Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hii hotuba muhimu. Kwa kweli kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru sana Serikali; naishukuru sana Wizara hii, naungana na wasemaji waliotangulia, ukiangalia hotuba hii kwa kweli imeanza kutupa suluhisho la matatizo katika kilimo. Mambo mengi ambayo yameonekana kwenye hotuba hii nawiwa kutoa shukrani sana kwa Mheshimiwa Waziri Tizeba na timu yake. Naona sasa kwamba iko dhamira ya kusaidia wakulima tuweze kuinua uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru pia wananchi wa Ushetu kwa kutoa mchango mkubwa sana katika kilimo. Kilimo chetu katika eneo letu ndiyo kinatupa pia mapato ya kutosha katika Halmashauri kupitia mazao ya biashara; pamba na tumbaku, tunaweza kuendesha vizuri na kutoa huduma vizuri katika Halmashauri yetu. Kwa hiyo, nawapongeza sana wananchi pia kwa uvumilivu. Tumekuwa na shida kubwa, katika msimu uliopita hatukupata kabisa pembejeo kwa mazao mengine, lakini pamoja na hayo naona tulikuwa tumeweka nguvu kubwa sana kuhakikisha kwamba tunaweza kuzalisha chakula na mazao mengine ya biashara vya kutosha. Kwa hiyo, nawapongeza sana wananchi wa Ushetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uti wa mgongo. Utaona katika hotuba hii, Mheshimiwa Waziri amerejea kutukumbusha kwamba kilimo kinachangia sehemu kubwa la pato la Taifa, kinaajiri watu wengi. Sisi tuseme kwa upande wa kwetu Ushetu, kilimo ndiyo hicho ambacho tunakitegemea kiweze kututoa katika huu umaskini. Kwa sababu mimi naweza kusema kwamba asilimia mia moja ya wananchi wa Ushetu tunajihusisha katika kilimo. Iwe ni Mbunge, nalima; Diwani, analima; awe ni mfanyabishara, analima. Kwa hiyo, watu wote wanajishughulisha na shughuli za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kabisa sisi ni wadau wakubwa na tunahitaji sana hii Serikali itusaidie ili tuweze kusonga mbele zaidi. Kwetu hata wanafunzi pia wana mashamba. Kwa wale wenzangu wanajua jilaba, kwamba tuna mashamba madogo madogo ya wanafunzi. Hata watoto wadogo wa shule wana part time ya kulima, wanakuwa na mashamba. Kwa maana hiyo, tunaona uko umuhimu sana kwamba tunawazoesha watoto kwa nia ya kuona kwamba wanathamini hiki kilimo kweli na ni uti wa mgongo wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo hapa nataka niyaseme tu kwa ufupi sana. Kwanza naiomba sana Serikali kupitia Wizara hii, iweke dhamira ya kweli kuweza kuhakikisha kwamba haya ambayo yapo kwenye hotuba yanatekelezwa ili yaweze kutusaidia. Kwa sababu utaona kabisa kwamba ni muhimu tuzalishe ili tuwe na chakula cha kutosha na kwa kweli tutakuwa tunaweza kuinua uchumi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri sana Serikali pia iangalie na kuchambua, kuna mambo ambayo tunayaona kwenye ripoti. Kwa sababu nilikuwa nikiangalia taarifa ya BOT ya Mwezi Machi, 2017, naona ile trend ya uzalishaji mazao, bei na mauzo ya nje imekuwa ikishuka. Sasa naishauri tu Serikali ifanyie kazi, ichambue vya kutosha ili baadaye tuweze kupata suluhisho la kuona kwa nini wakati wote uzalishaji, bei na mauzo yanaendelea kushuka?

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kutolea mfano katika zao la tumbaku ambalo sisi tunalizalisha kwa wingi. Nimeona mauzo ya tumbaku yamekuwa yakishuka sana. Kuanzia mwaka 2013 tuliweza kuwa na mauzo ya dola milioni
7.3 lakini mwaka uliofuatia (2015) tuliweza kufikia dola milioni 41.2; lakini utaona kabisa mwaka 2017 kuna dola 9.4, tulishuka sana. Sasa na mazao mengine ya kahawa, pamba, katani, korosho na karafuu, utaona kuanzia mwaka 2013 mpaka 2017 tumekuwa tukiendelea kushuka, lakini pia ule uzalishaji kwa ujumla utaona nao umeshuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma nikaona kwamba mwaka 2013 pia tulikuwa na tani chache ambazo tulikuwa tumezalisha, lakini mwaka 2015 kulikuwa na uzalishaji mkubwa wa zao hili la tumbaku lakini mwaka 2017 pia tumeshuka karibu nusu. Lazima tuseme kwa nini tunashuka hivyo? Kwa hiyo, nafikiri hizi data zinazopatikana ni vizuri Serikali ikazifanyia kazi ili tuweze kuinua uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kilimo ni muhimu kwa sababu nilikuwa naangalia uwiano tu wa mazao ambayo tuliuza nje, ukilinganisha na maeneo mengine ambayo tulikuwa tumejipatia kipato, tumesafirisha madini na bidhaa nyingine za plastiki na kadhalika. Sasa kwenye kilimo, mifugo na uvuvi tulikuwa tumepata kati ya asilimia 59 hadi 64 ndiyo mchango wake. Kwa hiyo, unaona kabisa kwenye eneo hili ni muhimu sana kulitazama ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kwetu tunapata mvua mapema kuanzia Septemba. Kwa hiyo, niisihi tu Serikali yangu kupitia Wizara hii kwamba suala la pembejeo liwekewe umuhimu wa hali ya juu kwamba ikifika mwezi wa Tisa tuweze kupata hizi pembejeo mapema kama mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeze sana Serikali kwa kuja na utaratibu huu wa kuagiza hii mbolea kwa pamoja kwa sababu ilikuwa ni tatizo kubwa sana. Hili zoezi la mbolea likisimamiwa vizuri kwa kuzingatia kwamba wananchi katika baadhi ya Kata zetu zimekuwa ni model, tunazalisha kuanzia gunia 25 hadi 30 kwa ekari endapo tunalima kwa wakati na kutumia pembejeo kwa usahihi. Ziko Kata ambazo zimeonesha mfano, kama Kata ya Kinamapula, Kata ya Ubagwe, Kata ya Ulewe, zimeweza kuzalisha hadi magunia 30 kwa ekari.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa mwaka uliopita 2016 hatukupata pembejeo hizi kabisa kwamba wananchi wamekuwa na manung’uniko kwa kukosa mbolea. Kwa hiyo, naiomba tu Serikali kwa kipindi hiki kinachokuja na kwa vile tumeendelea kuwaahidi wananchi kupitia vikao vyetu kwamba Serikali inajipanga katika utaratibu mzuri, ambao ndiyo huu sasa Wizara imekuja nao, kuhakikisha wananchi wapate hii mbolea ya kutosha lakini waipate kwa wakati ili sasa twende tukazalishe; na tuweze kuhakikisha kwamba hili suala la njaa linaondoka kabisa na uchumi unakwenda juu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine Mheshimiwa Waziri atusaidie; kwa vile tunazalisha chakula cha kutosha na kumekuwa na shida sana ya soko la mazao ya chakula hapo mwanzoni tunapoanza kuvuna, kama inawezekana kupitia Halmashauri zetu Mheshimwia Waziri asaidie tupate maghala ya Halmashauri ili tuweze kuhifadhi chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo wananchi wanahitaji tena kupata fedha kwa haraka kwa ajili ya maandilizi ya kilimo, waweze kuuza na kupata fedha. Wakati huo tutakuwa tunahifadhi chakula kwa ajili ya matumizi ya Taifa kwa ujumla na wananchi wanapata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tuliangalie hili, kwa sababu kama chakula kinazalishwa kwa wingi na wananchi wanategemea kuweza kupata fedha kutokana na ziada kwa ajili ya kushughulikia mambo yao mbalimbali pamoja na maandalizi ya kilimo kwa msimu unaofuata, tunavyofanya zuio la wananchi kufanya mauzo ya chakula hiki cha ziada, kwa kweli inatuharibia ile trend nzuri ya kwenda kuzalisha kwa wingi msimu mpya. Naomba hii tuitazame. Kwani wengine wanaendesha kilimo kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee na suala la mbegu. Tumeona mkazo mkubwa umekuwa kwenye mbegu chache, zaidi kwa mbegu za mahindi. Kwa mfano, tunaweza kupata mbegu za mahindi kwenye maduka, lakini tumeacha kwenye maeneo mengine kama mbegu za pamba kupata zenye ubora, kupata mbegu za mpunga na zenyewe hatuzipati. Kwa hiyo, nafikiria Serikali iangalie pia zoezi hili la mbegu za kila aina.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia matumizi ya maabara. sisi kwetu Ushetu tumekuwa na maabara ndogo ambazo Serikali imetusaidia, nashukuru sana. Katika Kata ya Mpunze tunacho kituo kwa ajili ya kufanya majaribio ya hizi mbegu, lakini hakijatumika sawasawa. Naomba Serikali iweze kuweka msisitizo ili kama mbegu mara zinapopatikana, basi maabara hizi zianze zenyewe kuotesha ili tuone kama germination rate iko nzuri ili wananchi wanavyonunua hizi mbegu tuwe na uhakika kwamba mbegu hizi hazijachezewa, tumepata mbegu zenye ubora na tuweze kusonga mbele bila wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, kama tumekuwa na maabara hizi zitumike, lakini zitupe majibu; nasi tutadakia kwa ajili ya kuelimisha wananchi wetu umuhimu wa kutumia hizi mbegu ambazo ziko bora inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nishauri ni kwa kumalizia tu ni kuhusu matumizi ya hizi nyenzo; trekta na power tiller, lakini utaona kwamba mashine hizi zinapatikana mjini tu. Wizara ijipange, ione namna ambavyo itatuwekea vituo angalau kidogo tuwe na sample ya hizi mashine au vitendea kazi. Wananchi wayaone waweze kuhamasika kuweza kutumia haya matrekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu kwa sehemu kubwa tunalima sana kwa kutumia maksai. Kwa maana hiyo wananchi wako na utayari sasa wa kurahisisha kilimo chao na sisi baada tu ya mvua kunyesha wiki moja ile ya kwanza tunaweza kukamilisha mashamba yetu. Wananchi wana speed kubwa, hawataki kupoteza wakati pale mvua za mwanzo zinavyoanza kunyesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasi maeneo yetu Mheshimiwa Waziri atazame ili haya matrekta ambayo yako kwenye mpango wa kuzalisha yatakapokuwa tayari, basi yasogee katika maeneo yetu ya uzalishaji ili pia wananchi waweze kupata hamasa. Tunao uwezo wa kununua matrekta ili tuweze kuzalisha kwa wingi zaidi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi hii.