Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuwawakilisha wananchi wangu wa Shinyanga katika bajeti hii ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyeki, napenda kuongea na Mheshimiwa Waziri na kumwomba atusaidie matatizo ya ushirika pale Kahama. Mheshimiwa Waziri wote tunafahamu Sheria ya Ushirika namba 20 ya mwaka 2003 inasema wazi kwamba Ushirika ukifilisika mali zake zitakwenda katika Ushirika mwingine. Hilo limekuwa likifanyika tangu mwaka 1984, mwaka 1986, lakini cha kushangaza hivi karibuni pale Kahama Chama cha Ushirika kimepewa Kampuni. Wamepewa Kampuni kinyume na utaratibu na Mahakama imetengua lakini mpaka leo Chama kile cha Ushirika
kimeng’ang’aniwa na Kampuni na wale wananchi ambao walijiunga pamoja, ambao ni wakulima wadogo wadogo wakatengeneza Ushirika, wakajenga vibanda, wamenyang’anywa maeneo yao. Suala hili nimeshalipigia kelele mara nyingi humu Bungeni na hakuna msaada wowote unaoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alitazame jambo hili kwa jicho la pekee. Wale wakulima ni watu ambao ni wanyonge, hawana pesa, hawawajui watu wakubwa, lakini kwa sababu walioko pale ni mapapa, ni mafisadi, wamewanyang’anya maeneo yao wale watu, vibanda zaidi ya 200 vimechukuliwa, soko lile limemilikishwa kwa mtu mmoja ambaye ndiye mwenye hisa nyingi kwenye Kampuni ile na wale watu wanakosa pa kukimbilia. Namfahamu vizuri Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Tizeba ni mtetezi wa wanyonge. Namwomba sana aje kwetu pale atusaidie kutatua tatizo hili kwa sababu limekuwa ni tatizo sugu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wale watu wakihoji kuhusu Ushirika Mheshimiwa Waziri wanakamatwa, wanaenda kuwekwa ndani, wanaanza kuhojiwa, wanatishwa, vitisho hivyo ni unyanyasaji kwa raia wanyonge wa Tanzania hii. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kutatua tatizo la ushirika kwa sababu limezidi, kwanza ni kinyume cha Sheria, Mahakama imeshatengua Kampuni ile kumiliki, ile hati iliyopo pale ya Kampuni imetenguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza wanatakatisha hati ile, wanafanya kui-renew ili ionekane kwamba ni hati halali. Kweli tatizo hili limezidi, limekuwa la muda mrefu lina miaka zaidi ya 27, tunaomba Mheshimiwa Waziri tafadhali aje atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo niongelee suala la upigaji chapa ng’ombe, tumezinduliwa mradi sasa hivi wa kupiga chapa ng’ombe. Wanasema ni kwa ajili ya sababu za kiusalama wanataka kutambua ng’ombe na wale wanaokuja kutoka nchi za jirani. Hata hivyo, wanasema upigaji chapa hawa ng’ombe gharama yake ni Sh.3,000/= kwa kila ng’ombe. Sisi Wasukuma tunasifika kwa ufugaji. Familia za vijijini Sh.3000/=, Sh.1,000/= ya kula tunahangaika kutafuta hiyo Sh.3,000/= tutaitoa wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndizo tozo za kero ambazo zilipigwa marufuku na Mheshimiwa Magufuli. Kama wanaleta mradi basi watafute namna ya kuutekeleza mradi ule bila kuwaumiza wananchi na Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa kwamba kupiga chapa ng’ombe kunashusha thamani ya ngozi ile inapotakiwa kuuzwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunasema tunakwenda kwenye Tanzania ya Viwanda, tunasema tuwakwamue wananchi kwenye umaskini, leo tunaenda kuwapiga chapa ng’ombe wao na tunawatoza Sh.3,000/=. Tunaomba majibu tunahitaji kujua ni njia gani itatumika kuwapiga chapa bila kuwabughudhi, bila kuwakera wakulima hawa ambao ufugaji kwao ni biashara, ufugaji ni maisha, lakini ufugaji kwao ndiyo chakula cha kila siku na ndio utamaduni wetu vile vile. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie sana majibu juu ya hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pia suala la punda. Usukumani punda wanatumika kwa ajili ya kubeba mizigo, maji, ndio usafiri kule kwetu. Hata hivyo, hivi leo nikikueleza punda wanauawa, punda wanauzwa, wamekuwa ndio biashara. Mheshimiwa Waziri, China wanabiashara ya ngozi, wananunua ngozi hizi za punda na wanatengeneza anti aging, dawa ambayo inayozuia kuzeeka na inaongeza nguvu za kiume pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri, biashara hii…

MWENYEKITI: Mheshimiwa umesemaje? (Kicheko)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la punda lina dawa ambayo inatumika kule China kupunguza kuzeeka, lakini pia inaongeza nguvu za kiume. Kwa sababu hiyo thamani ya punda ni Sh.50,000/= mpaka Sh.190,000/=, lakini thamani ya ngozi ya punda ni pound 160, ngozi peke yake. Juzi Mheshimiwa Mwijage wakati anapitisha bajeti yake hapa alisema amepiga marufuku uuzaji wa punda. Hii haitoshi, tunatakiwa tuisimamie kama tunavyopiga marufuku mambo ya pembe za ndovu na biashara nyingine, kwa sababu hii itapelekea kupotea kwa hawa punda ambao ni mifugo tunayoitegemea sisi kama njia ya usafirishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tumeamua kuingia kwenye biashara hiyo basi tuwe na mechanism ya kuongeza hawa punda wawepo wawe ni wanyama wa biashara, waongezeke tuwe na jinsi ya kuboresha, kwa sababu hii mifugo iko chini ya Wizara yako na hii mifugo sisi tunaitumia kama njia ya usafirishaji kule kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ethiopia wana mifugo milioni 7.5 hii ya aina ya punda, lakini kuna nchi ambazo zimepiga marufuku na wameweka sheria, nchi kama Burkina Faso, Niger na Pakistan wameshaweka Sheria. Kusema tu haitoshi, tunafungua mianya ya wale watu ambao watakuwa wanafanya ujangili wa mifugo hii. Tusifungue mianya kwa sababu hatimaye itatuathiri sisi wenyewe. Tuweke sheria ambazo zitazuia, lakini kama unataka kufanya biashara hiyo na wafanye kwa njia halali na kuwe na misingi ya kuzuia upotevu wa wanyama hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu kwa kweli Ushetu, Tarafa ya Mweli hakuna hata josho, tarafa nzima ina kata karibu sijui ngapi, hakuna hata josho la kuoshea ng’ombe. Sasa bajeti ya Kilimo na Mifugo haifiki hata trilioni moja na tunategemea eti huu uti wa mgongo wa Kilimo Kwanza; sijui hata hiyo sera iliishia wapi; tunategemea eti malighafi itokane na mazao wa kilimo na mifugo, eti uti wa mgongo wa nchi hii ni kilimo, wakati huo huo hata bajeti yenyewe haiakisi malengo ya nchi hii ya Tanzania ya kutokana na malighafi za kilimo na mifugo. Hivi kwa nini tuendelee kuwadanganya Watanzania? Mimi sina wasiwasi na ukusanyaji wa kodi katika nchi hii, wasiwasi wangu ni allocation ya bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atueleze mkakati wake wa kuongeza kilimo na mifugo kwa nchi hii kuelekea ku-connect na wazo la Tanzania ya viwanda ukoje? Ukiangalia ni theory tu, utekelezaji wa theory hii mimi siuoni, naona tu ni maneno yanasemwa na mwakani wanatumia kitabu kile kile wanabadilisha mwaka wanabadilisha vitu vidogo wanarudisha kitu kile kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, anaakisi vipi, anashirikiana vipi na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutengeneza barabara ili atusaidie kule Ushetu, Kinamapula, Nyandele sijui Wandele sijui wapi, anatusaidia vipi kuleta barabara tuweze kulima kilimo cha tumbaku? Pamba imeshakufa, zao la biashara tulilonalo Shinyanga sasa hivi ambalo tunalitegemea ni tumbaku, lakini hakuna miundombinu iliyoboreshwa kila siku ni hadithi mtatekeleza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.