Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nampongeza Waziri na timu yake kwa hotuba na bajeti nzuri. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii kwa wapiga kura wangu ambao huko Muleba Kusini ni ama wakulima ama wafugaji ama wavuvi, nitachangia vitu muhimu katika sekta hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo huko Muleba Serikali ni kama imetusahau, hatuna wala hatuoni jitihada za Serikali kuwaendeleza wakulima wa kahawa na wakulima wa migomba, maharage, mihogo, viazi vitamu na kadhalika. Nasema hivi nikiwa pia shahidi kwani nami ni mkulima. Sijamwona bwana shamba wa Wilaya akipita kuangalia hali ya mazao. Rais wetu mpendwa ameelekeza msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Sijui tatizo la hawa Mabwana Shamba ofisi na Mabwana Shamba mashamba, Mheshimiwa Waziri anatusaidiaje na je, tatizo lao ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri awasikilize nao wamweleze tatizo lao, wakulima hatuna msaada sana wa Ofisi ya Kilimo Wilayani. Haigawi pembejeo, haitoi utaalam, haitutembelei kujua tatizo ni nini. Serikali, tena ya Awamu ya Tano itusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wanahitaji ardhi, lakini watu wameongezeka na ardhi inazidi kupungua kwa uwingi wetu na uwingi wa mifugo. Kwa hiyo, land pressure, uhaba wa ardhi hivi sasa ni mojawapo ya matatizo yanayoikabili nchi hii. Juhudi za Rais wetu kuendeleza viwanda zitasaidia kupunguza land pressure kwani vijana watapata ajira viwandani, kwa sasa viwanda bado, pamoja na hatua nzuri za uhamasishaji zinazoendelea. Kwa hiyo, vijana wanahitaji kupewa ardhi, ili wajiajiri katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itueleze ina mpango gani kuorodhesha vijana wote wasio na ardhi waume kwa wake ili wapewe ardhi na kujiajiri katika kilimo. Kuwaacha wazazi peke yao ndiyo wahangaike kuwapatia vijana wao ardhi kuanzisha mashamba ya kisasa haitasaidia. Mheshimiwa Waziri anatambua bila kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na umwagiliaji viwanda vitashindikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna viwanda bila malighafi na malighafi inatokana na kilimo. Naomba Serikali na Waziri anapohitimisha anieleze mpango wa kuwapatia ardhi vijana wa Kata za Muleba ambazo ni Kushasha, Ijumbi, Nshamba, Biinabo, Ikondo na Kibanga, Bereza na Muleba kuhamishwa na kupewa mashamba ukanda wa Ziwa Burigi. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili alichukue na kulifanyia kazi. Vijana katika Kata hizi wana haki ya kuhamia Mjini kwani hawana pa kwenda, hawajakataa kulima ni landless, hawajawezeshwa, tunaomba youth resettlement program ndiyo hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake Muleba hatumiliki mashamba ya migomba au vibanja, ni mali za ukoo kwa kawaida, lakini wanawake tuna jukumu la kulima mfano mahindi, maharage, karanga, kwenye grass lands au nyeya. Sasa uhaba wa ardhi umefanya mashamba ya migomba pamoja na miti kupanuliwa hadi kwenye hizo nyeya, matokeo yake wanawake uchumi wao na lishe vinakosekana kwenye familia kwa kukosa mikunde, legumes, ambayo inatoa protini, isitoshe zile sehemu ndogo zilizobaki wanapolima na mifugo nayo haina sehemu za malisho. Mheshimiwa Waziri naomba atueleze ana utaratibu gani kuwapatia wafugaji maeneo ya kuendeleza ufugaji wa kisasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji hawana maeneo, wapo kwenye mapori ya akiba siyo kwa kupenda, bali kuepuka migogoro na wakulima. Nasikitika kutamka bayana kwani Serikali na hasa ndugu yangu Mheshimiwa Tizeba, jambo hili ama hajaonekana kulielewa au anaamini propaganda za wanaonufaika kwa kudai rushwa kutoka kwa wafugaji katika mapori ya akiba kwamba, mifugo ni ya Wanyarwanda na Waganda huko Kagera. Naomba Serikali ilete taarifa zake katika jambo hili katika uwazi ili ukweli ambao Rais anahimiza ujulikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtandao muovu unaoeneza propaganda hizi na wananchi tuko tayari kueleza ukweli. Tanzania ya viwanda haiwezi kushamiri bila kupunguza eneo la hifadhi kutoka asilimia 28 ya sasa na kugawa kiasi cha kutosha kwa wafugaji ili wapewe hati ya ardhi kukopesheka na kuanzishwa small scale ranching association. Hakuna njia nyingine, kupora mali za wafugaji kwa kutaifisha mifugo yao bila kutuonesha hiyo mifugo imenunuliwa na nani na imehamishwa kwenda wapi baada ya kunadiwa huko porini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutuhadaa, kusababisha umaskini badala ya kuuondoa. Kuswaga mifugo kutoka mapori ya akiba kuzingatie agizo la Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa Wakuu wa Mikoa kwamba, wabaini maeneo ya ufugaji kabla ya zoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, wavuvi wasisumbuliwe na nyavu ndogo wakati hawahusiki na viwanda vinavyozitengeneza na kuziingiza nchini. Ziwa Victoria ni hazina ambayo haijapewa kipaumbele. Mheshimiwa Waziri anajua usalama wa wavuvi hautoshi, majambazi yanapora na kuua. Serikali inaombwa kuendelea kutumia vyombo vyake katika eneo hilo. Aidha, utaalam wa ufugaji wa samaki katika ziwa lenyewe bila kuathiri mazingira ni jambo ambalo litahitaji utafiti wa Serikali kuonesha njia kama sehemu ya kuendeleza viwanda vya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.