtu wa Mafia yoyote anayepinga uhifadhi, wote tunaunga mkono uhifadhi; lakini aina ya uhifadhi unaoendelea Mafia na hii Taasisi ya Hifadhi ya Bahari, maarufu kama HIBAMA siyo uhifadhi bali ni uporaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi kama jina lake lilivyo, wanatakiwa wahifadhi, lakini badala yake hifadhi ya bahari wamekuwa ni waporaji na wauzaji wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nimuulize ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, hawa amewatuma waje kuuza ardhi au waje kuhifadhi maeneo ya mazalia ya samaki? Tunataka aje na majibu mazuri kabisa, kwa sababu hivi sasa, hivi ninavyozungumza, hifadhi wameshauza visiwa viwili. Kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa, sasa hivi wako katika mchakato wa kuuza Kisiwa cha Mbarakumi na baadaye wanakwenda Nyororo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Hifadhi inasema wakati wanawaondoa hawa wavuvi katika hivi visiwa sheria inasema haya ni maeneo tengefu; na maeneo tengefu hayatakiwi kuwa na makaazi ya kudumu. Wanachofanya hifadhi, wanawaondoa wavuvi, vile visiwa wanaviuza kwa wawekezaji. Sasa inapingana na dhana nzima ya maeneo tengefu. Pale Shungimbili wameuza, imejengwa hoteli ya nyota tano; usiku mmoja dola 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie, toka imeuzwa kisiwa kile, Halmashauri ya Mafia haijapata hata senti tano, hatuujui mkataba uko wapi? Tuna sababu gani sisi tena ya kuipenda Hifadhi ya Bahari?

Mheshimiwa Naibu Spika, hoteli ile ya nyota tano iliyojengwa pale, wale wanaoitwa wawekezaji wamebadilisha mpaka jina. Mheshimiwa Simbachawene nimemwona hapa, labda watusaidie wenzetu waliopo Serikalini, mamlaka ya kubadilisha majina ya maeneo, ni mamlaka ya nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, inayoitwa Thanda Hoteli, wala si majungu unaweza uka-google ukaiona, Thanda –‘T’ for tangle, ‘h’ for hotel, ‘a’ for alpha, ‘n’ for November, ‘d’ for delta and ‘a’ for alpha. Thanda hoteli utaiona pale ukiisha- google tu, unaona Thanda Hoteli Mafia. Thanda Ireland Hoteli Mafia. Hakuna kitu kama hicho Mafia. Mafia kuna Kisiwa kinaitwa Shungimbili, hakuna kisiwa kinaitwa Thanda Ireland. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie mamlaka haya ya kubadilisha mpaka jina la kisiwa wameyapata wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, wamejenga pale hawana hata building permit. Building permit anatoa Mkurugenzi wangu wa Halmashauri, yeye mwenyewe anashangaa anasema mimi naona majengo yanaota tu pale kama uyoga. Sasa tunataka kujiuliza wakati wanavichukua visiwa hivi kuvifanya maeneo tengefu, hoja ilikuwa kwamba kuna kiumbe kinaitwa kasa. Kasa anakwenda kupanda pale kutaga mayai.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo mmeshawauzia hawa wawekezaji, wameweka miamvuli pale Wazungu wanapunga hewa muda wote; huyo kasa atapanda juu kwenda kutaga mayai saa ngapi katika mazingira kama hayo? Kuna mambo ya ajabu sana yanaendelea pale Mafia. Kuna aina ya uporaji unaoendelea pale. Sasa tunawauliza ninyi mmekuja kuhifadhi, mmekuja kuuza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema wala sitatoa shilingi, lakini nitakachofanya, tutamwandikia Mheshimiwa Rais tumwambie kwamba Mafia inauzwa. Visiwa viwili vilishauzwa, watauza cha tatu, watauza na kisiwa kikubwa, mtatuhamishia sehemu nyingine kwa sababu tumewaambia miaka miwili, hamtaki kusikia. Kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana. Hata wananchi kuulizwa basi juu ya ule uwekezaji! Sheria zinasema, hawa watu wa hifadhi wamekuwa na kiburi na ni wababe sana. Wao wanaamini hiyo inayoitwa Sheria ya Hifadhi ina supersede sheria zote za nchi; Local Government Act mpaka Katiba ya nchi haimo. Wanakwambia hii hifadhi imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge, kwa hiyo sheria nyingine zote hazifai, inayofaa ni Sheria ya Hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana yule bwana anakuja pale anajenga hoteli, hahitaji building permit, hawataki kuwashirikisha wananchi, wananchi hawakuulizwa na hakuna mihtasari. Leo hapa nina hii document; nilipowauliza mbona wananchi hamkuwauliza? Wanasema wananchi tumewauliza, wakaenda kukaa na watu wanane pale Kirongwe baadaye ndiyo wanasema wananchi tumewauliza sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana nimwulize ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, kaka yangu, tena rafiki yangu sana; mambo haya yangefanyika kule Buchosa, yeye angekubali? Yeye ana visiwa kule; vingeuzwa visiwa vya Buchosa angekubali? Kwa sababu kila siku namwambia kitu hiki hiki kimoja hataki kusikia, kwa nini? Tunataka aje na majibu thabiti kabisa, kwa nini hifadhi ya bahari wanaendelea kuuza visiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo unaoitwa uhifadhi. Nenda pale Kigamboni Dar es Salaam kule Kijiji Beach, South Beach kule maeneo yale kaa kuanzia asubuhi mpaka jioni, yanapigwa mabomu utafikiri nchi iko kwenye vita na Ikulu iko pale pale. Hawa watu wa hifadhi wanaacha kwenda kukamata wapiga mabomu pale, wanakwenda kuuza visiwa kule Mafia, hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wanahamisha wananchi wa Nyororo, wavuvi wa pale, wamekaa karibuni miaka 15 wanawaondoa wanataka kuweka hoteli nyingine ya Nyota tano. Kisa nini? Wanasema sasa haya ni maeneo ya tengefu. Tunasema maeneo tengefu kusiwe na makazi ya kudumu. Kwa nini mnawatoa wavuvi halafu mnajenga hoteli? Hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jibondo, kisiwa kingine hiki; ndugu yangu Kwandikwa anafahamu sana haya. Wananchi wa Jibondo hivi sasa wako siege hawawezi kwenda kufanya shughuli zozote, wamezuiwa na watu wa hifadhi wasivue. Sasa tunawauliza, mmekuja kuwasaidia wananchi kuwahifadhi au kuwamaliza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuona kwamba uvuvi umeshindikana, wakaamua kulima kilimo cha mwani baharini. Wakalima wakapata mwani mwingi sana, wakaweka katika ma-godown yao. Imekuja meli kupakia ule mwani na kupeleka sokoni. Hifadhi ya bahari wanasema ile meli inavunja matumbawe, inaharibu mazingira. Kwa hiyo, hairuhusiwi kuingia, ule mzigo umeozea ndani. Nataka tuwaulize tu ndugu zangu, hivi ninyi hamna huruma? Hawa watu wa hifadhi hamna huruma? Watu mzigo umejaa ndani, hawaruhusiwi kwenda kuuza...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja