Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na neno la shukrani. Shukrani hizi nazielekeza katika maeneo matatu. Nimeanza na neno la shukrani nikizingatia na Mheshimiwa Rais wetu alianza na neno la shukrani, kwa maana kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, nikiamini yeye ndiye muweza pekee na nafahamu ndugu zangu kutoka kule Jimbo la Mpanda Mjini sikuyaweza kwa nguvu zangu, ni kwa uwezo wake yeye Mwenyezi Mungu, kupitia kwa waja wake ametusaidia leo kuwepo mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme nikiungana mkono na Mheshimiwa Rais, nitawashukuru wananchi hawa, lakini namna ya pekee ya kuwashukuru ni kuwafanyia kazi na ndiyo maana hata Mheshimiwa alijikita katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani hizo naomba nizielekeze kwa wananchi wote kwa ujumla wao. Tutasema maneno mengi, lakini utulivu tuliouona wakati wa uchaguzi ni kwa sababu wananchi walikuwa tayari kushiriki uchaguzi ule na kutoa amani hiyo tunayoendelea kuiona hapa. Kwa hiyo, naomba na nikiamini mwananchi ndiye bosi wangu, ndiye Afisa wangu, hivyo, naendelea kuwashukuru wananchi hao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwashukuru viongozi mbalimbali wa dini, lakini naomba nivishukuru vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama. Katika hili naomba niwe muwazi, nimeushuhudia weledi hasa kule kwangu Katavi, Askari Polisi na vyombo vingine vingine vya
dola vimeshiriki kutufanya tushiriki uchaguzi salama. Kwa hiyo, nisipowashukuru nitakuwa siwatendei haki. Viongozi wa dini nafahamu kwa muda wote wamekuwa wakiliombea Taifa hili, nchi hii amani, kwa hiyo, nimesema ni vizuri nikiwashukuru hawa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu, amejikita kwenye ahadi na kuna neno moja zuri ambalo nimelipenda katika rejea yake, ametuambia, anaomba atutoe wasiwasi, tulivyoahidi tumeahidi na anaahidi kwamba ahadi ni deni. Hili ametukumbusha sisi Wabunge,
lakini akawakumbusha wenzetu ambao ni Madiwani, tumeahidi na ahadi ni deni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukimkuta kiongozi mkubwa kama huyu analizungumza hili na hakuna kitu kingine ambacho nimeendelea siku zote kukifuatilia na nikasema huyu mtu kweli Mwenyezi Mungu kamsimamia, pale ambapo muda wote anamtanguliza Mwenyezi Mungu na
anasema katika haya yote mema ya kuifanyia nchi hii tumuombee. Naamini, hakimu mwenye haki ni Mwenyezi Mungu, ndiye pakee atatusaidia kumlinda Mzee huyu ili atimize azma ya haya ambayo amekusudia kuwafanyia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe ndugu zangu Wabunge, lakini niwakumbushe Madiwani tunayo kazi, tuna ahadi kwa watu wetu, wananchi kwa sasa hivi wameendelea kuonyesha utulivu. Nimekuwa nikisikiliza kupitia vyombo vya habari, ukipita katika makundi
mbalimbali, wanatushauri wanasema hata mkibahatika kuwepo hapo jengoni, hebu toeni nafasi ya utulivu kwa Mzee huyu ili tuone ataifikisha wapi nchi yetu. Kwa hiyo, niwaombe sote tuliopo hapa, tutoe nafasi, hata namna yetu ya kuchangia, kushiriki katika shughuli mbalimbali,
tutoe nafasi ili tuone wapi tutaipeleka nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba nijikite katika suala la amani na utulivu. Tuna wajibu wa kuilinda amani, ni wajibu wetu mkubwa kuilinda amani na nashukuru katika hotuba yake Mheshimiwa Rais amezungumzia hatokuwa na simile kwa wale atakaochezea amani na utulivu wa nchi hii. Kwa hiyo, ili tuweze kujikita kwenye suala la viwanda, ambayo ni azma kubwa ya kuitoa nchi hii kuifikisha kwenye uchumi wa viwanda, bila amani na utulivu hatuwezi tukafika huko. Nilikuwa najaribu kuangalia usemi mmoja wa Kichina, lakini tafsiri yake ni ya Kiswahili unasema hivi; nikisikia nasahau, nikiona nakumbuka, nikitenda naelewa au nafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunasikia habari ya Mheshimiwa huyu kuhusu suala zima la kwamba hapa ni kazi tu, watu wakawa wanasahau, lakini baada ya kuona yale anayoyafanya sasa hivi kuhakikisha mapato ya nchi hii yanapatikana na maeneo mengine watu wamekumbuka, ahaa, kumbe yale tuliyokuwa tunasikia ni sahihi, lakini kwa hili ambalo tunaendelea kuliona elimu bure ambayo ni matendo yametendeka sasa hivi, ndio tunaendelea kufahamu kwamba Mzee huyu anamaanisha na anatembea kwenye yale aliyokuwa akiyasema.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la elimu, nishukuru kwa sababu zifuatazo:-
Tunapo zungumzia habari ya elimu bure changamoto haziwezi kukosekana, huu ni mwanzo, tumeanza na hilo na changamoto ni kitu cha kufanyia kazi. Siku zote ni muumini wa jambo moja, unapokuwa ni mtu wa kulalamika muda wote, wewe unakuwa ni sehemu ya tatizo, kwa hiyo naogopa kuwa sehemu ya tatizo, niwe sehemu ya kutatua tatizo. Kwa hiyo, changamoto tutakazoziona katika suala zima la elimu bure ambayo hiyo ni sehemu ya kuchangia hotuba ya baba huyu. Nasema kwamba tukiwa wawakilishi wa watu tutakuwa na wajibu wa kusema hapa, maana ukiwa na chai kama haina sukari utafanya zoezi la kuongeza sukari na kama sukari imezidi, unaweza ukaongeza hata maji, lakini tofauti na kutokuwa na chai kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la huduma ya afya, nishukuru na niseme kwamba, kule ninapotoka Katavi eneo hili la huduma ya afya ni jambo muhimu. Watu wetu akinamama na watoto, wazee tuendelee kama alivyozungumziwa Mheshimiwa Rais kuangalia makundi hayo,
kuangalia akinamama, watoto na wazee na ile sera yetu ya afya bure kwa makundi hayo tuendelee kuizingatia na naomba niendelee kumkumbusha Mzee huyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la barabara, bila kuiunganisha nchi hii na ninashukuru hata kiongozi aliyepita aliongelea habari ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, mikoa na maeneo mengine ya Wilaya kwa maana ya barabara kwa kiwango cha lami. Mimi ndugu yenu
ninayetoka Katavi, mkoa ambao leo hii tuna zaidi ya tani 3000 za mazao, natamani kuona mazao haya yakienda kwa Watanzania wengine waliopata uhaba wa chakula, lakini ili tuwafikishie ni kwa kuiunganisha eneo lile na barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hapo niseme Mheshimiwa kwa nia yake njema na nashukuru aliniambia ndugu yangu Kapufi ukibahatika kuwa Mbunge, kanikumbushe katika haya. Naendelea kusema alilolisema kuhusu barabara ni jambo jema, aliyoyasema kuhusu maji
ni mambo mema, aliyoyasema kuhusu afya ni mambo mema na wakati akiyafanya hayo akumbuke kule Katavi aliahidi suala hilo na ndio mkoa pekee uliobakia. Katavi, Kigoma na Tabora hatujaunganishwa kwa kiwango cha lami, tunatamani kuyaona maendeleo hayo na
kushiriki uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema, unapokuwa na sehemu nyingine anavunja barabara kwa sababu ni nyembamba ili aipanue, mwingine hata hiyo nyembamba hana, hapo ni eneo la kufanyia tafakari ya kina. Watu wa maeneo hayo wazalishaji wazuri eneo la
utalii wa nchi hii tuna maeneo mazuri ya kuweza kufanyia shughuli hizo za kitalii niendelee kumwomba Mzee huyu na kwa kuwa haya yote ameyaainisha katika hotuba yake kwamba, tutaangalia maeneo hayo ya utalii, tutaangalia masuala ya barabara na tutaangalia huduma za afya. Katika huduma za afya niendelee kumkumbusha Mzee huyu, tujikite katika vifaa tiba.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, najua kengele hiyo ni ya mwisho, nashukuru kwa kunisikiliza. (Makofi)