Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi na leo nisimame mbele ya Bunge lako kuchangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kutambua hatua iliyoanza au aliyoifanya Waziri wa Kilimo; kwa sababu nilivyokuwa najaza hii nafasi kwa maana ya kuja kuchangia Wizara ya Kilimo na Mifugo, nilidhamiria kuwa mtu mwenye hasira sana, lakini kuna jambo ambalo nimeliona humu, kitendo cha kujaribu kufuta ushuru mdogo mdogo kwa maana ya ushuru wa mazao pamoja na mifugo, nimetambua hatua hiyo. Naomba niseme kwa nini nilidhamiria kuwa na hasira? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wangu wa Simiyu kulikuwa na changamoto moja kubwa sana ambayo ilikuwa inafanyika kwa wafugaji kila wanapokwenda kuuza ngombe kwenye minada kulikuwa na utaratibu anaingiza ngombe kwenye mnada bure. Wakati wa kutoa ngombe anatozwa ushuru wa Sh.1,000/= kila kichwa cha ngombe, awe ameuza au hajauza ushuru lazima atoe. Jambo hili lilipelekea kuleta matatizo makubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu. Kwa kutambua hili kwamba wamefuta ushuru huu, ndiyo maana nikajikuta hasira yangu kidogo imepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ushauri, pamoja na kutoa kodi hizi, naomba basi Mheshimiwa Waziri apeleke waraka haraka sana kwenye Halmashauri zetu, ili jambo hili lianze kutekelezwa kwa haraka na wananchi waweze kunufaika na mifugo yao ambayo wanaitunza kwa muda mrefu, wanatumia gharama kubwa ili waweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu yalikuwa kwamba sisi Wasukuma ng’ombe ni ATM yetu. Ukipatwa na janga la njaa kwenye familia, unachagua ngombe wawili, watatu unapeleka mnadani, unauza unanunua chakula. Sasa walivyokuwa wanaambiwa wauze, wasiuze, lazima walipe ushuru, nilikuwa napata masikitiko makubwa sana, kwa sababu huyu mtu ana njaa halafu unamwambia atoe ushuru wakati ng’ombe hajauzika, ilikuwa ni jambo la aibu sana katika mkoa wetu. Kwa hiyo nashukuru katika hilo kwamba limeonekana na naomba nisisitize waraka upelekwe haraka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilisimama hapa nikichangia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; nilijaribu kugusia suala la pamba, lakini leo nataka nimtafute mchawi wa pamba. Zao la pamba tunamtafuta ni nani aliyesababisha zao hili lipotee? Kumekuwa na historia ya wakulima wa pamba, zamani tumekuwa tukipewa mbegu ambayo ilikuwa na manyoya kidogo, ile mbegu walikuwa wananunua wazazi wetu, tunalima tunazalisha. Mbegu ile ikibaki, ninachokikumbuka tulikuwa tunakwenda tunatengeneza magodoro, tunaendelea kulalia mbegu ambayo ilikuwa inabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kushangaza sasa hivi, nataka kujua, ni nani aliyeshauri mbegu hii ya pamba ipelekwe saluni, halafu iletwe sisi tuanze kupanda? Nataka kujua, maana tumeletewa mbegu ambayo ni ya kisasa na mbegu hii haioti na ikiota inaota mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mwananchi ametumia gharama kubwa kuandaa shamba la pamba matokeo yake anavuna kidogo. Heka moja inatoa kilo 30, anakwenda kuuza kilo ya pamba Sh.1,000/=, halafu tunasema kwamba leo tunamtafuta mchawi ni nani? Mchawi wa pamba ni Serikali yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiambiwa pamba ya Tanzania ni chafu…
T A A R I F A . . .
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na kumheshimu dada yangu, ingekuwa sheria inaruhusu ningemjibu kwa kinyumbani, lakini taarifa yake siipokei, kwa sababu amekubali kwamba tatizo ni kwamba wananchi hawakuelewa matumizi ya ile pamba. Ilikuwa ni jukumu la nani kuwaelimisha hao wananchi kama siyo Serikali? Kama Serikali haikuwajibika kuwaelimisha namna ya matumizi ya hii mbegu, maana yake bado mchawi ni Serikali yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka kwenye suala la mbegu hii kumekuwa na changamoto ya kuchelewesha mbolea. Tunategemea sana kilimo cha msimu. Mvua zetu ni za msimu; kuna mvua za kulimia, kuna mvua za kuoteshea, kuna mvua za mwisho. Sasa wananchi wamekuwa wakiletewa mbolea kwenye mvua ya kuvunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tatizo ni kuleta mbolea, naomba Mkoa wa Simiyu, jana nilizungumza kwamba sisi tunazalisha mbolea. Kama tunazalisha mbolea, naomba basi wananchi wapewe elimu waweze kuitumia mbolea ambayo wao wanaizalisha kule, ambayo ni mbolea ya ngombe, kuliko kusubiri mbolea ambayo haijulikani itakuja wakati gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba wananchi wale wakifundishwa matumizi ya mbolea wanayoizalisha, hakuna ngombe atakayedondosha kinyesi chochote, watatamani hata kuwafungia maliboro kwenye nanii ili kuhakikisha ile mbolea haipotei. Ni kwa sababu hawajui matumizi yake, ndiyo maana ile mbolea inapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze kuhusu suala la mifugo. Tumekuwa na changamoto sana kuhusiana na suala la malisho. Mwaka 2016 niliuliza swali hapa, kuhusu kutenga maeneo ya kuchungia. Nikadai eneo la Maswa Reserve kwamba limekosa sifa, kwa nini lisirudishwe kwa wananchi ili waweze kuchungia ngombe zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na changamoto kwenye maeneo ambayo yako karibu na hifadhi…
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naomba niunge mkono hoja ya Upinzani. Ahsante sana.