Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja na kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo wamekuwa wakizifanya. Umuhimu wa kilimo hauna maelezo, kwani unachangia asilimia 29.1 ya pato la Taifa na kuleta ajira kwa asilimia 65.5 kutokana na asilimia kubwa hususan vijijini kujishughulisha na kilimo. Aidha, napongeza kodi/tozo ambazo zimeondolewa, hiyo itawapa afueni kubwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana na kushangaa kutokana na fedha za maendeleo kupelekwa kidogo mno, yaani asilimia 3.31 ya fedha zilizoidhinishwa. Naomba tuweke umuhimu na kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga tunalima mazao mengi ya biashara kama katani, nazi, korosho machungwa, viungo na kadhalika; lakini pamoja na Serikali kufuta hati za mashamba ya mkonge Wilayani Muheza, bado Wizara haijaonesha juhudi za kufufua zao la katani na kulifanya kuongeza pato la Taifa kama zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi zinaendelea kufanyika kwa Maafisa Kilimo kuendelea kutoa elimu Wilayani Muheza, namna bora ya kulima machungwa, minazi na viungo vya chai na kadhalika wakati tunaendelea na mihogo kutafuta wawekezaji wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahishwa sana na ulimaji wa korosho ambapo Serikali imewapa wakulima pembejeo bure, jambo ambalo litaongeza ari ya kulima kwa bidii. Tunaomba Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho afanye mipango ya kutuletea mbegu Wilayani Muheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifikirie namna ya kutoa mbegu na mbolea bure kwa baadhi ya mazao, hii itawaongezea motisha wakulima. Kwa mfano, kuna wakati nchi ya Malawi ilifanya hivyo na walivuna mahindi mengi sana na kuongeza pato lao la Taifa. Aidha, nchini Zimbabwe pia waliwahi kuwakopesha wakulima zana za kilimo na wakaongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ubora wa mazao, pia Wizara inabidi isaidie sana wakulima. Ubora wa mazao yetu ukilinganisha na nchi nyingine kwa baadhi ya mazao, bado tunahitaji wataalam wetu walifanyie kazi. Kwa mfano, zao la pamba tunakosa kupata bei nzuri kutokana na ubora na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Kilimo cha Mlingano cha Utafiti kinakufa, kwani Chuo hicho hakipelekewi fedha kabisa na mambo mengi yako ovyo. Tunaomba wapelekewe fedha chuo hicho kifufuke. Muheza tunafuga sana ng’ombe. Kiwanda cha Tanga Fresh kinategemea sana maziwa kutoka kwa wafugaji wa Muheza, namshauri Mheshimiwa Waziri atutumie wataalam wake wawasaidie wafugaji hawa kuongeza maziwa kitaalam na pia namna ya kuwapatia mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umwagiliaji bado tupo nyuma sana. Inabidi tufanye kazi tuweze kuwa na mashamba makubwa na ya kisasa. Tutumie zana za kileo za umwagiliaji. Tukitaka kuwa na kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda, ni vizuri Mawaziri husika kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara kama Waziri wa Kilimo, Ardhi, Maji, Nishati, Umeme na Fedha.