Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Wizara hii ndiyo utii wa mgongo wa nchi yetu ya Tanzania lakini niwashukuru sana na kuwapongeza Mawaziri wote wawili mara nyingi sana nikiwa na changamoto huwa nawaona, Naibu Waziri amekuwa akinisaidia na Waziri amekuwa akinisaidia, kwa hiyo nawapongeza sana. Niwapongeze kipekee zaidi baada ya kutoa tozo katika mazao mbalimbali ambazo wakulima ilikuwa ni shida na changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri mchache kwa Serikali hasa tukianza na Jimbo langu la Busokelo ambako mara nyingi sana tunazalisha lita za maziwa zaidi ya 30,000,000 kwa mwaka lakini yanaharibika kabla hayajafika kiwandani kwa sababu hatuna kiwanda katika Halmashauri ya Busokelo. Tumejitahidi kujenga lakini tumeshindwa, tunaomba Serikali iweze kutusaidia katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu tunazalisha pia ama tunalima viazi mviringo, viazi vitamu, ndizi kwa wingi, mpunga na mazao mengine mbalimbali na hayo yote yanashindwa kufika sokoni kwa sababu ya miundombinu ambayo haiko rafiki kwetu. Kwa hiyo, tunaomba kama itawezekana kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo katika maeneo yale kwa kuwa ninyi watu wa kilimo ndio wenyewe kwa sababu ninyi ndio mnaosimamia sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tozo ambazo zimetolewa hasa katika zao la chai. Zao la chai sisi ni wakulima wakubwa katika nchi hii ya Tanzania katika Wilaya ya Rungwe. Kuna hii tozo ambayo inaitwa gharama za uendeshaji wa vyama vya wakulima nafikiri kwa typing error imeandikwa ni Sh.5 lakini tozo hii ni Sh.9.50, ningeishauri Serikali isiiondoe kwa sababu kwanza hivi vyama ni vichanga na Serikali inahubiri habari ya ushirika. Sasa wakishawaondolea hawa maana yake watatawanyika kabisa hawatakuwa na nguvu yoyote ya kuweza kusimama na kulisimamia zao hili la chai, kuna kodi nyingi ambazo ningeshauri huko ndiko wangeweza kuondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, zao la cocoa pia tunalima kule lakini hapa sijaona hata kidogo kutamkwa katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Naomba pia walizingatie kwa sababu ni muhimu na linaingiza fedha nyingi za kigeni kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pembejeo limekuwa likizungumzwa lakini nipongeze Serikali kwa sababu tumeamua kwamba ziletwe kwa bulk procurement. Wazo langu na ombi langu kwa Serikali kwamba katika nchi ya Tanzania kila sehemu tunazalisha ila kwa bahati mbaya majira yanatofautiana. Kwa hiyo, hata kama watanunua hizo pembejeo basi ziende kwa majira husika katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la TEHAMA na kilimo. TEHAMA na kilimo kwa nchi ambazo zimekomboka limekuwa ni msaada mkubwa sana katika nchi hizo. Hii TEHAMA itumike vizuri katika kuendeleza mazao mbalimbali nchini si kilimo tu hata uvuvi lakini pamoja na shughuli zingine zozote za kibinadamu zinazomwingizia kipato. TEHAMA inatumika namna gani? Kama sasa hivi tukijenga data center itapunguza gap kati ya watafiti wanaofanya tafiti pamoja na mkulima kwa sababu mtafiti mara nyingi anafanya tafiti lakini zile tafiti haziwasaidii wale wakulima wadogo wala wavuvi, wala wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kupitia TEHAMA maana yake watakuwa wanapata SMS direct kutoka data center hiyo kwenda kwa mkulima kama watakuwa na simu za mkononi tu inatosha kabisa. Kupitia TEHAMA pia tutapunguza majanga mbalimbali kwa kutoa taarifa kwa jamii mapema. Kwa mfano, mwaka jana tulikuwa na changamoto kubwa ya ukame, kama wakulima wa maeneo mengi wangepata taarifa kwamba kuna changamoto za ukame zinakuja kupitia simu za kiganjani mikononi mwao tusingekuwa na shida ya chakula katika maeneo tofauti tofauti katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tu TEHAMA itasaidia zaidi kutafuta masoko. Kama Serikali itakuwa inasaidia kutafuta masoko dunia halafu wanatuma massage moja tu kwa wakulima fulani labda wa zao la pamba, chai, kahawa na mazao mengine maana yake itasaidia wale wapate taarifa mapema kuliko vile ambavyo kila mkulima mmoja mmoja anajitafutia soko lake pale anapoona yeye inafaa. Kwa hiyo, tukiwekeza katika TEHAMA najua na nina hakika kwamba wakulima wetu hawatakuwa kama walivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango wangu huu kidogo, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana.