Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na hatimaye kusimama katika ukumbi wako wa Bunge kuweza kuchangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakumbuka mwaka 2015 wakati wa uchaguzi alisema kodi kero zimezidi na hatimaye leo ndani ya mwaka mmoja na nusu tunakwenda kuona kodi kero zimenakwenda kuondolewa. Mheshimiwa Rais hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Naibu wake pamoja na timu yake yote. Niwaombe basi haya waliyoyaandika kwenye vitabu hivi waende wakayafanyie kazi. Tunawaamini, tunaamini watatekeleza yale ambayo wametuletea leo ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo bila afya hakiwezi kwenda na natambua kabisa mchango mkubwa wa wanawake katika sekta ya kilimo. Naomba uniruhusu nitumie fursa hii kuwashukuru sana Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kuweza kunisaidia kwa wanawake wa Mkoa wa Shinyanga, msaada wa vifaa vya kujifungulia akinamama, nawashukuru sana Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba nijielekeze sasa katika bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Maeneo yetu yanatofautiana kwa kiasi kikubwa. Ninaposema yanatofautiana nina maana gani? Mkoa wa Shinyanga kwa miaka mfululizo sasa tumekuwa hatupati mvua za kutosha na Mkoa wa Shinyanga huwezi kuwaambia wananchi waende wakalime. Yuko tayari kulima kimeungua analima, kinaungua analima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kusema kwa mwaka huu tukaouanza ambao msimu wake wa mvua umekwisha tuna upungufu mkubwa wa chakula. Mkoa wa Shinyanga ni Wilaya moja angalau inakuwa inafanya vizuri kwenye suala la chakula, lakini nayo kwa mwaka huu kidogo hapako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Kwandikwa Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Jimbo lake ndio kidogo ndio kidogo linakuwa linaupatia Mkoa wa Shinyanga chakula, lakini kwa mwaka huu, Jimbo la Ushetu hawakuweza kufanya vizuri kwa sababu ya ukosefu wa pembejeo. Kwa hiyo, nikiuchukua Mkoa mzima wa Shinyanga hali ya chakula tuna upungufu kwa kipindi hiki tunachokwenda naomba Mheshimiwa Waziri atuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa haifanani na maeneo hayafanani, Mheshimiwa Waziri ananitazama naomba hili alichukue alifanyie kazi. Hatupendi Waheshimiwa Wabunge wa Shinyanga kusimama humu tukasema haya, Wasukuma si watu wa kuwaambia kwenda shambani watu wote humu ndani ni mashahidi, Msukuma ni mtu ambaye anainuka mwenyewe anakwenda shambani, hakuna mtu wa kumwambia aende shambani, lakini hali ya hewa ilivyo, ndiyo inatulazimu kufikia hatua ya kusema tuna upungufu wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda sasa hivi mfuko wa sembe, wa kilo 50 unauzwa Sh70,000/=. Ninaposema tuna upungufu wa chakula naomba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi waangalie. Ghala la chakula tunalo pale karibu, hatuhitaji chakula cha bure, tunahitaji wananchi wetu wapate chakula chenye bei nafuu. Niwaombe wafanyabiashara, niwaombe mikoa ambayo wanajinasibu wana chakula cha kutosha, watuletee chakula Mkoa wa Shinyanga watuuzie kwa bei ambayo ni nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niseme kwamba Serikali ya Mkoa wa Shinyanga mwaka 2010/2011 ilikaa na kubaini maeneo ya kuweza kuwa na kilimo cha uhakika katika Mkoa wa Shinyanga ili kuuondoa Mkoa wetu katika kilimo cha kutegemea mvua za juu. Ilibaini eneo la bonde la Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na wataalam kutoka Wizara ya Kilimo walitembelea eneo hili, sijui hayo yaliishia wapi? Tangu mwaka 2010/2011 mpaka leo kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna bonde zuri kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, matokeo yake ni nini. Hata mwaka huu ninavyoongea mvua zimenyesha za mwisho mwisho, bonde lile limejaa maji, lakini hayana kazi tena, yanapotea kwa sababu hatuna sehemu ya kuyahifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara ituangalie Mkoa wa Shinyanga kwa sababu hata aliyekuwa Waziri Mkuu kipindi kilichopita, Mheshimiwa Mizengo Pinda, alikuja Shinyanga na akaiona hali ya Shinyanga akaahidi kulisimamia bonde hili na kuhakikisha Shinyanga tunakuwa na kilimo cha umwagiliaji. Tukikimbilia kusema kule kwenye milima na maporomoko ya maji ndio wapewa kilimo cha umwagiliaji, wanakuwa hawatutendei haki wale ambao hatuna maporomoko ya maji na milima inayoporomosha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali itutazame Mkoa wa Shinyanga kwa jicho la huruma, watutazame waweze kutuwekea miundombinu na kamwe hawatatuona tunasimama na kusema tuna upungufu wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kilimo cha umwagiliaji nasikitika sana, najua kilimo na umwagiliaji ni vitu ambavyo vinaendana kwa pamoja, nina hakika Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji yuko hapa; suala hili lilitekelezwa kwenye umwagiliaji kipindi kilichopita. Mradi wa umwagiliaji wa Kijiji cha Ishololo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. Mradi huu umetumia fedha nyingi, mamilioni ya fedha, lakini ukifika kwenye mradi ule unaweza ukalia. Tumeachiwa mashimo tu. Tuta lile baada ya mwaka mmoja limebomoka na maji yanapita, hakuna kinachohifadhika kwenye bwawa lile la umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Mheshimiwa Waziri akisimama hapa aniambie. Nataka kujua waliokwenda kutekeleza mradi ule wa Kijiji cha Ishololo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamechukuliwa hatua gani kwa sababu mradi ule ulikuwa umelenga kuwafaidisha na kuwanufaisha wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, lakini mradi ule tena hauna tija kwetu kwa sababu tumeachiwa mashimo na tuta lile limekatika na maji yanapita yanapitiliza hayana sehemu ya kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba majibu ya Serikali, Mradi ule wana mpango gani nao ili tuweze kuwa na tija nao, bila ya hilo Mheshimiwa Waziri kwa kweli sitamwelewa. Naomba awasiliane na watu wa Maji na Umwagiliaji wamweleze mradi huu wa Ishololo hatima yake ni nini? Yale mashimo yaliyoko pale hatuhitaji kuyaona, tunahitaji kuona mradi unafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la mbegu. Tunapokwenda kwenye maeneo ya ukame kama Mkoa wa Shinyanga, tunawaambia wananchi wetu wabadilike wapande mbegu ambazo zinastawi kwa muda mfupi. Hata hivyo, kinachonisikitisha sana mbegu hizi zinauzwa bei kubwa sana. Unapomwambia mwananchi akanunue Stuka sijui akanunue Pama sijui akanunue kitu gani, kile kimfuko cha kilo moja kinauzwa mpaka 12,000, mwananchi wa kawaida hawezi kumudu kununua mbegu hizi na kwenda kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewashawishi wananchi kwa kipindi hiki tutoke kwenye zao la mahindi twende tukalime mtama. Mbegu yenyewe ya mtama kwa mwaka huu ilikuwa ni adimu mno, haipatikani. Niiombe Wizara itufanyie mpango mkakati wa kuweza kutuletea mbegu hizi ili na sisi tuweze kuwa tunavuna kwa muda unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye soko la mazao. Miaka ya 2008/2009, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga iliweka mpango mkakati wa kuwa na soko la mazao, soko la mchele. Tunaposema mchele wa Shinyanga maana yake kweli Shinyanga kuna mchele, mchele wa Dodoma, mchele wa Arusha, unatoka Shinyanga. Tulipenda Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tuwe na soko la mchele pale katika Kata ya Didia na mipango hii ilitoka Halmashauri ikaenda mkoani ikaja Wizarani, sijui ilifia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie ana mpango gani wa kuhakikisha kwamba mchele sasa unakuwa na soko lake katika Mkoa wa Shinyanga na kuweza kununuliwa? Kuna watu wengi wanaokuja kununua mchele lakini hatuna soko la uhakika, tunahitaji na sisi kuwa na soko ili mchele wetu uweze kununuliwa sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye mifugo. Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa ambayo ina mifugo ya kutosha. Kwa nini wafugaji wetu wanaondoka? Ni kwa sababu ya hali kama hii ninayoisema ya ukame, marlsho hayapo, maji hayapo, ni kwa nini Wizara haifikirii kwenda kwenye maeneo kama Mkoa wa Shinyanga ambapo wafugaji wanahangaika kuhama na mifugo, wakawapa utaalam wa kupanda zile nyasi ambazo zinapandwa Mwabuki, zinapandwa pale Mpwapwa na maeneo mengine ili wafugaji wetu wasiendelee kuhama na mifugo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika mfugaji ukimwelisha na ukamwonesha hizo nyasi zinapandwa vipi, na zinapatikana wapi, hakuna mfugaji atakayehama kwenye eneo lake na kwenda kutafuta malisho sehemu nyingine.
Naomba Wizara watuambie mna…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba, naomba pia Wizara iongee na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili ule mradi wa umwagiliaji... (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.