Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji. Kwa kuwa dakika ni tano nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi nzuri. Pia mchango wangu niuelekeze moja kwa moja kwenye Mradi wa Maji wa Wami – Chalinze Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na namshukuru sana, na maelekezo yake na namna ya maelezo ya Serikali kwenye hotuba hii, na namna ambavyo mkandarasi yule amepewa siku 100 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mradi wa awamu ya tatu; nilikuwa nadhani kwa kuwa changamoto za upatikanaji wa maji Jimbo la Chalinze zimekuwa kubwa, na kwa kuwa mkandarasi huyu anaonekana hata miradi mingine performance yake si nzuri, je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kumbadilisha mkandarasi huyu? Kwa sababu siku alizompa zinakamilika tarehe 31/05 na leo tuko tarehe 11?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa swali la nyongeza nililoliuliza juzi Mheshimiwa Naibu Waziri alinijibu amefikia asilimia 45. Hata hivyo mradi huu unakabiliwa na changamoto nyingi, maji yanayotoka sasa hivi ni machafu, wananchi wanapata taabu, maji hakuna na hata bili wanazopewa wengi wamekatiwa lakini wanaendelea kulipia service charge. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, na kwa kuwa Jimbo letu la Chalinze na Wilaya ya Bagamoyo kuna wawekezaji wengi wamejitokeza hususan, naomba nimsemee hapa mwekezaji wetu anayejenga kiwanda cha usindikaji matunda pale Msoga, Chalinze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuwa rasilimali inayohitajika ni maji na kwa kuwa maji sasa hakuna na kiwanda karibu kinafunguliwa, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kukubaliana na makubaliano ambayo yameingiwa mradi wa CHALIWASA pamoja na mwekezaji wetu huyu, kwamba yupo tayari kununua baadhi ya vifaa kwa ajili ya kuboresha mradi ule ili maji yapatikane ambayo mimi nadhani yanaweza yakasaidia kiwanda, yakatusaidiwa na wananchi wa Chalinze?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mradi wa Chalinze autazame kwa macho ya huruma, hali si shwari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwa kupitia bajeti hii kwenye hotuba yake nimeona kwenye ukurasa wa 90 mpaka 92 namna gani ambavyo Serikali imeonesha kabisa chanzo hiki cha shilingi 50 kwa lita moja ya diesel au petrol haitoshi. Kwa hiyo, nadhani kwa kukiri kwao kwenye hotuba hii sasa ni nafasi ya Bunge letu na Kamati yetu ya Bajeti kuweza kuongeza hicho kiwango ambacho Serikali yenyewe imekiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye ukurasa wa 120 Serikali imeonesha kwamba mahitaji ya ujenzi wa miradi mipya ya maji ni makubwa na wameomba wawekezajii wengine au wadau mbalimbali kujitokeza ku- support jitihada hizo na ndiyo maana hapa ninamwomba Mheshimiwa Waziri, nilishamweleza, hivi aone ombi la mwekezaji wetu kuomba kugharamia sehemu za ukarabati wa uchakavu wa miundombinu ya mradi wa maji Chalinze ili waweze kukatana kwenye bili. Kwa nini suala hili linachelewa hivyo? Uwekezaji ule ni zaidi ya bilioni mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wilaya ya Kisarawe nayo ina changamoto kubwa ya maji, Wilaya ya Rufiji nayo ina changamoto kubwa ya maji. Hivi karibuni kuna binti yetu amepoteza maisha kwa kuchota maji katika Mto Rufiji. Kwa nini sasa Mto Rufiji usitumike kuwa chanzo cha maji katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utaona miradi mingi, mfano mradi kupitia DAWASA, upanuzi wa bomba la maji Ruvu Chini na Ruvu Juu yote imepita katika Mkoa wa Pwani lakini kwa bahati mbaya sana hatuna Mamlaka ya Maji ya Mkoa, tunatumia mamlaka ya maji DAWASCO ambayo tunadhani inazidiwa na utoaji huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo, ningemwomba Mheshimiwa Waziri atueleze, ni kwa nini Mkoa wa Pwani tunakosa kigezo cha kuanzisha Mamlaka ya Maji, wakati ukizingatia vyanzo vingi vya maji vinavyopeleka maji katika maeneo mengine viko katika Mkoa wa Pwani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika kuongezea mchango wangu, kwa nini kata za Mzenga, Mafizi hazina maji wakati ni kilometa 28 kutoka bomba kuu la maji linalopeleka maji Dar es Salaam? Kwa hiyo, ningemwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba bajeti imepungua kwa kiwango hiki nadhani pia atakapokuja kufanya majumuisho atueleze pengine kuna sababu ya msingi. Pengine katika hiyo bilioni 600 tutaongeza maji kwa kiwango cha asilimia ngapi, na Watanzania wangapi wataongezeka katika kupata huduma ya maji kwa bajeti hii iliyopitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bagamoyo Mjini kuna miundombinu ya DAWASA imejengwa pale lakini hawapi maji. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashoria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)