Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuunga mkono hoja zote za Kamati ya Kilimo, Mifugo pamoja na Maji kwa sababu mimi ni Mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa ujumla kwa jinsi wanavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu makubwa ya Bunge ni kuishauri Serikali. Kamati yetu mwaka jana tuliishauri Serikali, tukaomba tuongeze tozo kutoka shilingi 50 kuwa shilingi100; lakini kwa bahati mbaya Serikali haikukubaliana na ushauri wa Kamati na mwaka huu Kamati yetu tena imeishauri Serikali, tuongeze tozo kutoka shilingi 50 mpaka shilingi 100. Haya yanajieleza wazi, tunaona kuna gape hapa, kama hii tozo ingekuwa imetozwa toka mwaka jana hili gape linalozungumzwa sasa hivi lisingekuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali iwe inasikiliza ushauri wa waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa naomba anieleze kwa nini Serikali ina kigugumizi cha kusaini mkabata wa Tanzania na Australia ambao ulikuwa unaweza kutoa maji katika majimbo matatu ya Wilaya ya Mufindi pamoja na Wilaya ya Kilolo, kwa nini Serikali inapata kigugumizi? Hela ziko wazi, tulichotakiwa ni kusaini tu ule mkataba; kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa naomba atupe majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Mufindi Kaskazini lina kata 11, lakini cha kusikitisha hakuna hata kata moja yanye maji. Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni zetu moja ya vipaumbele muhimu tulisema tupate maji, lakini ukienda kwenye kata za Ikwea, Sadani, Igombavanu, Ihalimba kote hakuna maji. Ifike wakati hawa Waheshimiwa wenzetu Mawaziri waje watusaidie kujibu hoja huko kwenye maeneo yetu, lini maji yatapatikana katika maeneo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mufindi miongoni mwa Wilaya kubwa hapa nchini, ina majimbo matatu, lakini cha kusikitisha tumepata bilioni 1.5 kwenye Jimbo la Mufindi Kusini, Mufindi Kaskazini pamoja na Mafinga Mjini. Kwa nini tunapata hela? Uwiano wa kugawa hii hela unapatikana vipi? Kuna baadhi ya maeneo zimekwenda shilingi bilioni 200, why? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike sehemu kuwe kuna uwiano ambao unaridhisha. Unakuta kuna maeneo mengine yanaonekana yako bora zaidi kuliko maeneo mengine. Waziri aje atwambie wanatumia vigezo gani kupeleka shilingi bilioni 200 kwenye maeneo mengine na kwenye eneo lingine hakuna hata senti tano? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya taasisi kama RDO zinafanya kazi kubwa sana za maendeleo katika maeneo yetu. Hii taasisi ya RDO inasaidia kuleta support ya maji katika kata ya Ndabulo, lakini kwa masikitiko makubwa sana Serikali hatuwaungi mkono. Inafika sehemu hata vifaa ambavyo vinasaidia kuleta maji katika maeneo yale vinachajiwa (be charged) VAT. Watu wanatoa maji bure kwa wananchi, leo tunaendelea kuwa-charge VAT. Badala ya kuwasaidia hawa watu tunawa-demoralise.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya World Bank kama miradi ya Ukami, Mapanda pamoja na Igomaa, mpaka leo mwaka wa saba miradi hii haijatekelezwa na hela zilishalipwa. Atakapokuja Waziri hapa atueleze kwa nini miradi hii haijakamilika na Serikali inatakiwa ichukue hatua gani kusudi hii miradi ikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mzee Pinda aliahidi kutoa shilingi milioni 295 kwa ajili ya kuendeleza bwawa la kilimo pale Nundwa, lakini mpaka leo hela hizi hazijatolewa. Kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri, baada ya bajeti hii aje atembelee kwenye maeneo yetu aone hali halisi katika maeneo yetu ili kusudi aweze kutusaidia watu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini na Wilaya ya Mufindi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja.