Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wachangiaji waliopita kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, nipongeze pia timu yake kwa pamoja kwa kazi nzuri ambayo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wakati anaomba kura alizungumzia sana hasa katika suala zima la kuondoa tozo katika mazao mbalimbali na hili ameshaanza nalo, Mheshimiwa mchangiaji aliyepita anasema tozo, jamani ni hatua kwa hatua. Ameanza na tozo sasa baadaye itakwenda kwenye kutafuta masoko, ni hatua kwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitasema sana kuhusu pamba kwa sababu wewe Mtemi ni shahidi, tumezungumzia sana kuhusu zao la pamba, bei na mambo mengine. Najua Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni sikivu, sasa yale ambayo tutakuwa tunayasema humu ni vizuri Serikali ikayachukua na kuyafanyia kazi. Si jambo jema sana Waheshimiwa Wabunge wanasema jambo hilo hilo lakini tukumbuke zao la pamba kwa Kanda ya Ziwa ndiyo baba na ndiyo mama, ndiyo kila kitu. Uchumi wa Kanda ya Ziwa unategemea zao la pamba, bila pamba kwa kweli katika Kanda ya Ziwa sijui kama wengine tungekuwemo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa sababu hata tukiulizana humu ndani ikifika pahali tunabeza pamba, sijaona humu Mbunge aliyevaa nguo ya ngozi ya ng’ombe au ya punda; wote tumevaa nguo zinazotokana na zao la pamba. Sasa kama mahitaji ya pamba ni makubwa, leo hatutaki kuzingatia na kuona kwamba zao hili ni zao la biashara na linasaidia nchi hii, kwa kweli tutakuwa hatujitendei haki. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali ilione hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuhusu kilimo cha kutumia matrekta. Mwaka jana kama unakumbuka wakati Waziri anawasilisha taarifa yake hapa alisema kwamba kuanzia sasa na kuendelea tunataka tuanze kununua matrekta ya kutosha ili kusudi jembe la mkono tukutane nalo makumbusho au sehemu nyingine. Sasa nimejaribu kuangalia kupitia Mfuko wa Pembejeo, wali-project kununua matrekta 79 lakini yaliyonunuliwa ni matrekta 43, matrekta ya mikono power tiller 10, hakuna hata moja lililonunuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu wa fedha wamekisia kununua matrekta mapya 71. Sasa sioni kwamba hivi kweli nia ni kununua matrekta nchi hii ipate matrekta ya kutosha. Hata hivyo, tukitaka kulima kisasa, kilimo kipana, mashamba makubwa ni lazima tutumie matrekta; hatuwezi tukaendelea kutumia jembe la mkono halafu ukawa na kilimo kikubwa. Lazima matrekta yatumike, kama hukumwezesha yule mtu mdogo kule chini kumkopesha kupitia huu Mfuko wa Pembejeo matrekta yatakuwa labda ni ya mjini tu lakini wakulima wakubwa wapo vijijini na bila kuwakopesha wakulima kule vijijini hawawezi kulima kwa kujitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Tizeba yeye ni mtoto wa mkulima pamoja na kwamba ametoka kwenye wafugaji, yeye ni mtoto wa mkulima anaifahamu Mwanza, hebu atusaidie hasa upande wa matrekta ili kusudi matrekta yaende yakafanye kazi yake kule yalime kwa kilimo siyo cha kujikimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye mazao kujitosheleza hasa kwa chakula. Inashangaza kuona kwamba eti nchi hii, nitoe tu mfano Mkoa wa Morogoro tulikubaliana hapo mwanzo kwamba kuwe na ghala la chakula la Taifa, lakini sioni jitihada zozote zile kuonesha kwamba ni kweli pale ni ghala la chakula. Tulisafiri juzi kwenda Mlimba, mito tuliyokutana nayo, nikauliza hivi Mkoa wa Morogoro una jumla ya mito mingapi? Nikaambiwa Mkoa wa Morogoro una jumla ya mito zaidi ya 1000 na inafaa kwa umwagiliaji. Sasa unajiuliza hivi tatizo letu ni akili zetu au kutokutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mkoa huu una mito zaidi ya 1000 na inatiririsha maji mwaka mzima, hivi kilimo cha kumwagilia kinatushinda nini? Una mito zaidi ya 1000 huwezi kumwagilia, maji unayaacha tu yanatiririka yanakwenda baharini; kwa nini maji yale tusiyatumie kwa ajili ya umwagiliaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hivi inawezekana kweli Tanzania tukawa tuna njaa? Hivi mwanzo wakati wa Baba wa Taifa, kuna mikoa minne ilichaguliwa, the big four ikawa inazalisha chakula cha kutosha kwa makusudi. Tukawa na siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona lakini hiki kilimo cha kufa na kupona sasa hivi sijui kimefia wapi, siasa ni kilimo nayo imefariki dunia, hakuna. Sasa hii mikoa mitano au minne, leo tukisema kwamba hebu tuiwezeshe hii mikoa iliyokuwa inazalisha kwa wingi chakula, chakula hicho kiweze kusaidia maeneo mengine yenye ukame lakini mikoa hiyo na yenyewe tumeiacha, hatupeleki mbolea na tukipeleka mbolea ni ya shida.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwa hii mikoa mitano au minne hebu turudi nyuma tuagalie ni wapi tumekosea na wapi sasa tufanye nini. Nashauri, siyo jambo jema sana kukaa tunalia hapa kwamba chakula hakuna, lakini lazima tulie kwa sababu inawezekana wenzetu wataalam mnataka kutusaidia lakini hamtaki kutusaidia. Ukitazama ile timu ya Mheshimiwa Waziri ina Maprofesa na Madaktari waliosomea mambo ya umwagiliaji lakini umwagiliaji sasa unaonekana na wenyewe hauna tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye suala la pembejeo kwa mfano upande wa zao la pamba inasikitisha tu, imesemwa jana hapa. Pembejeo zinaenda kwa wakati ambao haufanani na majira yanafahamika kwamba majira ya kulima pamba ni mwezi fulani, kupeleka dawa ya kupulizia wadudu ni mwezi fulani na kupeleka mbegu ni mwezi fulani lakini inapelekwa tofauti. Kwa utaratibu huu mazao yetu yanakwenda kufa. Tulikuwa tunaongoza kwa mazao mengi tu si katani, pamba, korosho wala kahawa lakini leo mazao yote haya yameshuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji ukitazama kwenye majedwali huku unashuka, mfano zao la pamba mwaka jana ilikuwa tani 122; mmekisia tani laki moja na nusu, hamuwezi kufika pamba haipo msijidanganye. Hii tani laki moja na nusu hamuwezi kupata hata siku moja, mmetoka kwenye tani 122 mnataka kwenye 150 mtaipata wapi? Pia hawa wakulima wa pamba mnawasaidia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri na kumwomba sana Mheshimiwa Tizeba najua changamoto ziko nyingi kwenye Wizara yake, lakini hebu wakae na wataalam hasa kwenye suala la chakula kwa sababu hata Mheshimiwa Rais amesema jamani tunalia njaa, tunasema hatuna chakula, Masanja yeye analima anavuna, Athumani kwa sababu ni mvivu halimi, anakaa anasema kwamba tunaomba chakula cha njaa, lakini kama tuki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Naunga mkono hoja.