Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye Wizara hii nyeti.

Awali ya yote, kwanza nawapongeza Serikali kwa kuondoa tozo zile ambazo zilikuwa ni usumbufu sana kwa wananchi wetu hasa wakulima. Nawapongeza sana kuwa Serikali sikivu na kuweza kutuondolea hiyo kero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianzie kwenye mifugo. Kuna sehemu moja inaitwa Nkenge, Misenyi kule kuna blocks. Zile blocks kuna watu wamezikodisha lakini hawana mifugo. Ajenda hii ni ya muda mrefu, tangu alipokuwa Mheshimiwa Mbunge Mshama, amekuja Kamala na mimi leo naichangia ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Serikali ni nini? Serikali inajua, kwamba wafugaji wa eneo lile sio wale ambao wana asili ya maeneo yale. Watu wamechukua ma-block wanakaa Dar es Salaam na popote wanapokaa, watu kutoka nje wanaingiza mle mifugo wanakodisha. Wananchi wa eneo la Misenyi hawana mahali pa kufugia, wanatangatanga na mifugo yao. Wasukuma walioko huko wanafukuzwa, wanafanya nini, sasa Serikali ituambie, suala hili limekuwa la muda mrefu. Mheshimiwa Waziri wakati anakuja hapa hebu, aje na majibu mazuri ili usituamishie kwenye taratibu zile nyingine za kutaka kujua kwa nini mpaka leo Serikali inakuwa na kigugumizi katika eneo hili la Misenyi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wana haki yao katika nchi yao, lakini unafanyaje kumpa block mtu mfanyabiashara? Je, vigezo vyenu ni vipi vya kugawa hizi blocks wakati mnawapa watu? Kila mwenye hela ndio anapewa, lakini hana mifugo. Watu wanateseka, wanaangaika, watu wa maliasili wanakamata ng’ombe za Watanzania, zinakwenda kwenye shida, lakini wale watu maeneo yapo. Serikali haifanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili tunaomba majibu sahihi ili angalau tuwaambie wananchi wetu kule kwamba haki yao ya kufuga inafananaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye eneo la uvuvi. Wavuvi hasa nchi nzima sasa, wamekuwa wakichomewa nyavu zao, wakinyang’anywa, wakikamatwa wakisumbuliwa, sisi wavuvi tunafuata maji yalipo, lakini nyavu zinauzwa madukani na viwandani. Sasa Serikali pamoja na kwamba inakusanya kodi kutoka kwenye nyavu, ni lini italeta sheria humu Bungeni kwamba labda hizo nyavu zisitengenezwe? Kwa sababu mimi ni mvuvi, nimeshanunua nyavu, nimepeleka majini, kesho nakamatwa mimi na mali yangu. Anayepata hasara ni mtu huyu mlalahoi. Sasa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi inawajali wanyonge. Wanyonge hawa wa kuvua, lini haki yao itapatikana? Kule anayewauzia, anawapa risiti. Kwa nini, hamnyang’anyi mkafuata mwenye duka aliyemwuzia akarudisha gharama yake basi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi kwa kweli ni shida. Mheshimiwa Waziri atuambie, ni lini wanaleta sheria ya hao wanaosabisha kuuza halafu wananchi wanaonunua ndio wanakuwa na hatima ya kunyanganywa mali zao, kufilisika, kupata taabu na kuchomewa mitumbwi? Ni shida sana. Kwa hiyo, naomba viongozi wa Wizara ya Kilimo na Serikali yangu tuleteeni majibu mazuri ambayo yatawapa imani wavuvi kule walipo baharini na ziwani ili wawe na amani na kazi yao kwa sababu ndiyo maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la ajira, ambalo pia ni eneo la Kilimo. Katika utaratibu, tunapenda viwanda, tunapenda uwekezaji, na kadhalika. Nataka kuuliza swali moja, nina mtu anaomba nimtaje kabisa, nita-declare interest. Kuna mtu anaitwa Vedic yuko kwenye Kampuni inaitwa Alpha Group. Mtu huyu mwaka 1997 sisi wavuvi wa Kanda ya Ziwa tutakumbuka, alikuja kama mhasibu kwenye kiwanda kinaitwa TFP (Tanzania Fish Process) pale Mwanza kama mhasibu. Kibali chake cha kuishi alikuwa na kibali Class
B. Leo ni miaka 20 anaitwa Manager Group. Hivi akija mtu kama mhasibu mpaka akafikia umeneja, Watanzania wangapi wanakosa kazi kwenye eneo hilo? Huyu mtu analindwa kwa style gani? Kibaya zaidi mtu huyu amezidi kuongeza wafanyakazi wa nje akiwaleta kama watalaam wa samaki, lakini watu hao leo tukienda pale Kipawa wanauza samaki. Yaani yupo pale anapokea hela ameingia kama mhasibu. Ukienda pale Kilwa wanavua mpaka pweza. Mtu amekuja kama mhasibu ni mtu wa nje, anazuia Watanzania kufanya kazi ambazo ana uwezo nazo, anavua samaki pale, anavua mpaka pweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka pale, shuka kule Tunduru anauza, Kilwa Kivinje anauza, Mtwara Supermarket wanauza, Lindi, Songea, sasa hivi ajira mnazilindaje jamani? Ninyi watu wa Kilimo na Mifugo, inawezekanaje akaja mtu miaka 20 anapewa kibali huyo huyo? Kile alichokuja kufanya, haijawahi kupatikana Watanzania wenye sifa hizo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema mimi ni mfanyabiashara wa samaki, namjua, wala sisemi kwa bahati mbaya. Anayetaka kunijibu aje nimpe majibu, ninayo. Mtu huyu ameondoa Watanzania wote kwenye ajira, analeta ndugu zake, wanawaingiza mle kama wataalam samaki, kazi wanayofanya sasa, wako mtaani. Lini Mhindi akaenda kuchukua pweza baharini? Amepita wapi? Vibali (permit) hivi nani anatoa? Tunawalindaje Watanzania wetu waliosoma ambao wazawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuseme, Serikali yangu naomba inisamehe katika hili, lazima niseme. Huyu mtu anaitwa Vedic katika nchi hii, yeye ni nani? Mpaka anaingia kwenye siasa, naye anachagua watu wanaotakiwa kuwa viongozi katika nchi hii. Kwa kibali kipi? Naomba Mheshimiwa Waziri aje na maelezo hapa, huyu Vedic ana kibali cha aina gani katika nchi hii? Kwa nini vibali watu wanavyokuja navyo hawavifanyii kazi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu kama RK ana miaka 20 nchini. Tangu alivyokuja Vedic, RK akaja, wakienda ukaguzi, wanafungiwa kabatini. Nchi ipo, kwa nini? Hawa Watanzania mnawasaidiaje? Raslimali ni zetu lakini mnasema wawekezaji waje, hamwendi kuwakagua na ninyi ndio maliasili pale. Ndiyo wazee wa uvuvi mko hapa. Kwa nini hamwasaidii Watanzania wenzenu? Viwanda hivi si viko chini yenu? Kwani hamna haki ya kuuliza? Sisi tunawapa data, wataalam wenu kule kama wame-associate na wale, nao mwende mwambie. Haiwezekani, haiwezekani mtu miaka 20 amekuja mhasibu, leo ni Group Manager, haiwekani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda pale Mafia, nimekaa Mafia Kilindoni. Pale Vedic, miaka hiyo, mpaka leo, hapana! haki ya Watanzania lazima ipatikane. Haki ya Watanzania kama Wizara ya Mifugo, ninyi ndio mmekalia; tutaleta na maswali mengine humu ndani. Mheshimiwa Waziri bila kunipa maelezo ya kina, sijawahi kushika shilingi, lakini leo niko na wewe. Lazima unipe majibu ya kina. Inakuwaje mtu mmoja anakuja kama mvuvi, leo anataka na kwenye siasa atupangie nani achaguliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, nina swali na ninaomba kutoa maelezo kidogo. Hivi suala hili vipi? Hawa watu wetu wanaouana kila siku, wakulima na wafugaji, Serikali mmejipangaje? Leo tunaliongelea kwenye kilimo, lakini kwa mawazo yangu kidogo naomba nitoe ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili linaihusu ardhi, kwa sababu lazima ardhi apange maeneo ili watu wasiuane. Eneo hili linahusu maliasili, leo ng’ombe wako kule, wanafukuzwa, wanachinjwa, wanauzwa shilingi 5,000. Suala hili linahusu sheria, linahusu maji, lazima kuwe na visima na malambo ya watu ambako watu watawapeleka ng’ombe, linahusu TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri atuambie, lini mnakuja na ajenda ya kuwanusuru wananchi wetu kufa. Watu kuuana kwa kugombania maeneo ya malisho ya uchungaji. Lini mnakuja natafasiri kamili hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua suala hili ni mtambuka hamwezi kulifanya ninyi, lakini ninyi kama Serikali lini mtakaa kuleta majibu kuwaokoa Watanzania hawa.

Hawa watu wanaouana ni Watanzania, tuna haki ya kuwalinda, tuna haki ya kuwahudumia, lakini tukisema leo, wewe Bwana Mifugo utasema mimi sina ardhi, utasema sina maji. Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri atuambie, Serikali mtuambie lini mnaenda kukaa pamoja mkakutana mkaleta majibu ya yanayofanana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekti, naunga mkono hoja.