Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kunipa nafasi ili niweze kuchangia mada hii ambayo iko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwanza kuipongeza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kuhakikisha kwamba sekta hii ambaYo ni sekta muhimu inapiga hatua na kuweza ku- support sekta zingine ambazo zinategemea kilimo kama Sekta ya Viwanda, Mazingira na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia vitabu hivi viwili, kitabu cha Hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na kitabu cha Kamati ya Kudumu ya Bunge, ya Kilimo, Mifugo na Maji, nimefarijika kutokana na malengo ambayo yapo katika bajeti hii. Pia nimefarijika zaidi baada ya kuona kwamba utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais, zinaendelea kudhihirika kwa vitendo hususani pale ambapo wameendelea kuondoa zile kodi za kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Kagera Wilaya ya Ngara, sisi ni wakulima wa zao la kahawa, kwa muda mrefu sana zao la kahawa limekuwa na bei chini kutokana na tozo nyingi. Zilikuwepo kodi 26 sasa zimeondolewa kodi 17; naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais na Wizara ya Kilimo kwa kazi hii nzuri. Vile vile nipongeze hata kwa kodi ambazo zimepunguzwa kwenye Sekta ya Mifugo, kodi saba zilizoondolewa zitafanya maboresho katika sekta hii ya mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mipango mizuri ambayo imeainishwa katika kitabu hiki cha bajeti katika kuboresha sekta hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini kutokana na bajeti hii kuwa ndogo napata mashaka kidogo katika utekelezaji wa baadhi ya malengo ambayo yamewekwa katika mpango huu wa utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kunapokuwepo na ufinyu wa bajeti na inapotokea kwamba sasa hata pesa hazipelekwi kwenye miradi ya maendeleo inavyotakiwa, athari ni kubwa na zinaonekana katika maeneo mengi. Kwa mfano tumeshuhudia kwamba upo upungufu kwa mfano wa watumishi hususan Wagani katika maeneo mbalimbali, tumeshuhudia upungufu wa bajeti katika vituo vya utafiti, tumeshuhudia kuwepo na upungufu wa fedha hususan katika kuboresha miundombinu katika sekta ya mifugo kwa mfano ujenzi wa malambo, ujenzi wa majosho na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwamba katika utekelezaji sasa wa bajeti hii, pamoja na kwamba kuna ufinyu huu, kuna upungufu huu, nina uhakika kama tutaweza kusimamia vizuri na tukaenda kulingana na jinsi ambavyo tumeweka vipaumbele, tunaweza tukapiga hatua, sina mashaka kwa sababu dalili naziona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari ambazo nimezisema, kwa mfano kwenye vituo vya utafiti kuna mahali ambapo mpaka sasa hivi kwenye vituo vya utafiti kama kituo cha Naliendele, baadhi ya watumishi ambao wamestaafu hawajaweza kupata stahiki zao hususani kama pesa kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao, lakini bado pia, watumishi wanapostaafu replacement ya watumishi wengine inakuwa ni tatizo kutokana na ufinyu wa bajeti. Kwa hiyo niwaombe katika maeneo haya ambayo ni muhimu Serikali iweze kuyaangalia na kujikita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua jitihada za Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Naibu Waziri, na watendaji wao. Binafsi upande wangu katika Jimbo langu la Ngara, wamekuwa wakinipa ushirikiano mkubwa na ndiyo maana nasema kwamba, ili tuweze kuinua sekta hii ya kilimo pamoja na kuzalisha mazao ya chakula lakini ni lazima pia tuangalie uzalishaji wa mazao ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu kubwa tunaangalia mazao ya chakula kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na chakula cha kutosha, lakini tunapokuja katika suala la kuinua kipato cha mwananchi na kuinua uchumi wa nchi hii kupitia sekta ya kilimo, lazima tuangalie uboreshaji katika mazao ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mazao ambayo tumeyazoea korosho, kahawa, pareto, pamba na kadhalika; lakini yapo mazao mengine ambayo hatujayazoea Tanzania lakini ni mazao ambayo yamefanya vizuri katika nchi zingine na ambayo yameweza kuinua uchumi mkubwa katika Mataifa hayo. Ndiyo maana katika jitihada zangu binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Ngara za kuangalia fursa zilizopo, na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, tumeamua kuanzisha zao jipya la Stevia, ambalo ni zao linalofanya vizuri duniani sasa. Naishukuru Wizara kwa ushirikiano wanaonipa kwamba tayari sasa tunaingia kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii kama nilivyoomba wakati ule kwenye swali langu la nyongeza, kwamba kituo cha Maruku ambacho kitafanya utafiti kwa kushirikiana na Kampuni ya East Africa Stevia and agro investment kwenye zao hili la Stevia basi bajeti iweze kutengwa kwa ajili ya kituo hiki cha Maluku na utafiti huu uweze kufanyika katka Jimbo la Ngara. Ni pesa kidogo tu ambazo haziwezi kuzidi milioni 20 kwa kuanzia kwa ajili ya utafiti huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Mifugo. Sekta hii ni sekta muhimu, lakini ni sekta ambayo imekumbana na changamoto nyingi. Katika Wilaya yangu ya Ngara tuna mifugo mingi, tuna ng’ombe takribani 70,000, mbuzi wasiopungua 190,640, nguruwe takribani 20,000 na kondoo zaidi ya 75,000 lakini hatuna lambo hata moja, yaani bwawa la kunyweshea mifugo. Kwa hiyo hii inakuwa ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo ambayo ilikuwa inachungiwa kwenye hifadhi za Burigi na Kimisi sasa mifugo hiyo inaingia vijijini ambako hakuna huduma hizi za mabwawa na malambo, kwa maana hiyo vyanzo vya maji ambavyo ndivyo vinavyotumiwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya kawaida vinazidi kuharibiwa kutokana na mifugo hii, ambayo ni mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ya bajeti yake aweze kuangalia ni namna gani ambavyo wanaweza wakatenga kiasi fedha kwa ajili angalau ya kuweza kuchimba hata malambo manne basi kwa sababu tuna tarafa nne basi kwa kuanza angalau Malambo manne ili kila tarafa iweze kupata lambo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ngara naweza nikasema ni lango la kuingilia na kutoka kwenye Nchi za Maziwa Makuu, lakini pia ni Jimbo ambalo lina fursa nyingi. Kama nilivyotangulia kusema na ambavyo nimesema wakati nachangia kwenye Wizara ya Maji, niipongeze Wizara kwamba baada ya mchango wangu wameangalia kwa makini na tayari bonde la Murongo limetengewa fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu, ambalo liko katika Kata ya Bukililo. Pia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.