Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, uchangiaji wangu utakuwa na theme kwamba nchi hii inahitaji mabadiliko ya fikra kwa sababu hapa tulipo tumegota. Kama kilimo tunakipa asilimia chinjo kila mwaka, kama kilimo kinapata asilimia tatu tu katika maendeleo, wakati huo tunasema tunataka maendeleo ya kilimo na maendeleo ya kilimo haya tunataka yaungane na viwanda, nafikiri tunahitaji fikra mpya. Hapa tulipo tumegota. Miaka 53 ya nchi hii haiwezekani tusiweze kujilisha au kusimamia wakulima wetu. Nafikiri tumegota na tunataka mabadiliko ya fikra katika kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulipo hivi sasa, nchi hii ina ardhi ya kutosha, ina maziwa ya kutosha, ina mito ya kutosha, ina ukanda wa bahari wa kutosha, lakini ni kitu gani tunajitosheleza? Je, tunajitosheleza kwa chakula? Tunajitosheleza kwa uvuvi? Tunajitosheleza kwa mazao ya nyama au maziwa? Sifikiri katika yote hayo kama tunaweza kuyatimiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema hivi mara nyingi tunakuwa tunalaumiwa, lakini nafirikiri badala ya kwenda mbele kwa kilimo tunarudi nyuma. Kwa sababu baada ya miaka 53 haiwezekani kwa mfano, Kenya ambao sisi tunawapita kwa idadi ya ng’ombe kwa zaidi ya mara mbili ya mifugo wana maziwa ya kutosha sisi hatuna au nchi nyingine nyingi ambazo tunapakana nazo. Kwa hiyo, katika utewekezaji wetu wa kilimo, tumeshindwa kupima muda, fursa na rasilimali zetu. Kwa sababu hiyo, ninaamini kwamba tunahitaji fikra mpya, hapa tulipo, tumegota. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulipo hivi sasa, nchi hii, kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia ni kwamba tuna ekari ambazo ni arable na ambazo zinalimika ni milioni 13,500,000; tuna ukanda wa bahari wenye maili 1,400; tuna eneo la mikoko ambalo lina hekta za mraba 115,000 lakini kwa mfano kwenye bahari mpaka hivi leo hatujaweza kuvuna rasilimali za bahari na wanaokuja kuwekeza tunawakamata, tunawashitaki na tunawanyang’anya vyombo vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utaalamu ambao hautaki tena kuvumbua; nchi za Philipines Cambordia, Malaysia na nyingine zinatumia mikoko ambao sisi tunaihifadhi tu, lakini kina kitu kinaitwa mud crab farming, yaani ufugaji wa kaa katika mikoko ambao una utajiri mkubwa sana, lakini bado hatujautumia. Naamini tumegota katika fikra na tunataka tupate mapinduzi ya fikra. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nashangaa katika nchi hii ambayo asilimia 52 ni misitu. Tuna eneo la maji ambalo linaweza kuzalishwa kwa kilimo ni zaidi ya hekta za mraba 61,500; lakini haielekei kama kuna connectivity baina ya Serikali yenyewe na Wizara kwa Wizara, kwa sababu kama kuna connectivity ingekuwa hadi hivi leo isingewezekana rasilimali zote tulizonazo tusiweze kuzitumia vya kutosha. Nafikiri tunataka fikra mpya, sasa hivi Serikali inaonekana kama imeshindwa katika eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje katika leather industry. Tanzania ni ya tatu kwa ng’ombe Afrika; ni ya 11 kwa ng’ombe duniani. Ina asilimia ya ng’ombe asilimia 1.67 ya dunia. Tumefaidika nini katika leather Industry? Kama hatuna leather Industry, ina maana hakuna maana ya kufuga ng’ombe maana hatupati maziwa ya kutosha, hatuna viwanda vya maziwa, ngozi yetu hatuitumii vya kutosha. Kwa hiyo, haina maana ya kufuga. Nafikiri tumegota, tunataka fikra mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye mazao ya chakula, tumebaki katika yale yale ambayo ni traditional; na vile vile mazao ya biashara ambayo ni traditional. Sasa hivi sisi tunajifunza, tuna hali ya hewa nzuri sana au ya kila namna; ipo joto kidogo, baridi kidogo, ipo ya mchanga kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mazao mapya ambayo tunaweza kuyavumbua, tumeingia kwenye vanilla kidogo kwa Kilimanjaro na Kagera. Hivi sasa bei ya vanilla ni dola 500 kwa kilo moja. Sisi kama nchi tumehiza vipi zao hili? Kuna mazao kama zafarani (saffron) ambayo kilo moja ni dola 4,000. Tumefunguka vipi kama nchi? Nafikiri tumegota na tunataka mapinduzi ya fikra. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna masoko yamejifungua chungu nzima. Tuna Vietnam wamekuja kuingia mkataba na sisi, tuna Wachina, tuna Waturuki; tumefikiria vipi juu ya mazao? India peke yake inaweza kumeza kwa siku 15 mazao yote ya choroko ya Tanzania, kunde zote za Tanzania. Tumewafunza vipi watu wetu kutumia soko hilo? Tunataka mabadiliko ya fikra, tunafikiri CCM mmegota kimawazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii pia hatuoni upya wa mambo ambayo tunayafanya. Walisema kwamba walitaka wamtue mwanamke ndoo, walisema wanataka wamnyang’anye mkulima kijembe cha mkono, lakini kwa miaka kadhaa hivi leo bado ni tradition farming. Niambieni nchi hii, wapi kuna shamba la kilimo la kisasa la mwekezaji ambaye analima kwa maelfu ya heka kuitoa nchi hii katika njaa? Nafikiri mmegota na inabidi tupate mabadiliko ya fikra. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kuna haja kubwa ya mabadiliko. Kwa fikra zangu, nadhani sasa hivi irudisheni agenda kwa wananchi, mwaambie wananchi kwamba katika kilimo, mifugo na uvuvi, mmeshindwa; ili baada ya bajeti hii turudi tena kwa wananchi tujadili jambo hili. Kwa sababu nafikiri kunahitajika mapinduzi ya fikra na fikra hamwezi tena kuitoa ninyi kwa sababu mmeshindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.