Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Mariamu Ditopile Mzuzuri

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Naomba nitangulize shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza ahadi yake. Alisema kipindi cha kampeni, yeye akiahidi anatekeleza. Kwa Wana-Dodoma ametuletea Makao Makuu na kweli Serikali imeshahamia. Kipindi cha kampeni wananchi waliilalamikia CDA kwamba amethubutu, ameivunja mamlaka ya ustawishaji. Sisi tunamwambia tuko naye bega kwa bega, tunasema uungwana ni vitendo asubirie 2020, Dodoma tuko naye pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyongeza tu ni kwamba Serikali tunaomba sasa muda muafaka umefika wa kuleta muswada wa Sheria ya Makao Makuu. Leo hii tunajadili Wizara nyeti, tunajadili maisha robo tatu ya Watanzania. Kwa mujibu wa hotuba yako Mheshimiwa Waziri, umesema kwamba sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, imeajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania.

Waheshimiwa Wabunge, everybody is entitled to his/ her opinion, lakini lazima tuseme ukweli. Wao wanaosema tumeganda wakati Sudan inategemea chakula kutoka Tanzania, Kenya wanategemea mahindi kutoka Tanzania, Uganda wanategemea mahindi kutoka Tanzania na mazao mengine! India wanategemea chorosho, choroko, dengu, mbaazi zote zinatoka Tanzania. La msingi ni kwamba tunatakiwa tuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naomba niwaambie, Waziri wa Fedha na Naibu Waziri, naomba mnisikilize. Mipango yenu ni kwamba tunataka kupeleka nchi kwenye uchumi wa viwanda, tunataka kuwa na uchumi wa kati, tuwekeze kwenye kilimo, mifugo na uvuvi. Kilimo, mifugo na uvuvi ni afya, kilimo, mifugo na uvuvi ni ajira, itampunguzia kaka yangu Antony Mavunde adha aliyokuwa nayo. Kilimo, mifugo na uvuvi ni fedha na uchumi, kilimo, mifugo na uvuvi ni amani. Tukiwa na njaa tutaweza kuwa na amani?

Kwa hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, ukipeleka hela kwenye kilimo, mambo yako yote, mpango wa maendeleo utafanikiwa kwa asilimia 200. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi, lawama nyingi sana zimemwendea Mheshimiwa Waziri. Namfahamu Mheshimiwa Waziri. Nimeshalima naye, ni mkulima mzuri sana. Tena bahati nzuri analimia hapa hapa katika Mkoa wetu wa Dodoma. Mheshimiwa Waziri amekua kama mtoto wa mfugaji, kazaliwa kwenye jamii ya ufugaji, anatoka Kanda ya Ziwa, anaelewa uvuvi. Ukikaa na Mheshimiwa Waziri, maono aliyokuwanayo kwa Wizara yake ni makubwa, lakini hana fedha, atafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze umuhimu wa utafiti, sayansi na teknolojia katika kilimo. Kwa Kiingereza tunasema, science and technology innovation in agriculture. Tunasikitika, bajeti ya ugani iko wapi? Bajeti ya utafiti ikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu chote, leo hii nchi yetu ina watu takriban milioni 50, baada ya miaka 10 tutakuwa na watu zaidi ya milioni 65. Hakuna mpango mkakati wa kutuvusha kutupeleka huko na yote Mheshimiwa Waziri siyo kosa lake; huna utafiti, uta-project vipi? Utapangaje mipango yako vizuri kama hujafanya utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote, niwaambieni, dunia nzima kati ya watafiti wanaoheshimika ni Tanzania. Kigoma Watanzania walifanya utafiti wa mbegu ya michikichi ambayo Malyasia ndio wanatumia. Leo hii niwaambieni, kuna Mtanzania mmoja alikuwa Serikalini, amefyatuliwa risasi juu, amechukuliwa na Bill Gates Foundation Marekani kama mtafiti na aliombwa abaki kule afundishe masomo ya kilimo, lakini amechukua uzalendo wake, amerudi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa utafiti naomba niwaambieni Serikali, leo hii mjiulize kwenye uvuvi, Ziwa Victoria sisi ndio wenye sehemu kubwa, lakini ukienda kwenye statistics za dunia, Uganda imetupita, yenyewe ni ya sita katika uvuvi wa Ziwa Victoria. Sisi ni wa nane, kwa nini? Leo hii tujiulize Bukoba kahawa mwaka 1978, miaka 30 na kitu iliyopita walikuwa wanazalisha zaidi ya tani 140,000, lakini leo kwenye kitabu mmeona, tuna-project kuvuna tani 47,000 kwa sababu hatujafanya tafiti ya kuendeleza hizi kahawa. Miche imekuwa mikuu, haizalishi, imekuwa dormant. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu niwaeleze umuhimu wa science and technology innovation. Leo hii tunafurahi hapa kusema kwamba tunalisha East and Central Africa, lakini tusipojipanga vizuri, tunu hii tuliyopewa na Mwenyezi Mungu tutaikosa, Malawi wamejipanga kwenye pamba. Malawi ni nchi ndogo, lakini leo hii inaenda kutupita kwenye uzalishaji wa pamba kwa sababu ya tafiti na kujipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuongelea suala la mbegu. Tumejaribu sana kuendeleza kilimo. Nashukuru Serikali ilijaribu kutoa matrekta, lakini hebu tuweke azimio, Mheshimiwa Waziri, kaa chini. Vituo unavyo, mahitaji unayajua, sitaki kuzungumzia sana yaliyokuwemo humu. Hebu tusonge mbele, tuwafunge watu midogo. Tuweke azimio kwamba Serikali ihakikishe kila mkulima anapata mbegu bora. Wakulima wetu wamekuwa wanatumia nafaka. Nendeni mkasome muone tofauti ya mbegu na nafaka (seed and grain). Mkulima analima heka yake moja, akivuna mahindi, yale yale aliyoyavuna, anahifadhi anaifanya mbegu. Siyo mbegu! Atajikuta alivuna mawili atabaki na moja. Kwa hiyo, tuweke azimio, uwezo huo tunao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba kuzungumzia Mkoa wangu wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma unafanya tremendous kwenye kilimo, ingawa watu wanajua kwamba ni kame. Msimu wa mwaka 2013/2014 Tanzania iliuza tani 860,000 China, kati ya hizo tani 300,000 ufuta umetokea hapa Dodoma. Tuna maonyesho ya Nane Nane. Pale inaonekana mazao yote yanawezekana. Kwani ile ardhi ya Nane Nane ni ya wapi? Ni Arusha? Siyo ya Dodoma! Lakini humu sijaona Mheshimiwa Waziri. Nina vijana wengi na kila siku nawapigia kelele waingie kwenye kilimo. Hebu tuhamishe basi ile Nane Nane tuipeleke Chamwino, tuipeleke Kondoa, tuipeleke Chubi. (Makofi)

Mheshimiwa Ally Saleh kauliza kuhusu shamba kubwa, twende Chubi kwa Mheshimiwa Kijaji ukaone shamba kubwa za hizo heka unazosema na mwekezaji ujifunze. Tembea, no research, no right to speak. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongea kwa sababu niko field, najua raha ya kilimo, najua machungu ya kilimo, najua mafanikio na ninajua tukiweka nguvu kidogo, tutafika mbali. Nataka sana vijana. Vijana wanataka red market, wanataka mitaji, hatuna sehemu ya kuwapeleka zaidi ya kilimo. Tuwekeze jamani! Leo hii haiwezekani, nchi ya Egypt ina River Nile peke yake. Source ya River Nile ni Lake Victoria. Kale ka-Nile kanatokana na Lake Victoria wanakatumia, wanafanikiwa vibaya mno! Sisi wenye Ziwa Victoria, wenye Ruvu na mito kibao hatuongei, kwa nini tunashindwa kutumia hizi fursa? Tumeona mwenyewe Mheshimiwa Waziri umeshasema hii ndiyo sekta ambayo inaleta pesa kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie kwenye uvuvi katika Ziwa Victoria, kuna samaki anaitwa sangara. Sangara jamaniā€¦(Makofi)

(Hapa kengele ililie kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)