Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tuanze mkutano huu wa bajeti mwaka 2016 kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Wabunge na hasa Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu ukiukwaji wa sheria mbalimbali za nchi katika masuala ya bajeti. Jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Andrew Chenge alitoa changamoto kuwa Wabunge tuseme ni sheria gani zimekiukwa katika mchakato mzima wa bajeti ya nchi hii sasa. Kwa maoni yangu, kuna ukiukwaji kadhaa wa Sheria ya Bajeti, Sheria namba 11 ya mwaka 2015, katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu. Nitaeleza kwa ufupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha (8) cha Sheria ya Bajeti kinaeleza namna ambavyo mfumo wa bajeti ya Serikali unapaswa kuwa. Kifungu cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa bajeti unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka planning and budget guidelines zipitishwe na Bunge katika Mkutano wake wa mwezi Februari kila mwaka. Sheria inataka budget ceilings ziidhinishwe na Kamati ya Bajeti na baadaye linapokaa kama Kamati ya Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa Bajeti uliokuwa na Bajeti ya shilingi trilioni 23.7 kama ulivyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango hata hivyo bajeti inayojadiliwa sasa ni shilingi trilioni 29.5, tofauti kabisa na siyo tu viwango vilivyopitishwa na Bunge mwezi Februari bali pia hata vipaumbele vyake ni tofauti. Hili ni suala la utawala bora (governance issue) kwani taratibu za utungaji wa bajeti zimeainishwa na sheria na kama sheria hazifuatwi ni vigumu sana hata bajeti yenyewe kutekelezwa. Ili kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama Kamati ya Mipango na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa bajeti kuendelea au angalau kabla ya kupitisha bajeti kuu mwezi wa Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Ikulu, inapaswa kuzingatia sana sheria na taratibu tulizojiwekea kwani madhara ya kutofuata sheria ni makubwa mno. Kwa mfano, hivi sasa bajeti za taasisi hazimo kwenye vitabu vya bajeti ya Serikali kinyume na Sheria ya Bajeti ambapo hivi sasa bajeti za taasisi zote za umma zinakuwa ni sehemu ya bajeti ya Serikali na Wabunge wanapaswa kuwa na nyaraka za bajeti hizo. Ofisi ya TRA kwa mujibu wa kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti ilipaswa kuunganisha bajeti ya mashirika yote ya umma na kutoa kitabu chake kwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa Wabunge kuhusu masuala haya ili kuzuia ukiukwaji wa Sheria tulizojitungia wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU na kesi za ufisadi mkubwa nchini; ufisadi wa hatifungati ya shilingi trilioni 1.2, Standard Bank ya Uingereza; tarehe 8 Machi, 2013, Serikali ya Tanzania ilikopa fedha $ 600 milioni (1.2 trilioni) kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc. Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda (floating rate) umeanza kulipwa mwezi Machi mwaka huu (kama Serikali imeanza kutekeleza mkataba).
Mkopo huu utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana. Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba jumla ya $897 milioni (takribani shilingi trilioni mbili). Mkopo huu umegubikwa na ufisadi na kwa kuwa baadhi ya Watanzania wamefikishwa Mahakamani kuhusiana na sehemu ya mkopo huu, sitapenda kueleza upande wa waliopo Mahakamani. Kesi iliyopo mahakamani inahusu $6 milioni ambazo inasemekana (kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama) kuwa zilitumika kuhonga Maafisa wa Serikali ili Benki hiyo ya Uingereza iweze kupata biashara iliyopata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo, hawapo Mahakamani mpaka sasa. Vile vile waliotoa rushwa hiyo hawapo Mahakamani mpaka sasa. Waliopo Mahakamani ni wanaosemekana kutumika kupeleka rushwa. Mjumbe kushtakiwa lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mbele yangu nina barua ambayo kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 kutoka kona zote za dunia wamesaini kutaka Benki ya Standard ya Uingereza ichunguzwe kwenye suala hili la hatifungani. TAKUKURU walitumia taarifa ya taasisi ya Uingereza ya SFO katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard Bank. Hatujui ni kwa maslahi mapana ya Uingereza au ni kwa kupitiwa. Sisi Tanzania tumejikuta tunafuata matakwa ya Uingereza katika jambo hili, kiasi cha hata kutumia ushauri wa kitaalam wa Waingereza katika jambo hili. Leo hii TAKUKURU inasaidiwa katika kesi hii na wataalam kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza!
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania walioandika petition kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote kujulikana. Standard Bank walihusika kwa kiwango gani katika kutoa rushwa ili kupata biashara? TAKUKURU wanapaswa kufanyia kazi jambo hili kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, mashtaka ya kutoa rushwa ili kupata biashara nchini. Hata hivyo, TAKUKURU inaogopa Wazungu, inaogopa kuwaudhi watu wanaowapa ushauri wa kitaalam kuhusu kesi za rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maslahi ya Tanzania hapa ni makubwa mno iwapo tutafanikiwa kuonesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu. Tukifanya hivyo, Tanzania itafaidika kwa namna mbili. Moja, itakuwa ni fundisho kubwa kwa Makampuni ya Kimataifa kwamba Afrika sio mahali pa kuhongana kupata kazi na kutoadhibiwa.
Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake, tutakuwa tumeokoa zaidi ya shilingi trilioni mbili katika Deni la Taifa na kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kuhudumia wananchi wetu wenye afya na elimu. TAKUKURU waongozwe na maslahi mapana kwa Taifa badala ya kutafuta sifa ndogo ndogo za wangapi wamefikishwa Mahakamani. Ni lazima taasisi zetu sasa zianze kutazama mambo kwa picha kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii sio mara ya kwanza SFO kufanya ilichofanya dhidi ya Tanzania. Mnakumbuka kesi ya rada na Shirika la BAE la Uingereza. Safari hii Tanzania isikubali kubeba tu makubaliano ambayo SFO inafanya na Makampuni ya Kimataifa. Ni lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya. Haiwezekani wawe ni Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha wanaotoa rushwa hizo wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa zilizopo sasa kwenye vyombo vya habari ni kwamba, Benki hii kupitia tawi lake la Tanzania (Stanbic Bank) siku ambayo walipata deal la Bond ndio siku hiyo hiyo walipewa kazi na Serikali ya kufungua akaunti ya ESCROW kuhusu fedha za bomba la gesi kutoka Mtwara. Kimsingi biashara hii ya ESCROW akaunti katika Benki hii ni kubwa zaidi kutoka ile ya mkopo kwani ni biashara ya kutunza fedha za Bomba kwa miaka 20!
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki hii ilipata biashara kubwa kama hii bila ya kuwepo kwa zabuni yoyote ile na kuleta ushindani. Pia kama kulikuwa na umuhimu wa kufungua akaunti hii ni kwa nini Shirika la TPDC halikufungua akaunti hii katika Benki Kuu ya Tanzania? Haya ndiyo mambo ya TAKUKURU wanapaswa kuchunguza katika kulinda maslahi ya nchi yetu dhidi ya makampuni makubwa kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna taarifa kwamba hata fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huu hazikufika kule kunakotakiwa. Nimewasilisha maswali Wizara ya Fedha kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi zilikwenda. Hata hivyo, kutokana na orodha ya miradi niliyonayo na kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na wakandarasi, mradi wa Kinyerezi na hata mradi wa Kiwira ni dhahiri kuwa sehemu ya fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko. Uchunguzi wa kina unatakiwa kwenye eneo hili ili kupata ukweli na kuzuia mambo kama haya kutokea siku za usoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatumia kanuni ya 120(2) kutaka Bunge lako Tukufu kuunda Kamati Teule kuichunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni yake dada ya Stanbic Tanzania kuhusiana na mkopo wa hatifungani $600m, matumizi ya mkopo huo na ufunguzi wa akaunti ya ESCROW ya Bomba la Gesi Mtwara – Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa nawasilisha mezani nyaraka zote nilizonazo kuhusiana na mkopo huu kwa ajili ya Bunge kupitia kabla ya kuwasilisha hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuichunguza Standard Bank ICBC na Stanbic Bank.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchunguzi wa IPTL Tegeta ESCROW Account, mwaka 2014 TAKUKURU waliijulisha Kamati ya Bunge ya PAC kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka akaunti ya Tegeta ESCROW Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbic Tanzania. Katika taarifa zote ambazo TAKUKURU inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna hata siku moja wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini wahusika waliochota fedha za umma watafikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tupate kauli ya Serikali kuhusu jambo hili kwani ni moja ya JIPU kubwa ambalo tunadhani Serikali inalikimbia. Serikali inaogopa nini? Serikali inamwogopa nani? Kwa nini kesi ya ufisadi wa IPTL inakaliwa kimya?
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni mwanachama wa Open Government Partnership (OGP). Toka ianze, Tanzania ilisaini commitments mbalimbali kuhusu OGP ikiwemo kuwa wazi (online), taarifa ya mali na madeni ya Viongozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba nzima ya Waziri, suala la OGP halijatambulika kabisa. Serikali ina wajibu wa kulijulisha Bunge nini kinaendelea kwenye OGP.
Mheshimiwa Naibu Spika, Manispaa ya Kigoma Ujiji imechaguliwa kuingia kwenye OGP, Sub National Pilot. Hii ni heshima kubwa kwa Tanzania. Naomba Serikali itupe ushirikiano wa kutosha ili Manispaa ya Kigoma iweze kuwa taa kwenye OGP na kuipaisha Tanzania. Naomba Ofisi ya OGP Tanzania iandae mafunzo kwa Watendaji wa Manispaa kuhusu OGP.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kufahamu Serikali imefikia wapi kwenye utekelezaji wa Action Plan ya OGP? Naomba kupata maelezo kuhusu utekelezaji huo ili kuweza kufahamu maandalizi ya Action Plan inayofuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni maeneo gani ya Action Plan yametekelezwa na kwa kiwango gani? Je, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea na OGP? Maana kwenye hotuba ya Waziri sijaona eneo lolote linalotaja OGP.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani mpango huu ni mzuri sana kwa nchi yetu na itasaidia sana juhudi za Serikali katika kupambana na ufisadi kupitia uwazi katika uendeshaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Taasisi ya TAKUKURU kwa kuongeza nguvu ya kupambana na rushwa na ufisadi. Mkurugenzi Mkuu mpya ameanza vizuri sana na kazi ya Taasisi inaonekana kutokuwa na majalada yaliyofunguliwa na kesi zinazofunguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, TAKUKURU inapaswa kutafsiri “inafanya kazi kwa maslahi ya nani?” Ni lazima TAKUKURU kwenda kwenye mzizi wa rushwa ya Kimataifa badala kutaka tu kuonekana kuwa “kesi zimefunguliwa.” Mfano, kesi ya Hati Fungani ya $600m. Bila kuingilia kesi iliyopo Mahakamani ya Ufisadi wa $6m, hivi kwa kesi hii maslahi ya nchi ni nini? Nadhani maslahi ya nchi ni mkopo ghali wa $600m ambao mpaka tutakaporudi kulipa, utagharimu Taifa $897m ifikapo mwaka 2020. Hii inatokana na mfumo wa riba uliotokana na Board hiyo. Nani anafaidika? Ni Benki ya Standard KIC PLC ya UK na investors 1/3.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya TAKUKURU kuna washauri kutoka Uingereza. Unategemea hawa Wataalam wa UK, wataangamiza Benki yao? TAKUKURU lazima iamke na kufanya jambo kubwa ambalo litaitingisha dunia kwa kuchunguza na kuishtaki Benki ya Standard kwa kutoa rushwa ili kupata biashara nchini kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufisadi wa Kimataifa una mtandao mpana sana. Nchi yetu imeingia kwenye deni kubwa la shilingi trilioni 1.2 na riba ya shilingi bilioni 600. Iwapo TAKUKURU ina nia ya dhati ya kumaliza rushwa ya Kimataifa, ni muhimu kuungana na Watanzania duniani ambao wametaka Taasisi ya SFO ya UK kufungua upya jalada la Standard Bank.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili ni suala la national interest tukifanikiwa kwenye hili TAKUKURU itakuwa imeokoa deni la shilingi trilioni 1.8. Iwapo Standard Bank watashtakiwa, Tanzania haitalipa deni hilo, pia itakuwa somo kubwa kwa Makampuni ya Nje kuomba biashara kwa rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la waliopokea rushwa hiyo ya Hati Fungani, mbona hawapo Mahakamani? Benki ilitoa rushwa $6m, waliopokea rushwa ni wale walioleta biashara kwa Benki hiyo, lakini waliopo Mahakamani ni “madalali” wa rushwa. TAKUKURU inapaswa kutoa maelekezo ya kina sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupata taarifa kuhusu uchunguzi wa suala la IPTL na Tegeta Escrow. TAKUKURU walimaliza uchunguzi tangu mwaka 2014. Naomba kupata taarifa ni kwa nini wezi, matapeli na Mafisadi wa IPTL hawajafikishwa Mahakamani?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.