Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Wabunge wote waliochangia Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda nitaongelea suala la upungufu wa chakula kwa baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ukweli baadhi ya chakula kilichopo kwenye maghala na mashine za kukoboa mpunga ni chakula cha watu binafsi ambao wengi ni wakulima waliopata mavuno mengi mwaka jana, ambao ni kama asilimia15 ya wananchi hao wa vijijini na wakulima hawa ama hawataki kuuza kwa hofu ya njaa au wanasubiri bei zaidi isiyojulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu chakula hiki mpaka leo ni kingi sana kama kingekuwa cha Serikali lakini ni cha watu binafsi, kwa hiyo huenda hata takwimu zikatofautiana kadri muda unavyoenda. Itakumbukwa hata wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Wilayani Kahama nilimwomba awaruhusu wauze mchele wao nje maana soko la ndani lisingeweza kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna asilimia 25 ya wananchi ambao wanategemea kuuza mifugo yao ili wanunue chakula, lakini bei ya mifugo haipo kupelekea kurudi na mifugo yao toka minadani au magulioni bila kuuza na kuongeza hofu kubwa ya maisha kwa wananchi hawa hasa ikizingatiwa wanakabiliwa na ukame pia kwa ajili ya malisho na maji kwa ajili ya wao na mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya wananchi ambao wakiwemo watoto, wazee, wajane na watu wenye ulemavu mbalimbali na watu ambao ni maskini kabisa kundi hili ndilo linahitaji msaada wa dharura. Ni ukweli watu hawa walipata mavuno mwaka 2015/2016 lakini baada ya ukame wa mwezi wa Novemba – Desemba na Januari kuwa mkubwa ikapelekea mavuno machache na viwavi jeshi vikala kidogo kilichokuwepo kuwapelekea kupitia kipindi kigumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa historia na jiografia ya maeneo haya hakuna sehemu yoyote wanaweza kupata pesa ili waweze kununua chakula hata cha bei nafuu, hawana mifugo, hawana ndugu wa mjini ambao wanaweza kuwasaidia na hakuna hata sehemu ya kufanya kibarua ili waweze kupata pesa wanunue chakula, ikizingatiwa watakuwa kwenye njaa kuanza Juni – Januari ambapo kama hali ya hewa itabadilika katika maeneo haya ambayo ni karibu miezi saba mpaka nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri anapofanya majumuisho yake aje na jibu sahihi ili Wabunge wanaotoka maeneo haya yaliyoathirika na ukame tuwe na majibu sahihi kwa watu wetu, vinginevyo nitakamata shilingi ya bajeti.