Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja. Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha mapinduzi makubwa kwenye uchumi wa viwanda yanapatikana lakini tutafanikiwa tu iwapo tutakuwa na mikakati thabiti ya kulima kilimo cha kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali bado kuna changamoto nyingi ambazo hazina budi kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuyafikia malengo ya uchumi wa viwanda. Tukilima kilimo cha kisasa tutapata malighafi za kutosha, tutapata chakula cha kutosha na kuweza kuuza mazao ya biashara ndani na nje ya nchi na tatizo la njaa nchini litageuka kuwa historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 80 ya wakazi wa Mkoa wa Singida wanajishughulisha na kilimo na ndiyo ajira kubwa kwa vijana na wanawake. Hulima mahindi, mtama, mihogo, uwele, viazi vitamu kama mazao ya chakula na mazao ya biashara ni alizeti, vitunguu, pamba, ufuta na choroko lakini wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo:-
(i) Pembejeo zisizokuwa na viwango;
(ii) Bei kubwa ya pembejeo na zana za kilimo;
(iii) Uhaba wa wataalam na mashamba darasa ambayo husababisha uzalishaji kuwa mdogo;
(iv) Ukosefu wa mitaji na mikopo kwa wakulima;
(v) Ruzuku ndogo ya pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi zilizotajwa hapo juu zinakatisha tamaa vijana na wanawake wengi ambao wana hamasa kubwa ya kujikita katika kilimo cha kisasa lakini wanashindwa kufanya hivyo na kukimbilia mijini wakidhani huko ndiko kwenye maisha bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani ndiyo watu muhimu wa kuwapa mbinu bora za kilimo na hasa wakulima waliopo vijijini lakini Mkoa wa Singida una uhaba mkubwa wa maafisa hawa. Kwa Wilaya ya Iramba wako 79 wakati mahitaji ni 324; Wilaya ya Singida Vijijini mahitaji ni 188 lakini waliopo ni 45; Wilaya ya Mkalama mahitaji ni 185 na waliopo ni 38 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya uwepo wa Maafisa hawa wachache lakini nao wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi kama vile pikipiki na hivyo kushindwa kuwafikia wakulima wengi huko vijijini. Ni vyema Serikali ikaangalia jambo hili kwa kina kwa kuongeza Maafisa Ugani wa kutosha katika Halmashauri zetu kwa kuwa maafisa hawa ni kiungo muhimu katika kuyafikia maendeleo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nieleze masikitiko yangu juu ya mgao mdogo wa ruzuku ya pembejeo kwa Mkoa wa Singida kwa msimu wa mwaka 2016/2017 ambapo Serikali ilitupa tani 20 za mbegu ya mahindi na tani 100 za mbolea ya kupandia/kukuzia ambayo ni sawa na asilimia 0.29 ya mbolea kwa mahitaji ya mkoa mzima. Hiki ni kidogo sana kwa mkoa kwani mahitaji yetu ni kuanzia tani 33,000 hadi tani 40,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa inayolima mazao ya mafuta, kwa Mikoa ya Pwani ni nazi, kwa Mkoa wa Kigoma ni mawese, kwa Singida na Dodoma ni alizeti lakini Serikali haijalitaja zao hili kama zao la kimkakati ili tija iweze kuonekana na hata mpango wa SPDA II haujatilia mkazo zao hili. Kwa msimu uliopita, takribani tani 58,000 ziliuzwa nchini Congo ambazo ziliingiza zaidi ya shilingi bilioni 1.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo zao hili litatiliwa mkazo, uzalishaji utaweza kuongezeka lakini wakulima hawa wa alizeti wamesahaulika, wengi hawana mbinu mpya bado wanatumia mbinu za zamani ambazo husababisha uzalishaji mdogo hata viwanda vilivyopo vya kuchakata alizeti havina viwango vyenye ubora wa kutosha. Iwapo Serikali itaviendeleza viwanda hivi vitaweza kuzalisha mafuta mengi yenye ubora wa kuweza kuuzwa ndani na nje ya nchi. Ifike wakati sasa Serikali iwatazame wakulima wa zao la alizeti kwa kuwapa mbegu bora za F1, utaalam wa kilimo cha kisasa na ruzuku ya pembejeo ili kukiboresha kilimo hiki cha alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mfumo wa manunuzi wa pamoja wa pembejeo (bulk procurement). Naipongeza Serikali kwa kubuni mfumo huu kwani utamaliza matatizo yaliyopo katika mfumo wetu wa sasa. Wakulima wetu wameteseka sana kwa kulanguliwa na kuuziwa pembejeo zisizo na viwango kama ilivyotokea msimu uliopita wakulima wa pamba Singida walipata hasara kubwa. Hapa naishauri Serikali kuangalia mambo matatu kwa kina ili kufanikisha mfumo huu. Moja, ni udhibiti wa bei, ubora wa pembejeo na mahitaji kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nashauri Serikali kujikita katika kilimo cha umwagiliaji na hasa katika Mkoa wa Singida ili wananchi wa mkoa huu waweze kulima kwa msimu wa mwaka mzima kwa kuwa jiografia yake ni mkoa wenye ukame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake.