Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo. Pia nielekeze mchango wangu kwenye eneo la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema lolote, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Mawaziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwatetea na kuwasimamia wakulima. Ni kweli kwamba kilimo kinachukua nafasi kubwa ya Watanzania, lakini pia ni kweli kwamba tunaendelea kuimarisha mifumo ya kutetea haki na maslahi ya wakulima kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pia kwamba kuna umuhimu mkubwa wa Wizara ya Fedha kuangalia uwezekano wa kutoa fedha za kutosha kwa Wizara hii. Ukiangalia ukurasa wa 25 wa hotuba ya Waziri, unaonesha wazi kwamba fedha zinazotolewa ni kidogo sana hadi kufika Mei mwaka huu. Haitawezekana kutekeleza mipango na mikakati ya Wizara hii ambayo inabeba msingi wa uchumi wa nchi yetu kama fedha zinazotolewa hazitoshi mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kufikiria utaratibu mpya wa utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa 100% kwa wakulima. Hili ni jambo kubwa sana na ni jambo ambalo linaweza likachochea maendeleo katika sekta ya kilimo, hususan sisi tunaotegemea kilimo cha korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie utaratibu wa namna ambavyo mazao mchanganyiko yanaweza kununuliwa mwaka huu. Katika msimu uliopita wa mazao mchanganyiko kwa upande wa Mikoa ya Kusini, nazungumzia mbaazi na choroko, bei ya kilo moja ilikuwa shilingi 400 hadi shilingi 600. Ukweli ni kwamba bei hii haitoshelezi na haifanani na gharama za uzalishaji wa mazao haya kwa kilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza tayari wanunuzi wa choroko wameshafika kwa wakulima na wanaanza kununua choroko kwa shilingi 900; hii bado ni bei ya chini sana. Tunaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kusimamia uuzaji na ununuzi wa mazao haya ili kuwafanya wakulima wetu waweze kuona mazao yao yana tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa na Serikali kwamba wametafuta soko nchi za India, Vietnam na nchi nyingine ambazo wanatumia mazao haya kwa wingi, lakini hali halisi ya ununuzi wa mazao haya haiendani na kauli ya Serikali. Tunaomba sana, jambo hili liweze kusimamiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo kuhusiana na suala la kilimo cha korosho pamoja na suala la ununuzi na uuzaji wa zao hili. Naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuondoa tozo katika zao hili, kupunguza baadhi ya tozo. Tozo hizi baada ya kupungua zinapandisha bei, lakini zinatoa matumaini zaidi kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo katika zao la korosho zinawagusa kabisa wakulima. Zinawagusa na wanaziona zina tija kubwa, lakini yapo mambo ambayo Serikali inapaswa kuyatilia mkazo zaidi. Tunashukuru mwaka 2015/2016 ulifanyika ubadhirifu na Serikali katika mwezi huu inaendelea na imepiga hatua kubwa kuhakikisha kwamba wale waliofanya ubadhirifu katika tasnia hii ya korosho wanachukuliwa hatua kwa kuondolewa kwenye uongozi. Hili ni jambo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, katika msimu wa 2016/2017 korosho zimenunuliwa kwa bei nzuri na wale waliofanya ubadhirifu mpaka sasa hivi tunavyozungumza kesi yao iko mahakamani. Haya ni mambo ya msingi yanayoendana kabisa na kasi ya Serikali ya kutetea maslahi ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo la kujiuliza, kuna ambao walifanya ubadhirifu mwaka 2015/2016 na kuna ambao wamefanya ubadhirifu mwaka 2016/2017 na mpaka sasa tunapozungumza wakulima wa korosho wanadai fedha zao hata kwa msimu huu uliopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa korosho 2016/2017 katika Wilaya ya Masasi peke yake wakulima wanadai zaidi ya shilingi bilioni 1.5. Umefika wakati sasa wa Serikali kuhakikisha wakulima hawa wanalipwa. Serikali inaweza kuangalia uwezekano wa kutumia hata fedha ambazo zilikuwa ni michango yao wakulima, fedha ambazo zimewekwa katika Mfuko wa Pembejeo. Je, Serikali haiwezi kutumia fedha hizi kuwalipa wakulima wakati wanaendelea na utaratibu mwingine wa fedha hizi kurudishwa? Kwa sababu hali ya wakulima wetu ni mbaya na wakulima wanaendelea kudai, na sisi tumechoka na huu mzigo wa kuwasemea kila siku wakulima kwa mambo ambayo hayatatuliwi. Fedha zao zinatakiwa zipelekwe, walipwe kwa sababu korosho hizi zimeshauzwa, fedha zimekwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kero imezidi kuwa kubwa. Tunaomba Serikali itoe tamko na Waziri anapofanya majumuisho atuambie na asiposema nitashika shilingi kuhakikisha kwamba Waziri anaeleza commitment ya Serikali katika jambo hili. Korosho za wananchi bado hazijalipwa katika msimu uliopita, Serikali inaendelea na huo utaratibu, lakini ituambie ni lini jambo hili litakwisha? Wananchi wameuza korosho toka mwaka 2016 mwezi Oktoba, wengine mwezi Novemba. Kwa hiyo, Serikali ituambie inafanya nini katika hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la ushirika. Tunalo tatizo na Serikali ina jukumu kubwa sana la kuimarisha ushirika. Sekta ya Ushirika kwanza inakabiliwa na rasilimali watu ambayo haina weledi wa kutosha wa kusimamia ushirika. Serikali tunaomba iliangalie hili kuanzia katika vyama vya msingi mpaka katika Chama Kikuu cha Ushirika ili kuwa na watu wenye weledi wa kutosha wa kusimamia hasa yanapofika masuala ya fedha za wananchi. Kwa hiyo, Serikali iliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo lingine la ziada. Tunao watendaji wa Serikali, tunao watumishi ambao wana maslahi ndani ya mfumo wa ushirika na wana maslahi ndani ya biashara, hususan biashara ya korosho. Tumeeleza mambo haya kwa muda mrefu na Serikali baadhi ya mambo inaendelea kuyafanyia kazi; lakini tunaeleza wazi hatutakuwa tena tayari kuendelea kufanya kazi na watumishi ambao kwa namna moja ama nyingine wana maslahi ndani ya mfumo wa ununuzi na uuzaji wa korosho. Kwa kweli hawawezi kusimamia mfumo huu kwa kutetea maslahi ya wakulima wetu. Tunaomba Serikali iendelee kuchukua hatua na iwaondoe wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanashiriki katika biashara ya korosho na kushindwa kuwasimamia wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo ya kuzungumza. Naunga mkono hoja ya Serikali. Ahsante sana.