Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wote kwa pamoja kwa uchapakazi wake katika kuhakikisha Wizara hii nyeti yenye kuwagusa wananchi kwenye masuala ya kilimo, uvuvi na ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia suala la tumbaku. Tumbaku ni zao linaloingizia sana kipato Taifa letu, ukizingatia hata wanunuzi hununua na pesa ya kigeni yaani dola, lakini tumekuwa na tatizo kubwa na middleman wanaokaa katikati ya mkulima na mnunuzi, hawa wamekuwa wakisababisha wakulima kupata bei za chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirika. Tunaomba Wizara iimarishe vyama vya ushirika vya kilimo na mazao. Nashauri pia, sambamba na hili nizungumzie pia mikopo ya pembejeo. Sote tunatambua vyama vya ushirika wa mazao kama vile, mazao ya tumbaku, pamba, korosho, kahawa, michikichi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua jitihada za Serikali za kuanzisha Benki ya Kilimo. Kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kuweka matawi kwenye Kanda zote nchini ili basi wakulima wetu huko Majimboni waweze kupata fursa ya kukopa na kuendeleza mashamba yao. Uimarishaji wa mazao baada ya mavuno na kuongeza upatikanaji wa masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu uvuvi. Zao la uvuvi ni zao ambalo likifanyiwa kazi na kuwekewa mkakati wa kuwakopesha wavuvi zana za uvuvi kama maboti, mashine, nyavu za kisasa na kadhalika, lingeingizia Taifa letu kipato kikubwa. Mfano, nimeona ukurasa wa 18 Mheshimiwa Waziri kaonesha idadi ya samaki waliopo kwenye Ziwa ya Victoria, tani 2,451,296 Ziwa Tanganyika tani 295,000 na Ziwa Nyasa tani 168,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna tani zote hizi tungeweka mikakati ya makusudi ya kuvua samaki hawa na kuuza nje ya nchi tungepata kipato kikubwa cha Taifa, lakini nijuavyo mimi idadi hii ya samaki waliopo Ziwa Tanganyika ya 295,000 siyo ya kweli. Tuombe Serikali ifanye utafiti wa kina wa kujua idadi kamili na siyo kubuni tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma walikuja watafiti kutoka China na walifanya utafiti na kugundua Ziwa Tanganyika lina samaki wengi na lina aina ya samaki zaidi ya 250. Iweje leo utafiti uoneshe idadi hiyo ya 290,000. Tuombe utafiti ufanyike na kumbukumbu stahiki ziwekwe kwa faida ya nchi na faida ya vizazi vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zao la uvuvi kwenye tozo. Wavuvi wamekuwa wakitozwa tozo kubwa na nyingi, tuiombe Wizara ione namna ya kutoa maelekezo (Waraka) kwenye Halmashauri zetu ambako Maafisa Uvuvi ndiyo wako huko. Tuombe pia, Wizara iangalie zao la michikichi, zao hili lina faida kubwa na Kigoma ndiyo mkoa unaoongoza kulima zao hili. Zao hili lina faida kubwa, zao hili linatoa mafuta ya mawese (palm oil) na mbegu zake zinatoa mafuta ya Korea na pia linatoa sabuni za miche na sabuni za maji. Naamini utafiti ukifanyika wanaweza kupata faida nyingine nyingi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waziri aone namna ya kutoa miche bora ya michikichi ya muda mfupi wa miaka mitatu kwa bei nafuu kwani bei wanayouziwa wakulima, mche mmoja Sh.5,000/=. Eka moja inahitajika miche 50, swali ni wakulima wangapi wana uwezo wa kununua miche hiyo bora? Kuna ulazima wa kupata ruzuku ya miche hii ili wakulima wang’oe miche ya zamani na kupanda miche bora inayokua kwa miaka mitatu kama wenzetu wa zao la korosho wanavyoweza kupanda miche bora ya muda mfupi na leo zao la korosho limeingizia wakulima pato kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie migogoro ya wakulima na wafugaji kwenye Jimbo langu la Kigoma Kusini, Wilaya ya Uvinza. Mheshimiwa Waziri Wilaya ya Uvinza tunavyo vitalu vingi sana kwenye ranchi ya Uvinza. Vitalu hivi vingegawiwa kwa wafugaji wa Uvinza au wenyeji wa Uvinza, lakini cha ajabu vitalu vyote vimegawiwa kwa wageni toka mikoa mingine wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni aliwahi kutoa tamko vitalu vyote kwenye ranchi viangaliwe na vigawiwe kwa wenyeji wa maeneo hayo ili kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri akija kuhitimisha aniambie waliopewa vitalu kwenye ranchi ya Uvinza na je, kuna vitalu vilivyobaki ili basi mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Uvinza nijue na mwisho Waziri atakuwa tayari kunipa majina ya wamiliki waliogawiwa hivyo vitalu na maeneo yaliyobaki ili basi niweze kushauri jinsi ya kuvigawa vilivyobaki ili kupunguza migogoro ukanda wa reli na ukanda wa Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.