Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji


MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia japo muda kwa mfupi, lakini nitoe machache kuhusu hoja yetu iliyo mezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii kuungana na Wabunge wote na waliochangia kwamba Wizara hii ipewe fedha za nyongeza katika bajeti yake. Hatuwezi kuongea mengi. Waheshimiwa Wabunge wameongea mengi kuhusu matatizo ya maji katika nchi yetu. Maji yamekuwa ni janga katika nchi na nitashangaa Wabunge ambao wanasema bajeti inatosha. Bajeti haitoshi, iliyotolewa haikutosha, basi tuombe Serikali iweze kukubaliana na maoni ya Wabunge kwamba tozo ya sh.50 iongezwe ili tupate sh.100/= kutokana na lita za petrol na diesel. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo ambalo naona linatukabili sisi ni namna ya kusimamia fedha ambazo zitatolewa katika bajeti. Tunapoongelea miradi ya maji, siyo kwamba miradi ya maji haijawahi kuwepo. Inawezekana katika nchi yetu, tusingekuwa na kilio kikubwa cha matatizo ya maji kama fedha ambazo zilitolewa huko nyuma kutengeneza miradi ya maji katika kupitia mradi wa World Bank pamoja na ile miradi ya vijiji kumi, zingesimamiwa inavyotakiwa. Zingesimamiwa, ina maana tungekuwa tumepunguza kwa kiwango kikubwa matatizo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, pamoja na kwamba tunatoa kilio fedha ziongezwe, fedha hizi Waheshimiwa Mawaziri zisimamiwe ili tusije tukarudi kule nyuma kama ilivyokuwa katika miradi ya awali. Nashangaa pale watu wanapokuja hapa na kuimba nyimbo za kujisifu, lakini walioharibu na kushindwa kusimamia miradi hii ni Serikali iliyoko madarakani. Tunasifu Awamu ya Tano, lakini kulikuwa na ya Pili, ya Tatu na ya Nne. Ina maana wao walikuwa hawafanyi kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotaka ni kwamba miradi isimamiwe. Fedha tunazoomba kama Bunge tunawapa Serikali mafungu, basi mafungu hayo yasimamiwe kikamilifu ili miradi iweze kuleta matokeo mazuri na iweze kuonekana. Kwa mfano, kama sisi ambao Kamati zetu zinazunguka kutazama miradi hii, iwe ya umwagiliaji, iwe ya mabwawa ya matumizi, haifanyi kazi vizuri. Fedha zinatumika vibaya!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, aende pale Tabora, kuna ule mradi wa Nala, ni mabilioni ya pesa. Kuna miradi mingine ambayo Halmashauri inashindwa kulipa Wakandarasi na inapaswa ilipe fidia au ile hasara ya kuchelewesha kulipa. Kwa hiyo, unakuta Halmashauri hizi nazo zinajikuta zimeingia katika malipo makubwa kwa sababu ile miradi ya awali haikulipwa inavyotakiwa. Kwa hiyo, mambo yanakwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachoomba tulie kuongeza pesa, Serikali itusikie iongeze pesa hiyo, lakini isimamiwe inavyotakiwa ili miradi hii iweze kuleta matokeo mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka kusema ni kwamba katika mikoa mingine kwa mfano Mikoa ya Kagera, Mungu alikuwa ametujalia vijito vidogo vidogo ambavyo wanawake walikuwa wanavitumia kuchota maji, lakini vijito vyote hivyo vimekauka kwa sababu ya shughuli za kibinadamu katika hivyo vyanzo vidogo vidogo. Hii hali inapotokea, wanasiasa wananyamaza hasa katika ngazi ya Halmashauri. Hata ile Wizara inayohusika na Mazingira haichukui hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake, ile mito midogo midogo iliyokuwa inatiririsha maji mazuri ambayo watu walikuwa wanatumia kabla ya kupewa haya maji ya bomba, kulikuwa na hiyo mito, lakini sasa hivi yote imekauka. Imekauka kwa sasabu hakuna juhudi maalum za kuelimisha Watanzania, watu wamejisahau na mara nyingi wanasiasa wanaogopa kuchukua hatua kwa sababu ya kufikiria kwamba labda hawatachaguliwa tena.