Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu, na kwa kuwa muda ni mfupi, naomba moja kwa moja niende kuunga mkono mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sababu za kuunga mkono hoja ni kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na watendaji wake chini ya Waziri, Mheshimiwa Engineer Gerson Lwenge, watendaji wote wa Mamlaka za Maji nchini wanafanya kazi ya kupigiwa mfano. Ni ukweli usiopingika kwamba Waziri na timu yake wako vizuri na wanafanya kazi nzuri, fedha zote wanazozipata wanakwenda kutekeleza miradi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, zipo changamoto mbalimbali ambazo Serikali inatakiwa izifanyie kazi na ninaomba niungane na Wabunge waliozungumza kwamba upo sasa umuhimu wa kuhakikisha fedha zote zinazotengwa na Serikali zinapelekwa kama zilivyopitishwa. Kwa sababu huwezi kumlaumu Waziri, huwezi kulaumu watendaji kama hujawapelekea fedha za kutosha. Tunatenga fedha hapa, lakini fedha haziendi kama zinavyokusudiwa na taarifa inaonesha imepelekwa kwa asilimia 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali kwa kuimarisha miundombinu ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani, lakini vilevile na Mkoa wa Mara.

Ushauri wangu, naomba niishauri Serikali, ule mradi wa maji Pwani – Dar es Salaam pia uhudumie wananchi wa Mkuranga na Kisarawe kwa sababu pia miundombinu inatoka kule. Vilevile niwapongeze kabisa kwa dhati Mamlaka ya DAWASA kwa kazi nzuri sana ya kusimamia miundombinu ya maji maana kama wasingejenga inawezekana pesa zingepotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee niwapongeze DAWASCO kwa kazi nzuri ya uendeshaji, na ushauri umetolewa kwamba ipo haja ya kuangalia mamlaka hizi na kuziunganisha na mimi naungana nao. Pamoja na hayo naomba nitoe angalizo kwa Serikali, tusikurupuke. Kwa sababu mimi ninayezungumza nilikuwa Mjumbe wa Bodi ya DAWASA miaka tisa na nyuma huko tulikuwa na NUWA na baadaye tukaja na City Water na baadaye tumekuja na DAWASCO, tuliona Mamlaka ya DAWASA ibaki ijenge miundombinu, itafute fedha isimamie miradi na DAWASCO wabaki kuwa waendeshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu, naomba kabla ya kufikia kuziunganisha hizi mamlaka hebu angalieni historia ilikuwaje mpaka zikawa sasa mamlaka mbili kwa lengo la kubana matumizi. Hoja ni nzuri, lakini tusikurupuke, tuifanyie kazi polepole ili tulete tija tusije tukarudi kule nyuma ambapo tulikuwa tumetoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishukuru sana Serikali kwa kuimarisha miundombinu katika Mji wa Musoma, naomba niishukuru sana maana sasa Musoma tunakwenda kupata maji ya kutosha. Ushauri wangu pale chanzo cha maji kinapotoka Mji wa Musoma kinatoka pia Musoma Vijijini. Ninaomba kata ya Etaro, kata ya Nyegina, kata ya Nyakatende na wenyewe wapate maji kutokana na chanzo kile. Tukiacha bila kupata maji wale wananchi wa lile eneo wanaweza wakaharibu ile miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba niongelee Mradi wa Bitiama – Kyabakari – Mgango, mradi wa kihistoria, mradi wa kwa Baba wa Taifa, sasa ni miaka 30 mimi nausikia mradi huu. Ni juzi hapa niliusikia wakati Mwandosya akiwa Waziri, amekuja Mheshimiwa Dokta Mwakyembe ameuzungumza, leo anauzungumza Mheshimiwa Engineer Lwenge.

Mheshimiwa wenyekiti, nimepitia kwenye kitabu hiki upembuzi yakinifu umemalizika taarifa imepelekwa BADEA, na mwaka uliopita ilikuwa ni hivyohivyo. Nataka leo Serikali ituambie, hivi kama leo BADEA hawatoi fedha Serikali ina mkakati gani na hasa kwa kuzingatia kule maji yanakwenda mpaka kwa Baba wa Taifa, Baba wa nchi hii ambaye ametufanya wote tuko kama hivi tulivyo? Wananchi wa kule wana adha kubwa sana, wamezungukwa na mito, wamezungukwa na maji, lakini hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu wote waliosema tozo ya maji iongezeke, na mimi naungana nao kwa sababu tumeona kile kiwango cha shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta imeleta tija sana kwa nchi yetu. Naomba iongezeke shilingi 100 ili wanawake wa Tanzania wapunguziwe adha wanayoipata, wanawake wanatembea umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti nimegundua hata wanawake wanaojifungua kabla ya kufikisha umri tatizo ni maji, hata wanawake wanaozaa watoto bila kufikisha umri tatizo ni maji, mimba zinazotoka mpaka watoto wanafariki ni maji kwa sababu wanatembea muda mrefu kwenda kutafuta maji wakati wataalam wanawashauri wapumzike. Vifo vya watoto wanaofariki chini ya miaka mitano asilimia 40 ni watoto wanaozaliwa kabla ya umri na tatizo kubwa ni kwa sababu wanawake wanafanya kazi za shurba. Ataenda kutafuta maji, arudi akalime, arudi akamuhudumie baba, arudi akapike. Jamani, sheria inasema ni umbali wa mita 400 tu, ninaiomba Serikali isiwe na kigugumizi katika kuongeza tozo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena tumefanya research kabisa sisi wenzenu tumekwenda, wananchi hawana shida kuongezewa shilingi 100, tena haitaleta madhara yoyote katika kuongezeka mfumuko wa bei na kuongezea wananchi mzigo wa maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu aliye na gari ni kidogo ana maisha mazuri na wananchi wakiona matokeo wako tayari kuchangia shilingi 100. Ninaomba tusiogope, hebu twende na mpango huu, ije Finance Bill hapa Bungeni tuipitishe kwa kauli moja twende kuwakomboa wanawake na wananchi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana, Mungu akubariki sana.