Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini. Naipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kufuta kodi zenye kero kwa wakulima na wavuvi wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kero kubwa ya taasisi ya Serikali ya Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA) kwenye mgao wa maduhuli yatokanayo na watalii wanaoingia katika maeneo ya hifadhi, Halmashauri ya Mafia inapata asilimia 10 ya pato halisi, yaani baada ya kutoa gharama za uendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza asilimia 10 ni kiwango kidogo sana ukizingatia mzigo unaobebeshwa na Halmashauri kwenye kuendesha shughuli za afya, elimu na miundombinu. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri yeye ndiye mwenye kutengeneza kanuni, kwa kipekee tunamwomba sasa aridhie ombi letu la kubadili kanuni ili kiwango hiki kiongezwe kutoka asilimia 10 mpaka kufikia asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni hili la pato halisi (net income), baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji za hifadhi ya bahari zikiwemo semina, safari, likizo na malipo ya ziada, baada ya saa za kazi ibaki zile gharama za kukusanya mapato tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uwekezaji unaofanywa na hifadhi ya bahari katika visiwa vya Shungimbili, Mbarakuni na Nyororo. Kimsingi sisi watu wa Mafia hatupingi mwekezaji, bali namna ya uwekezaji na mchakato mzima ndiyo unaacha maswali mengi bila majibu. Kitendo cha kutowashirikisha wananchi hakikubaliki hata kidogo. Ni ushauri wetu kwamba suala la mwekezaji liachwe kwenye ngazi ya Halmashauri kutoka hifadhi ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ongezeko la vijiji vya eneo la hifadhi ya bahari. Hifadhi ilianza na vijiji vinne tu, lakini leo imeongezeka mpaka kufikia vijiji 13 na Wilaya ya Mafia ina jumla ya vijiji 23. Ukweli huo zaidi ya nusu ya vijiji ipo chini ya himaya ya hifadhi ya bahari na sasa wananchi wanakatazwa hata kulima mbali ya kuvua. Kilio chetu ni kwa nini mchakato wa kuongeza vijiji vya eneo la hifadhi haikushirikisha wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubinafsishaji wa kisiwa cha Nyororo na Mbarakuni usitishwe mara moja kwa maslahi ya Taifa hili ili kasa waweze kupata maeneo ya kutagia mayai yao, kuokoa kiumbe huyo asipotee katika sura ya nchi yetu.

Mheshimiwa Waziri, Meneja Mkuu wa Hifadhi ya Bahari awajibishwe kwa kosa la kuuza kisiwa cha Shungimbili kinyume na utaartibu wa kushirikisha wananchi na mwekezaji kujenga bila ya kuwa na kibali cha ujenzi (building permit). Vilevile huyu Meneja Mkuu alimwongopea Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara ya kiserikali Mafia kuwa Halmashauri ya Mafia haidai hifadhi fedha za maduhuli, lakini baada ya Waziri Mkuu kuondoka, Hifadhi ya Bahari walilipa Halmashauri shilingi milioni 44. Kitendo hiki cha kumdanganya kiongozi mkubwa huyu mbele ya Mkuu wa Wilaya ni kitendo cha utovu wa nidhamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.