Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya mimi kuungana na wachangiaji wenzangu katika kuchangia Wizara hii ya Kilimo na Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema. Sambamba na kumshukuru Mwenyezi Mungu, naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujali muda naomba niende moja kwa moja ukurasa wa 22. Katika ukurasa huu Wizara imeendelea kuhimiza matumizi bora ya mfumo wa stakabadhi ghalani. Naomba nimpongeze sana Waziri na naweza nikasema kwamba Waziri Mheshimiwa Dkt. Tizeba amekuja na mguu mzuri kwenye Wizara hii kwa sababu miongoni mwa watu ambao wamenufaika na mfumo huu wa stakabadhi ghalani ni sisi wakulima wa korosho wa Mkoa wa Ruvuma na hususani wa Wilaya ya Tunduru na Namtumbo tumefaidika sana kupitia mfumo huu wa stakabadhi ghalani na ni imani yangu kwamba kupitia mfumo huu utawezesha sana kuwasaidia wakulima wa korosho katika maeneo yote ambayo tunalima korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuwa rahisi kuukubali mfumo huu kwa sababu kumbukumbu zangu zinaonesha mwaka 2011/2012 wakulima wa korosho Wilayani Tunduru na maeneo mengine tulitumia mfumo huu lakini mpaka hivi tunavyozungumza wakulima wale hawakupata pesa zao bado wanadai. Kwa hiyo, haikuwa rahisi kuukubali mfumo huu kutokana na hizo changamoto ambazo zimejitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa nafasi ya pekee sana naomba sana nimpongeze Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na watendaji wake kwa hakika walijitahidi sana kuelimisha wananchi hatimaye waliendelea kuelewa mfumo huu na hivi sasa tunavyozungumza naomba niseme kwamba umeleta tija sana kwa wananchi wetu na mimi ni miongoni mwa waumini wa mfumo huu nitaendelea kuhamasisha kama kiongozi kuhakikisha mfumo huu unaendelea kuleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tulikuwa na kikao cha wadau, kupitia kile kikao cha wadau kumetolewa tamko la kugawa sulphur bure. Ni jambo jema na ni jambo lenye tija lakini naomba Waziri alete mchanganuo na vigezo ambavyo vitatumika katika kutoa sulphur. Kwa kuwa jambo hili lina tija lisije likaleta migogoro baadaye. Hivi tunavyozungumza wako wakulima kwenye mashamba yao wanatumia kuanzia mifuko 10, 20 na zaidi sasa tulipotangaza sulphur bure inawezekana watu wakabweteka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Wizara inayohusika ikatoa mwongozo mapema kujua vigezo ambavyo vitatumika katika kutoa hiyo sulphur. Niliomba nisisitize hili na nilisisitize sana kwa sababu linagusa wananchi. Kama hiyo haitoshi naendelea kusisitiza kwa sababu wako wafanyabiashara ambao wamekuwa wakileta sulphur kutoka nje ya nchi kuwauzia wakulima wetu sasa wasije wakabweteka kwa kuamini kwamba Serikali sasa itatoa sulphur bure na wale wasilete sulphur matokeo yake tena badala ya kuimarisha zao la korosho tukaliletea tena matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha basi ni vizuri aeleze ili wananchi wale ajue kwamba mfumo na vigezo vitakavyotumika katika kutoa sulphur bure. Ni jambo jema, binafsi napongeza Serikali yangu na kwa kuwa Serikali hii ikitamka inatekeleza naamini itatekeleza lakini ni vizuri iweke mchanganuo watu wajue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la tozo. Binafsi naomba nipongeze sana. Tunapozungumzia hizi tozo moja kwa moja zilikuwa zinagusa wakulima wetu. Tunapopunguza hizi tozo maana yake tunapunguza mzigo kwa wakulima wetu, naipongeza Serikali na naomba niendelee kusema kwamba hata kama kuna tozo zile zingine ambazo zinaleta ukakasi kwa wananchi wetu basi waziondoe ili mazao yetu haya yaendelee kuwa na faida, kwa mazao yote kwenye korosho, kahawa na mazao mengine yote. Kama kuna tozo zile ambazo zinaleta kero kwa wananchi wetu basi ziondolewe ili kuleta faida ya kilimo bora kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la uvuvi. Kwenye eneo hili la uvuvi naomba nizungumzie Wilaya ya Nyasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.