Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL J. PAPIAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza napongeza kazi inayofanywa na Wizara na watalaam wake na pili nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi anayoifanya na jitihada nyingi zote za kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo imetengwa hii ya shilingi bilioni 600 ambayo tunalalamika kwamba iende shilingi bilioni 900, mimi ninaona kwamba Wizara imepanga bajeti ambayo ndiyo halisi, kwa sababu hata hii shilingi bilioni 600 yenyewe tukisema leo tuiombe yawezekana hizo fedha zisifike. Fedha ambazo zimetoka ni chini, asilimia 19, ina maana kwamba hata hii tukiiomba yenyewe yawezekana isiwe halisi. Sasa mimi niombe na kushauri kwamba Bunge lako hili likubali tutengeneze ile shilingi 50 iongezeke kwenye mafuta ambayo ndiyo pesa halisi ambayo yawezekana ikawa ni halisi ya kwenda kupeleka kwenye miradi yetu ya maji, angalau ikaongeza Mfuko wa Maji kupata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wa wizara wanafanya kazi kwa nguvu kubwa, lakini huku chini kwenye halmashauri zetu watendaji wa Idara za Maji hawafanyi kazi ipasavyo. Idara ya Umwagiliaji Wizarani kuna tatizo la watu kukaimu, watu wengine wamestaafu. Hili suala la umwagiliaji nchini naomba litizamwe kwa kiwango kikubwa, suala la kukaimu linasababisha watu kushindwa kufanya kazi na kufanya maamuzi kwenye maeneo yao. Wale waliostaafu, kama hakuna watu wengine ambao wamewarithi ambao mmekuwa trained na kujua namna ya umwagiliaji nchini basi wale wapewe contract kwa muda wafanye training ya hao wengine ili waweze kusukuma kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa linalofanya nchi yetu ipoteze fedha nyingi ni tathmini ya miradi ya maji kuwa gharama kubwa sana. Mradi mdogo wa shilingi milioni 20 mtu ana tender shilingi milioni 200, hizi fedha zinavyotoka inalazimisha mradi kuwa nusu nusu na haifiki mwisho na mwisho wa siku miradi mingi ya maji nchini inakuwa viporo na haifiki mahali inapotakiwa.
Kwa hiyo tunaomba tulitazame hili, lakini kwenye tendering documents Wizara iangalie, Serikali iangalie ni namna gani tunaweza kwenda kwenye uhalisia unaoweza kufanya miradi hii iweze kukamilika na fedha za Serikali zisiweze kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafadhili, miradi mingi ambayo inakuwa supported na wafadhili mimi nadhani hawa wafadhili na wenyewe kuna jinsi wanatupiga chenga. Leo wameleta fedha, kesho wameahidi, keshokutwa wame- cancel, miradi haiwezi kuendelea, hii ni danganya toto. Nchi ijitizame upya ni namna gani tunaweza kutokana na haya masuala ya wafadhili, asubuhi amekushika tai, jioni amekuachia tunakuja Bungeni tunaahidi vitu ambavyo haviwezekani. Tujitizame upya tupunguze hili suala la utegemezi wa wafadhili ambao wanatufikisha mahali ambapo sipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kiteto wameniomba niiombe Wizara ya Maji, maeneo ya Ndido, Makame, Loolera tupewe bwawa moja angalau kwenye hii tarafa ili basi wale wafugaji wapate maji. Kanda hii ya maeneo ya hizi kata tatu hawahitaji maji safi na salama, wanahitaji ilimradi ni maji, ukinywa usiharishe, usife, ng’ombe wasife, yawe meupe, yawe meusi, yawe blue wao wanahitaji kitu kinachoweza kuitwa maji na Serikali ikawaambia haya ndiyo maji, kwa sababu wamelia miaka mingi hakuna mabwawa, mifugo inakufa, wananchi hawawezi kupata maji ya kutumia. Maji haya yote sisi tunayatumia kwa maana ya binadamu na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza na naomba Wizara yako kwamba tupate bwawa moja la maji kwenye tarafa moja kwa mwaka huu, hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunaomba, kuna mabwawa ambayo wananchi wanachimba wenyewe; ukichukua fedha Wizarani, ukaangalia namna gani ya ku- rescue situation kwa haraka, uka-fund wale watu wanaochimba yale mabwawa kwa mikono yao tunaweza
kuwa na mabwawa madogo madogo kwenye maeneo ambayo wakati Serikali haijapanga ile miradi mikubwa basi wananchi wana mabwawa madogo madogo ambayo wanaweza kuwasaidia maji kwenye maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nishukuru kwa Bwawa la Dongo ambalo limeingizwa kwenye mpango, lakini niiombe Serikali…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.